084-Al-Inshiqaaq: Utangulizi Wa Suwrah
084-Al-Inshiqaaq: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 25
Jina La Suwrah: Al-Inshiqaaq
Suwrah imeitwa Al-Inshiqaaq (Kuraruka), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida, na kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kumkumbusha mwanaadam kurejea kwake kwa Rabb wake, na kubainisha udhaifu wake na kubadilika kwa hali zake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Wasifu wa Siku ya Qiyaamah na hali za watu ndani yake.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa yatakayotokea Siku ya Qiyaamah, yenye kushtua nyoyo, Siku ambayo kila kitu kitatii Amri za Allaah Atakapoamrisha mbingu kuchanika, ardhi kutandazwa na kutolewa watu makaburini. Kisha akajulishwa binaadam kwamba, bila shaka atakutana na Rabb wake alipwe malipo yanayolingana na amali zake; njema au mbaya.
2-Imeelezewa watu watakaopokea Kitabu chao mkono wa kulia, ambao ni Waumini waliomcha Allaah na wakatenda mema, kwamba watahesabiwa hesabu nyepesi, kisha watawageukia ahli zao kwa furaha. Ama watu watakaopewa kitabu chao nyuma ya migongo yao ambao ni makafiri, hawa watapata maangamizi na wataingizwa motoni kwa kufru na kukadhibisha kwao Risala ya Allaah, na kutokuamini kufufuliwa.
3-Kisha kikatajwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia wekundu wa mbingu baada ya Magharibi, na Kuapia mwezi unapokamilika ukatoa mwangaza wake. Kisha jibu la kiapo ni kuwatambulisha wanaadam kwamba, bila shaka watapitia hali tofauti za maisha yao, ikianzia kuumbwa kwao kwa tone la manii mpaka kuzaliwa, kuishi kwao duniani mpaka kufa na mpaka kufufuliwa.
4-Wakaulizwa makafiri ni kitu gani kinachowazuia kumwamini Allaah (سبحانه وتعالى) baada ya Aayah Zake kufafanuliwa kwao? Na kwamba wanaposomewa Qur-aan hawanyenyekei na hawajisalimishi kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kutii amri Zake na Makatazo Yake, na kumsujudia. Na kwamba Allaah ni Mjuzi zaidi wa ukaidi wao wanaouficha kwenye nyoyo zao, hali wao wanajua kuwa yaliyoletwa na Qur-aan ni haqq (kweli).
5-Suwrah imekhitimishwa kwa kubashiriwa makafiri adhabu kali, na Waumini waliotenda mema wamebashiriwa kwa ujira usiokatika wala kupunguka.
Fadhila Za Suwrah:
Kuweko Sajdah At-Tilaawah (Sijda ya Kisomo) Ndani Ya Suwrah:
عَنْ أَبِي سَلَمَةَ، قَالَ رَأَيْتُ أَبَا هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَرَأَ إِذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ فَسَجَدَ بِهَا فَقُلْتُ يَا أَبَا هُرَيْرَةَ، أَلَمْ أَرَكَ تَسْجُدُ قَالَ لَوْ لَمْ أَرَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَسْجُدُ لَمْ أَسْجُدْ.
Amesimulia Abu Salamah (رضي الله عنه): Nilimuona Abu Hurayrah (رضي الله عنه) akiisoma
إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾
“Mbingu zitakaporaruka.” [Al-Inshiqaaq (84)]
Akasujudu wakati alipokuwa akiisoma. Nikamuuliza Abu Hurayrah: Je, Sijakuona ukisujudu? Abu Hurayrah akajibu: “Ningekuwa sikumuona Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) anasujudu, nami nisingesujudu.” [Al-Bukhaariy]
Faida:
Anayetaka Kuitazama Siku Ya Qiyaamah, Asome Suwrah hii:
عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ، وَهُوَ ابْنُ يَزِيدَ الصَّنْعَانِيُّ قَالَ سَمِعْتُ ابْنَ عُمَرَ، يَقُولُ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " مَنْ سَرَّهُ أَنْ يَنْظُرَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ كَأَنَّهُ رَأْىُ عَيْنٍ فَلْيَقْرَأْ إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ) و (إِذَا السَّمَاءُ انْفَطَرَتْ ) وَ (إذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ " . هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ غَرِيبٌ
Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan naye ni Ibn Yaziya Asw-Swan’aaniyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kutaka kuitazama Siku ya Qiyaamah, kana kwamba anaiona kwa jicho hili, basi na asome:
إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾
“Jua litakapokunjwa kunjwa na kupotea mwanga wake.” [At-Takwiyr (81)]
إِذَا السَّمَاءُ انفَطَرَتْ ﴿١﴾
“Mbingu itakapopasuka.” [Al-Infitwaar (82)]
إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾
“Mbingu itakaporaruka.” [Al-Inshiqaaq (84)]
[Ahmad (4806), At-Tirmidhiy (3333), amesema ni Hadiyth Hasan Ghariyb. Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhy]