077-Al-Mursalaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

077-Al-Mursalaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 50

 

Jina La Suwrah: Al-Mursalaat

 

Suwrah imeitwa Al-Mursalaat (Vinavyotumwa), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila na Faida. Na pia kutajwa kwake katika Aayah namba (1). 

 

Miongoni Mwa Makusudio Muhimu Ya Suwrah:

 

1-Ahadi ya adhabu kali siku ya Qiyaamah kwa wanaokadhibisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwaogopesha makafiri na kuwatahadharisha kutokana na ukafiri.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia Pepo zinazotumwa mfululizo. Na kwa pepo za dhoruba. Na kwa pepo zinazotawanya mawingu ya mvua. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaendelea Kuapia Malaika wanaopambanua haki na baatwil, halali na haraam, na Malaika wanaopokea Wahy kutoka Kwake kupeleka kwa Rusuli Wake, Wahy ambao unawapa viumbe nyudhuru na maonyo ili wasiwe na hoja Siku ya Qiyaamah kwamba hawajaletewa Rusuli na Risala ya Allaah. Kisha likaja jibu la Kiapo cha Allaah, nalo ni kuthibitisha kutokea yote waliyoahidiwa viumbe ya kutokea Siku ya Qiyaamah kama kupulizwa baragumu, kufufuliwa, kukusanywa katika Ardhw Al-Mahshar (Ardhi ya Mkusanyiko), na kuhesabiwa matendo; mema jazaa yake kuingizwa Jannah, na maovu  jazaa yake kuingizwa motoni.

 

2-Kisha ikafuatia kutajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah kama nyota kutoweka mwangaza wake, mbingu kupasukapasuka, majabali kupondekapondeka yawe kama mavumbi yanayopeperushwa, na Rusuli kutoa ushahidi wao wa kubalighisha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى). Kisha ikakariri Kauli ya Allaah kila baada ya Aayah kadhaa:

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ﴿١٥﴾

“Ole (wao) Siku hiyo kwa wenye kukadhibisha.” 

 

3-Yakatajwa maangamizi ya nyumati zilizopita kwa kukadhibisha Risala ya Allaah.

 

4-Zikatajwa hoja za mionekano ya baadhi ya Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kama kuumba viumbe, kuumba ardhi, kuthibitisha milima ardhini, kuteremshiwa mvua, kuhuisha na kufisha.

 

5-Ikatajwa baadhi ya vitisho kwa waliokadhibisha kama kuwekwa kwenye vivuli vyenye mwako wa moto, wasiweze kunena lolote la kuwanufaisha wala kupewa idhini ya kutoa nyudhuru. Wataambiwa kuwa hiyo ni Siku waliyoikadhibisha, ambayo ni Siku itakayokusanya viumbe wote tokea mwanzo hadi mwisho, Siku ambayo Allaah Atatoa Hukmu Yake na ukweli na ubatilifu utapambanuka.

 

6-Waumini wenye taqwa ambao waliogopa Adhabu za Allaah (سبحانه وتعالى), wamebashiriwa jazaa ya matendo yao mazuri kwa  kuwekwa kwenye vivuli na chemchemu wastarehe, na wapate matunda wanayoyatamani na vinywaji safi vya ladha nzuri, wale na wanywe kwa furaha.

 

7-Ikatajwa jazaa ya makafiri  kwa kuambiwa wale aina ya vyakula walivyokuwa wakila duniani ambayo ni starehe ya muda mfupi tu!  Hiyo ni jazaa yao kwa kukanusha Amri za Allaah kukataa kumnyenyekea Allaah na kuswali. 

 

8-Suwrah imemalizikia kwa onyo kwamba, ikiwa makafiri hawataiamini Qur-aan hii ambayo Aaayat Zake ziko wazi katika Hikma Zake, yenye mwongozo na Rehma, basi wataamini kitabu gani baada yake?

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Suwrah Ya Mwisho Ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameisoma katika Swalaah ya Magharibi:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ ـ رضى الله عنهما ـ أَنَّهُ قَالَ إِنَّ أُمَّ الْفَضْلِ سَمِعَتْهُ وَهُوَ يَقْرَأُ - ‏وَالْمُرْسَلاَتِ عُرْفًا - ‏ فَقَالَتْ يَا بُنَىَّ وَاللَّهِ لَقَدْ ذَكَّرْتَنِي بِقِرَاءَتِكَ هَذِهِ السُّورَةَ، إِنَّهَا لآخِرُ مَا سَمِعْتُ مِنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ بِهَا فِي الْمَغْرِبِ‏.‏

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): (Mama yangu) Umul-fadhwl alinisikia nikisoma:

وَالْمُرْسَلَاتِ عُرْفًا﴿١﴾

Akasema: “Ee mwanangu! Wa-Allaahi umenifanya nikumbuke kuwa ilikuwa Suwrah ya mwisho niliyoisikia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiisoma katika Swalaah ya Maghrib.” [Al-Bukhaariy]

 

2-Nyoka Alikimbia Alipokuwa Akiisooma Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 عَنِ الأَسْوَدِ، قَالَ قَالَ عَبْدُ اللَّهِ بَيْنَا نَحْنُ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فِي غَارٍ إِذْ نَزَلَتْ عَلَيْهِ وَالْمُرْسَلاَتِ فَتَلَقَّيْنَاهَا مِنْ فِيهِ وَإِنَّ فَاهُ لَرَطْبٌ بِهَا إِذْ خَرَجَتْ حَيَّةٌ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ عَلَيْكُمُ اقْتُلُوهَا ‏"‏‏.‏ قَالَ فَابْتَدَرْنَاهَا فَسَبَقَتْنَا ـ قَالَ ـ فَقَالَ ‏"‏ وُقِيَتْ شَرَّكُمْ، كَمَا وُقِيتُمْ شَرَّهَا ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Al-Aswad (رضي الله عنه): ‘Abdullaah [Bin Mas’uwd] (رضي الله عنه) amesema: Tulipokuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika pango ikateremka

وَالْمُرْسَلَاتِ

Naye anaisoma, nami naipokea kutoka kinywani mwake, na hakika kinywa chake kina rutuba (sio kikavu kwa kuisoma Suwrah hiyo).  Ghafla akatoka nyoka, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Lazima mumuuwe!” ‘Abdillaah akasema: Tukamfukuza akatukimbia. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Amesalimishwa na shari yenu kama mlivyosalimishwa na shari yake.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share