081-At-Takwiyr: Utangulizi Wa Suwrah

 

081-At-Takwiyr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 29

 

Jina La Suwrah: At-Takwiyr

 

Suwrah imeitwa At-Takwiyr (Kukunjikakunjika), na yanayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida, na kutajwa katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ukamilifu wa Qur-aani katika kuikumbusha nafsi juu ya kuharibika ulimwengu wakati wa kufufuliwa waja. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha hali za Qiyaamah, na vitisho vyake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa yatakayotokea Siku ya Qiyaamah, yenye kushtua nyoyo, kama jua kukunjwa na kupotea mwanga wake, nyota kuanguka, milima kupondwapondwa, ngamia kutelekezwa, wanyama mwitu kukusanywa, bahari zitakapowashwa moto, watu watakapounganishwa wema kwa wema, waovu kwa waovu, mtoto wa kike aliyezikwa hai kutokana na kudhalilishwa, atakapoulizwa ni dhambi ipi aliyofanya hata astahiki kudhulumiwa hivo! Sahifa za matendo zitakapokunjuliwa, mbingu zitakapobanduliwa.

 

2-Kisha ikafuatia kutajwa kuwa Jannah itakurubishwa, na moto kuwa utahudhurishwa; vyote hivi viwe mbele ya viumbe.

 

3-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaapia kwa sayari zinazotoweka mchana na kudhihirika usiku, na kuingia kwa usiku, na kupambazuka kwa asubuhi.

 

4-Ikafuatia jibu la Kiapo ni kuthibitishwa kwamba Quraan inatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na akatajwa anayeipokea ambaye ni Jibriyl (عليه السّلام) na zikatajwa sifa zake tukufu, na akathibitishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sifa nzuri, ambaye anaipokea Qur-aan na kuibalighisha. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuwaradd washirikina waliompachika sifa ovu ya umajnuni.

 

4-Imebainishwa kwamba Qur-aan ni mawaidha na ukumbusho kwa mwenye kutaka kuhidika.

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwekwa wazi ya kwamba, matakwa ya mja ni yenye kufuata Matakwa ya Allaah, Rabb wa walimwengu wote.

 

Faida:

 

Anayetaka Kuitazama Siku Ya Qiyaamah, Asome Suwrah hii:

 

عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ، وَهُوَ ابْنُ يَزِيدَ الصَّنْعَانِيُّ قَالَ سَمِعْتُ ابْنَ عُمَرَ، يَقُولُ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ مَنْ سَرَّهُ أَنْ يَنْظُرَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ كَأَنَّهُ رَأْىُ عَيْنٍ فَلْيَقْرَأْ ‏ إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ)‏ و ‏ (‏إِذَا السَّمَاءُ انْفَطَرَتْ)‏ وَ ‏ (‏إذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ‏"‏ ‏.‏ هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ غَرِيبٌ

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan naye ni Ibn Yaziyd Asw-Swan’aaniyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kutaka kuitazama Siku ya Qiyaamah, kana kwamba anaiona kwa jicho hili, basi na asome:

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾

 

“Jua litakapokunjwa kunjwa na kupotea mwanga wake.” [At-Takwiyr (81)]

 

إِذَا السَّمَاءُ انفَطَرَتْ ﴿١﴾

“Mbingu itakapopasuka.” [Al-Infitwaar (82)]

إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾

“Mbingu itakaporaruka.” [Al-Inshiqaaq (84)]

 

[Ahmad (4806), At-Tirmidhiy (3333), amesema ni Hadiyth Hasan Ghariyb. Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhy] 

 

 

 

Share