Harusi Inaweza Kufanyika Ikiwa Kuna Mtu Amefiwa Au Katika Eda?

 

SWALI: 

Asalam alkm.

na suali ambalo ningependelea unielezee.  Ni kweli kama ikiwa kuna eda katika family haifai kufanywa harusi?  Kuna harusi ambayo ilikuwa planned ifanywe mwezi wa nane lakini katika wiki mbili hivi zilizopita, kuna mtu amekufa katika family na sasa jamaa wanasema hawawezi kufanya harusi mpaka eda ikisha shuka.  Ni sawa kufanya hivyo?
 
Jazaka Allah kheir

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna makatazo katika sheria yetu kwamba akiweko mtu katika familia kwenye Eda, na kama Nikaah inataka kutendeka isifanywe kwa ajili ya Eda. Hayo na mependekezo ya hao watu labda kwa kumuonea vibaya aliyefiwa na mumewe kwa vile ni katika familia. Lakini tutambue kwamba Kiislamu hakuna kuweka msiba, zaidi imependekezwa tu kuwa ni siku tatu isizidi kwa waliofiwa. Baada ya hapo Waislamu wanatakiwa waendeshe maisha yao kama kawaida bila ya kuzuilika na jambo lolote. Na ikiwa mtu ana uwezo wa kutahamali na kuvumilia ule msiba wake chini ya siku tatu, basi hata siku hiyo hiyo sheria haimkatazi yeye au watu wake kufanya jambo lolote la kisheria lenye furaha kama Harusi. Ni mambo ya kiutu na kibinaadam ndio yanayomzuia mtu kufanya sherehe masiku machache anapofiwa, lakini Dini haimzuii mtu kuhudhuria au kuandaa ndoa au jambo lolote la halali kwa sababu wamefiwa. Kuna mambo ya ada na desturi ambayo yanaleta vikwazo na matatizo mengi katika jamii, mojawapo ni hili, baadhi ya watu wanapopatwa na msiba, wanaona kufanyika jambo la ndoa ni jambo halifai na wengine hata yakipita masiku na mawiki bado kwao si sawa kushereheka au kuendelea na mambo mengine ya kimaisha.

Hali hiyo hadi inakuwa ni vikwazo kwa wengine wenye mambo yao ya kheri kuyafanya kwa wakati huo kwa sababu tu kuna wengine wataudhiwa au kuonekana hawakuheshimiwa misiba yao.

Haya ni mambo ya ada yanayopaswa yaachwe na Waislam, na viongozi wa Dini ni wajibu wao kuielimisha jamii yao badala ya kuiendekeza na hali hiyo au kuwaonea muhaali kwa kuchelea kuonekana wabaya au kwa kuogopa kupoteza kukubalika kama baadhi ya viongozi wanavyodhani. Kumweka Allaah mbele ya kila jambo na kumtakasia yeye mambo ndio hekima, na hekima si kuridhisha watu kwa mambo yasiyo ya kisheria. Wengi wameshindwa kuelewa maana halisi ya hekima, au kwa makusudi wanaipindisha maana yake kwa ajili ya matakwa ya kibinafsi.

Jamii kubwa inabaki katika makosa na ujinga kutokana na Masheikh, Maustaadh na Maimaam kuwa kimya au kuwastahi watu kuwaambia ukweli pindi wanapoona munkaraat kwa kuchelea kupingwa au kukosa uluwa wa kidunia.

 

Inapaswa kufahamika kwamba kila hukmu inayopaswa kufuatwa iwe ina dalili kutoka katika Qur-aan au Sunnah, na kama hakuna dalili yoyote inayothibitisha kauli kama hiyo basi huwa haina asili na haipasi kufuatwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share