109-Al-Kaafiruwn: Utangulizi Wa Suwrah
109-Al-Kaafiruwn: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 6
Jina La Suwrah: Al-Kaafiruwn
Suwrah imeitwa Al-Kaafiruwn (Makafiri), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila, na kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Muhimu Ya Suwrah:
1-Utakaso kutokana na ukafiri na watu wake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kujiweka mbali kabisa kati ya wanaompwekesha Allaah na makafiri.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) awatangazie makafiri kwamba yeye haabudu wanavyoviabudu miongoni mwa masanamu na waungu wa urongo. Na kwamba wao hawamwabudu Mwabudiwa Mmoja Anayestahiki kuabudiwa. Na akasisitizwa tena awaambie makafiri hayo hayo. Na kwamba wao dini yao ni ya kuabudu masanamu yasiyoweza kuwanufaisha wala kuwadhuru, na yeye Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ana Dini Tukufu ya Uislamu ambayo ni Dini ya haki, ya kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee, Mwenye Kusikia na Kuona, Mwenye Uwezo wa Kunufaisha na kudhuru, na Mwenye Majina Mazuri Kabisa na Sifa Tukufu ambazo hakuna anayezimiliki isipokuwa Yeye Allaah (سبحانه وتعالى). Kuwatangazia hivyo makafiri, ni kwa sababu Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mjuzi wa kutambua kwamba miongoni mwa hao makafiri, wako ambao hawataamini kamwe!
Fadhila Za Suwrah.
1-Ni Sunnah Kuisoma Katika Swalaah Ya Sunnah Ya Alfajiri Na Magharibi:
عن أبي هريرة رضي الله عنه : أنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قرأ في رَكْعَتَي الفَجْرِ: قُلْ يَا أَيُّهَا الكَافِرُونَ وَ قُلْ هُوَ اللهُ أَحَدٌ . رَوَاهُ مُسلِمٌ .
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma katika Rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri:
قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ
[Al-Kaafiruwn (109)]
Na
قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ
[Al-Ikhlaasw (112)]
[Muslim na wengineo]
2-Ni Sunnah Kuisoma Katika Rakaa Ya Pili Ya Swalaatul-Witr:
عَنْ سَعِيدِ بْنِ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبْزَى، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أُبَىِّ بْنِ كَعْبٍ، قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الرَّكْعَةِ الأُولَى مِنَ الْوَتْرِ بِـ سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى وَفِي الثَّانِيَةِ بِـ قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ وَفِي الثَّالِثَةِ بِـ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ
Amesimulia Ubayy Bin Ka’b (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Rakaah ya kwanza ya Swalaah ya Witr:
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الأَعْلَى
[Al-A’laa (87)]
Na katika ya pili:
قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ
[Al-Kaafiruwn (109)]
Na katika ya tatu:
قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ
[Al-Ikhlaasw (112)]
[At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nasaaiy]
3-Ni Sunnah Kuisoma Katika Maqaam Ibraahiym (Kisimamo Cha Ibraahiym) Baada Ya Kumaliza Twawaaf Ya ‘Umrah:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَرَأَ فِي رَكْعَتَىِ الطَّوَافِ بِسُورَتَىِ الإِخْلاَصِ : قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ وَ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ
Amesimulia Jaabir Bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amezisoma Suwrah zinazojulikana za ikhlaasw katika Rakaa mbili baada ya Twawaaf. Nazo ni:
قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ
Na
قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ
[At-Tirmidhiy]
4-Thawabu Za Kuisoma Ni Kama Thawabu Za Kusoma Robo Ya Qur-aan:
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم :((قُلْ هو اللَّهُ أحَدٌ تعدلُ ثلثَ القرآنِ. و قُلْ يَا أيُّهَا الْكَافِرُونَ تعدلُ ربعَ القرآنِ))
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
قُلْ هو اللَّهُ أحَدٌ
ni sawa na thuluthi ya Qur-aan na
قُلْ يَا أيُّهَا الْكَافِرُونَ
ni sawa na robo ya Qur-aan.” [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar, ameisahihisha Al-Albaaniy Taz. Swahiyh Al-Jaami’ (4405), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (586)]