058-Al-Mujaadalah: Utangulizi Wa Suwrah
058-Al-Mujaadalah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa wengi.
Idadi Za Aayah: 22
Jina La Suwrah: Al-Mujaadalah
Suwrah imeitwa Al-Mujaadalah (Mjadala), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1); mwanamke aliyejadiliana na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mumewe.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kudhihirisha Ujuzi jumuishi wa Allaah uliokizunguka kila kitu kwa mapana yake na marefu yake, ili kuwalea watu wawe wanamchunga Allaah wakati wote, na kuwahadharisha wasije kwenda kinyume na Maamrisho Yake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kubainisha hukumu ya dhwihaar (aina ya talaka ambapo mume anamwambia mkewe: “Wewe kwangu ni kama mgongo wa mama yangu” na hivyo kumfanya kuwa ni haraam kwake kujamiana naye), na kubatilisha yale yaliyokua katika zama za jaahiliyyah (zama za ujinga kabla ya Uislamu).
3-Kuweka wazi siri za wanafiki, na kubainisha upotevu wao, na kauli zao za baatwil, na vitendo vyao viovu.
4-Kutaja baadhi ya adabu ambazo Waumini wanapaswa kujipamba nazo.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kuhusu mashitaka ya mwanamke aliyejadiliana na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mumewe aliyemtamkia dhwihaar, na kwamba Allaah Amewaona na Amesikia majibizano yao.
2-Imetolewa hukmu ya dhwihaar na kafara yake.
3-Imetajwa kufedheheshwa na mwisho mbaya wa waliopinzana na kumpinga Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
4-Kuthibitisha upana wa Ilimu ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba hakuna kinachofichika Kwake; ya dhahiri au ya siri.
5-Imedhihirishwa minong’ono waliyokuwa wakinong’ona maadui wa Uislamu na kumsalimia kwao Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa maneno yaliyomaanisha kumtakia maangamizi, na adhabu yao ya kuingizwa moto wa Jahannam.
6-Waumini wameamrishwa kutokunong’ona mambo ya dhambi na kumuasi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na wamche Allaah.
7-Waumini wanaongozwa baadhi ya adabu za vikao, na zimetajwa baadhi ya fadhila za ilimu.
8-Waumini waliwekewa sharia ya kutoa swadaqa walipotaka kunong’onezana katika kushauriana na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Lakini hukmu ya Aayah hiyo namba (12) ilifutwa, wakabadilishiwa kwa Aayah inayofuatia. Rejea Alhidaaya.com kwenye Makala ya An-Naasikh Wal-Mansuwkh (Kinachofuta Na Kinachofutwa)
9-Zimetajwa baadhi ya sifa za wanafiki, na kuwafanya kwao vipenzi Mayahudi, na kuapa kwao juu ya uongo, na kusahau kwao kumdhukuru Allaah, na kubainisha mwisho wao mbaya.
10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwasifu Waumini kwa al-walaa (kupendana kwa ajili ya Allaah) na kuwafanya rafiki wa ndani na vipenzi wanaompenda Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na al-baraa (kuwachukia na kujitenga) na wanaompinga Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) japokuwa ni watu wenye uhusiano wa damu nao. Na wakabashiriwa kwa Radhi za Allaah na kuingiziwa Jannah wadumu milele.