091-Ash-Shams: Utangulizi Wa Suwrah
091-Ash-Shams: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 15
Jina La Suwrah: Ash-Shams
Suwrah imeitwa Ash-Shams (Jua), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Msisitizo juu ya sehemu ndefu zaidi ya Qur-aan inayozungumzia juu ya kuadhimisha na kuitakasa nafsi na hasara ya kuifisidi kwa kutenda maasi. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
1-Kuhamasisha utiifu na kutahadharisha maasi.
2-Kuwatishia washirikina adhabu kama zilizowapata walio kabla yao.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia jua na mwangaza wake baada ya kuchomoza kwake asubuhi. Na Kuapia kwa mwezi unapolifuata jua likawa nyuma yake na kutoa mwangaza baada ya kuchwa jua. Na Kuapia kwa mchana unapodhihirisha jua waziwazi bila kufichikana. Na Kuapia kwa usiku unapofunika jua, ardhi ikawa giza. Na Kuapia kwa mbingu na kujengeka kwake imara. Na Kuapia kwa ardhi na kutandikika kwake ikawa kama tandiko wakaweza kuishi viumbe humo. Na Kuapia kwa nafsi Aliyoikamilisha umbo lake ili itekeleze kazi iliyoumbiwa nayo. Kisha Akaibanishia njia ya shari na njia ya kheri. Kisha yakatajwa yanayohakikishiwa kiapo, nayo ni kubainisha kufaulu kwa nafsi na kula khasara. Aliyefaulu ni mwenye kuitakasa nafsi kwa utiifu na matendo mema. Na aliyekula khasara ni mwenye kuitia nafsi katika maasi na kutokufanya matendo mema
2-Suwrah imekhitimishwa kuwatishia washirikina ya kwamba, itawapata adhabu na maangamizi kama ilivyowapata kina Thamuwd, pindi watakapoendelea katika ukafiri wao. Ikatajwa sehemu ya kisa cha kina Thamuwd waliokadhibisha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى) kupitia Rasuli wao Swaalih (عليه السّلام), na jinsi walivyovuka mipaka kuasi amri za Allaah, kwani pindi walipotaka waletewe muujiza ambao utawaonyesha ukweli wa Rasuli wao, Allaah Akawatolea ngamia jike kutoka katika jabali. Wakaamrishwa na Rasuli wao kwamba, huyo ni ngamia wa Allaah wasimguse kwa uovu, na wafanye zamu katika kinywaji; siku moja anywe ngamia, na siku moja wateke maji na wanywe wao. Lakini hilo lilikuwa zito kwao. Wakamkanusha Rasuli wao, na wakapuuza amri hizo, na mwishowe wakamchinja ngamia wa Allaah. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaadhibu na kuwaangamiza kwa kuwatumia ukelele mkali, na tetemeko la ardhi, wakafariki wa kuanguka kifudifudi majumbani mwao. Na Akazibomoa nyumba zao na Kuzisawazisha na ardhi.