17-Malaika: Je, Malaika Wana Sifa Ya Uzuri Wa Sura Na Umbo?

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

17:  Je, Malaika Wana Sifa Ya Uzuri Wa Sura Na Umbo?

 

Katika akili za watu, imejengeka taswira ya kuwa Malaika ni viumbe wenye sifa ya uzuri wa sura na maumbo kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa kuhusiana na akina mama walioalikwa na Zulaykha wakati walipomwona Yuwsuf (‘Alayhis Salaam):

 

"فَلَمَّا رَأَيْنَهُ أَكْبَرْنَهُ وَقَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ وَقُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا هَـٰذَا بَشَرًا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ"

 

“Basi walipomuona (Yuwsuf) walimpa haiba na utukuzo, wakajikatakata mikono yao, na wakasema:  Utakasifu ni wa Allaah!   Huyu si mtu!  Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu”.  [Yuwsuf: 31]

 

Hii ni dhana njema kwa upande wa viumbe hawa ambao hakuna binadamu yeyote aliopata kuwaona isipokuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyemwona Jibriyl (‘alayhis salaam) katika umbile lake la asili akiwa na mbawa mia sita.  Na Jibriyl ndiye Malaika aliyeelezewa sifa zake kwenye Qur-aan Tukufu.   Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ"

 

Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi. ● Mwenye muonekano jamili, muruwa na nguvu na kisha akalingamana sawasawa”.  [An-Najm: 5-6]

 

Hizi ndizo sifa za Jibriyl (‘alayhis salaam) kama zilivyoelezewa kwenye Aayaah hii.

 

Wengine wenye sura nzuri na maumbo ni pamoja na wale wanaomjia muumini mwema wakati anapokufa ambapo humjia wakiwa na nyuso nyeupe.  Wengine ni wale watakaowapokea Waislamu wakati wa kuingia Peponi na kadhalika.

 

Hivyo basi, Malaika kwa mujibu wa majukumu yao, wana maumbile na sura tofauti zikiwemo za kutisha na kuogofya.

 

 

Share