088-Al-Ghaashiyah: Utangulizi Wa Suwrah
088-Al-Ghaashiyah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa
Idadi Za Aayah: 26
Jina La Suwrah: Al-Ghaashiyah.
Suwrah imeitwa Al-Ghaashiyah (Kufunikiza Na Kutoa Fahamu), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth iliyonukuliwa kwenye Fadhila, na kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuwakumbusha wanaadam kuhusu Aakhirah na mambo yaliyopo huko ya thawabu na adhabu, na kuangalia dalili zinazoonyesha Uwezo wa Allaah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kubainisha hali za makafiri na Waumini Siku ya Qiyaamah.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kuelezea habari za Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo itawafunikiza watu, fahamu ziwatoke.
2-Kisha ikafuatia kuelezea hali za makafiri kwamba, nyuso zao zitadhalilika, watakuwa wametaabika na kuchoka, na wataingizwa motoni ambako watanyweshwa maji ya moto yatokotayo. Hawatakuwa na chakula isipokuwa kinachotokana na miba, kichungu mno! Chakula hicho hakimnoneshi mwenye kukila wala hakimuondolei mtu njaa.
3-Kisha ikaelezewa hali za Waumini kwamba, Siku hiyo nyuso zao zitakuwa zenye kuneemeka, zitafarijika kwa kutokana na kuamini kwao Aakhirah na kuridhika, wakafanya juhudi duniani na kutenda mema. Basi watakuwa katika Jannah za daraja ya juu ambako hawatasikia upuuzi, na wataneemeshwa kwa kila aina za neema na starehe.
4-Imethibitishwa Tawhyid ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji na kadhalika) na Uwezo Wake Allaah (سبحانه وتعالى) wa Kuumba na Kuunda kwa hikma viumbe, kama vile jinsi Alivyomuumba ngamia kwa muujiza, mnyama ambaye ana faida na hadhi kubwa kwa wanaadam. Basi washirikina wakatanabahishwa wamwangalie na wazingatie kwa kina mwili wake wote, ambao kila sehemu ya mwili wake una muujiza. Na kwamba mnyama huyu wa ajabu, ana manufaa makubwa kwa wanaadam katika maisha yao, kama vile katika biashara zao, na safari zao. Hivyo basi kuna ishara na dalili za wazi kabisa zenye kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah, kwamba ni Yeye Pekee Muumbaji wa viumbe na ulimwengu na yaliyomo ndani yake. Basi na watanabahi pia mengineyo ya Uumbaji wa Allaah kama mbingu, majabali na ardhi.
5-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) anaamrishwa akumbushe watu awawaidhi, na wanaokengeuka na kukufuru, wametishiwa adhabu kubwa ya Allaah.
6-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitishwa kufufuliwa viumbe na kuhesabiwa matendo.
Fadhila Za Suwrah:
Ni Sunnah Kuisoma Suwrah Hii Katika Swalaah Ya Ijumaa Na ‘Iyd Mbili:
عَن النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ، قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ وَالْعِيدِ بِـ { سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى } وَ { هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ } وَإِذَا اجْتَمَعَ الْجُمُعَةُ وَالْعِيدُ فِي يَوْمٍ قَرَأَ بِهِمَا .
Amesimulia Nu’maan Bin Bashiyr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى
Na
هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ
Katika Rakaa ya kwanza ya Swalaah ya Ijuma. Na inapojumuika Ijumaa na ‘Iyd katika siku moja, alizisoma pia (Suwrah hizo). [Muslim, An- Nasaaiy, Abuu Daawuwd]