05-Malaika: Matunda Ya Kuamini Malaika

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

05:  Matunda Ya Kuamini Malaika

 

Kuna matunda makubwa ya kuamini Malaika.  Kati yake ni:

 

1-  Muislamu anapata kujua U’adhwama wa Allaah Ta’alaa, Nguvu Zake, na Ufalme Wake, kwani ukubwa wa kiumbe unatokana na u’adhwama wa Muumbaji wake.  Allaah Anasema:

 

"وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ"

 

Na katika Ishara Zake, ni uumbaji wa mbingu na ardhi, na Aliowatawanya humo kati ya viumbe vinavyotembea, Naye kwa kuwakusanya Atakapo Ni Muweza”. [Ash-Shuwraa: (29)].

 

Ibn Kathiyr akiifasiri aya hii anasema:  “Hii ni pamoja na Malaika, majini, watu na wanyama wengineo, wakiwa wametofautiana maumbo yao, rangi zao, lugha zao, maumbile yao, jinsia zao na aina zao.   Na hawa wote, Allaah Ta’aalaa Amewatawanya kwenye majimbo ya mbinguni na ardhini”.

 

Na Malaika Jibriyl (‘Alayhis Salaam) ana mbawa 600 ambazo zinafunika mashariki yote.  Je, Allaah Aliyemuumba Atakuwa vipi?

 

2-  Muislamu anapata kumshukuru Allaah ‘Azza wa Jalla kwa kuwapa wanadamu uangalizi na ulinzi pale Alipowapa baadhi ya Malaika jukumu la kuwalinda, na Malaika wengineo jukumu la kusajili matendo yao na mengineyo katika maslaha yao.

 

3-  Kunamhisisha mtu kwamba Allaah Anamfuatilia, na kwamba Malaika Wake wanasajili matendo yake yote, na hii inakuwa ni chachu kwake ya kuongeza bidii katika ibada na kujiweka mbali na mambo mabaya.

 

4-  Na kwa vile wao hawamwasi Allaah kwa lolote Analowaamuru, na wanafanya yote wanayoamuriwa, kwa hili, Muislamu anajitahidi awaige katika kutekeleza Maamrisho yote ya Allaah Ta’aalaa.

 

5-  Kunamfanya Muislamu kuwa na pupa ya kuwepo mahala ambapo Malaika wanapapenda kama Misikitini, kwenye vikao vya elimu za dini, adhkaar na kadhalika.

 

 

Share