27-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Ndoa Ambazo Ni Batili Kisharia: Ndoa Ya Shighaar

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

  الأَنْكِحَةُ الفَاسِدَةُ شَرْعًا

Nikaah (Ndoa) Ambazo Ni Batili Kisharia

 

Alhidaaya.com

 

 

27:  Ndoa ya “Shighaar”:

 

Hii ni ndoa ambayo mtu anamwozesha mtu mwingine binti yake, au dada yake, au mfano wa hao, kwa sharti kwamba mtu huyo naye amwozeshe yeye binti yake au dada yake na kadhalika, ni sawa kwa mahari au bila mahari.

 

‘Ulamaa wote wameharamisha aina hii ya ndoa.   Jopo la ‘Ulamaa (Jumhuwr) wamesema kwamba ndoa hii ni batili kutokana na dalili zifuatazo:

 

1-  Hadiyth ya Jaabir:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الشِّغَارِ" 

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha (ndoa ya) “Shighaar”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1417)]

 

2-  Toka kwa Abu Hurayrah:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الشِّغَارِ، وَالشِّغَارُ أَنْ يَقُولَ الرَّجُلُ لِلرَّجُلِ: زَوِّجْنِي ابْنَتَكَ وَأُزَوِّجُكَ ابْنَتِي، أَوْ زَوِّجْنِي أُخْتَكَ وَاُزوِّجُكَ أُخْتِي" 

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha “Shighaar”.  Akasema Abu Hurayrah:  “Shighaar” ni mtu kumwambia mtu mwingine:  Niozeshe binti yako nami nikuozeshe binti yangu.  Au:  Niozeshe dada yako nami nikuozeshe dada yangu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1416), An-Nasaaiy (6/112) na Ibn Maajah (1884]

 

3-  Toka kwa Al-A’araj: 

 

"أَنَّ الْعَبَّاسَ بْنَ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ الْعَبَّاسِ، أَنْكَحَ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ الْحَكَمِ ابْنَتَهُ وَأَنْكَحَهُ عَبْدُ الرَّحْمَنِ ابْنَتَهُ، وَكَانَا جَعَلاَ صَدَاقًا، فَكَتَبَ مُعَاوِيَةُ إِلَى مَرْوَانَ يَأْمُرُهُ بِالتَّفْرِيقِ بَيْنَهُمَا، وَقَالَ فِي كِتَابِهِ: هَذَا الشِّغَارُ الَّذِي نَهَى عَنْهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم"

 

“Kwamba Al-‘Abbaas bin ‘Abdillaah bin Al-‘Abbaas alimwozesha ‘Abdulrahmaan bin Al-Hakam binti yake, na yeye  ‘Abdulrahmaan akamwozesha binti yake, na walikuwa wamepangiana mahari.  Mu’aawiya akamwandikia Marwaan na kumwamuru avunje ndoa hiyo.  Akasema kwenye barua hiyo:  Hii ni “Shighaar” ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameikataza”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2075)]

 

4-  Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

"مَنِ اشْتَرَطَ شَرْطًا لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهْوَ بَاطِلٌ، وَإِنِ اشْتَرَطَ مِائَةَ شَرْطٍ، شَرْطُ اللَّهِ أَحَقُّ وَأَوْثَقُ"

 

“Mwenye kushurutisha sharti lolote ambalo haliko katika Sharia za Allaah basi ni batili, hata akishurutisha masharti mia moja.  Sharti la Allaah ndilo lenye haki zaidi na lenye fungamano zaidi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2155) na Muslim (1504)]

  

5-  Kushurutisha mapasiano kati ya watu hao wawili kunapelekea uharibifu mkubwa katika ndoa hii, kwa sababu mwanamke hapa analazimishwa kuolewa na mtu ambaye pengine hakumpenda au asiyemtaka.  Inakuwa ni kuweka mbele maslahi ya mawalii juu ya maslahi ya wanawake, na hii ni dhulma kwao.  Lakini pia, wanawake hawa wanakosa mahari, hawayapati kama wanavyopata wanawake wengine.  Huu ndio uhalisia wa wanaume wenye kushabikia ndoa hii ya kuchukiza.  Isitoshe, baada ya ndoa, kunazuka misuguano, mivutano na magomvi, na hii ni katika adhabu za papo kwa hapo kwa wote wenye kukhalifu Sharia ya Allaah.  [Sehemu ya Risala ya Al-‘Allaamah Ibn Baaz (RahimahuL Laah yenye anuani: “Ndoa ya Shighaar”]

 

 

 

Share