055-Ar-Rahmaan: Utangulizi Wa Suwrah
055-Ar-Rahmaan: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah
Idadi Za Aayah: 78
Jina La Suwrah: Ar-Rahmaan
Suwrah imeitwa Ar-Rahmaan (Jina la Allaah), na yanayodalilisha, ni kutajwa mwanzo kabisa Suwrah, Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuwakumbusha majini na waanadam Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) zilizojificha na zilizodhahiri, na athari za Rehma Zake (Allaah) duniani na Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kukumbusha Uadhimu wa Allaah (عزّ وجلّ) na kubainisha wazi Neema Zake kwa Viumbe Vyake duniani na Aakhirah na kuwapinga wenye kukosa shukurani nazo.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kumtukuza Allaah (سبحانه وتعالى) na ihsaan Yake kwa viumbe kwa kuwaelimisha Qur-aan, Uwezo Wake wa kuwaumba na kuwafunza ufasaha.
2-Imebainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na baadhi ya Neema Zake kwa Viumbe Vyake.
3-Suwrah imekariri baada ya kila Aayah au Aayah chache Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) inayowahusu majini na wanaadam:
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٣﴾
“Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha.”
Hivyo basi imekariri mara 31 katika Suwrah hii tukufu.
4-Imekumbusha kutoweka kwa kila kilichopo juu ya mgongo wa ardhi, na kwamba Atakayebakia ni Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee. Na kwamba Anayepaswa kuombwa ni Yeye Pekee.
5-Imebainishwa udhalili na udhaifu wa majini na wanaadam kwamba hawataweza kupenya katika zoni za mbingu na ardhi. Na pindi wakijaribu kutaka kupenya, wataangamizwa kwa mwako wa moto!
6-Imetaja baadhi ya matukio na vitisho vya Siku ya Qiyaamah na mwisho mbaya wa makafiri, kuingizwa katika moto wa Jahannam.
7-Imetajwa aina mbili za mabustani ya Jannah na kila moja zimebainishwa raha na neema zake mbalimbali: (i) bustani mbili ambazo matawi yake yametanda (ii) bustani mbili nyenginezo ambazo rangi yake ni kijani iliyokoza.
8-Suwrah imekhitimishwa kwa kumtukuza Allaah (سبحانه وتعالى) Mwenye Ujalali na Ukarimu na Jina Lake Ambalo Limebarikika.