073-Al-Muzzammil: Utangulizi Wa Suwrah

 

073-Al-Muzzammil: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 20

 

Jina La Suwrah: Al-Muzzammil.

 

Suwrah imeitwa Al-Muzzammil (Mwenye Kujifunika), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuzibainisha sababu zitakazosaidia kuzisimamia tabu za da’wah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Maelekezo katika kile kinachopasa kujiandaa nacho, ili kubeba (kuvumilia) uzito wa mizigo ya da’wah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyenadiwa kwa Al-Muzzammil (Aliyejifunika nguo), aamke kwa ajili ya Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku kutekeleza ibaada) kwa muda mwingi.

 

2-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemthibitishia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kubalighisha Wahy, kwa kumwamrisha avute subira nzuri kutokana na maudhi ya makafiri.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Amewabainishia makafiri baadhi ya vitisho vya Siku ya Qiyaamah na adhabu Alizowaandalia.

 

4-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawakumbusha makafiri maangamizi ya Firawni alipomkadhibisha Rasuli wa Allaah; Muwsaa (عليه السّلام).

 

5-Ikafuatilia kutajwa baadhi ya vitisho vya Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo itawafanya watoto wawe na mvi, na mifupa yao kunyong’onyea kabisa.

 

6-Suwrah imekhitimishwa kwa kumsahilishia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waumini katika Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku, Tahajjud) kutekeleza ibaada katika hali ya safari, ugonjwa na pindi wanapokuwa wametoka kupigana Jihaad. Na wakawepesishiwa kuisoma Qur-aan katika hali hizo. Kisha wakaamrishwa kutekeleza faradhi za Swalaah na Zakaah, na kutoa swadaqa, na wakabashiriwa malipo makubwa na maghfirah kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

 

Share