Waislamu Wanapopata Madaraka Huwa Na Khiyana; Hawasaidii Wenzao

SWALI:

KWA NINI WAISLAM WALIOWENGI (NGUZO TANO WANAZINGATIA) WANAPOPATA MADARAKA ANGALAU YA USIMAMIZI TU (SUPERVISORY) ACHILIA MBALI NGAZI ZA JUU, WANAKUWA NA HIYANA NA HASADI ZA ROHO  JUU YA WAISLAMU WENZAO.

TOFAUTI NA DINI NYINGENE AMBAPO WANAKUWA NA HATA MTANDAO WA KUSAIDIANA? NINI HUKUMU YA WATU KAMA HAWA?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran ndugu yetu mpendwa kwa swali lako hilo. Hakika hayo uliyoyasema ni kweli kabisa na hilo limekuwa tatizo sugu katika jamii yetu. Imekuwa Muislamu aliye na madaraka aina yoyote anamfadhilisha asiyekuwa Muislamu kumpatia nyadhifa mbali mbali kuliko Muislamu aliye na uzoefu na elimu sawa.

Muislamu kwa njia yoyote ile hawi hasidi wala hafanyi hiyana kabisa. Kitabia Muislamu anawapendelea kheri watu wote – Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwani hawa wa pili ni wanaadamu nao wanahitaji kuvutwa kwa Uislamu ili wawe wanaadamu wazuri na wema zaidi. Muislamu hapendi tabia ya husda, kwani hiyo ni kupinga ugawaji kwa Allaah Aliyetukuka na fadhila Zake kwa viumbe Wake. Anasema Aliyetukuka: “Au wanawahusudu watu kwa yale aliyowapa Allaah kwa fadhila Yake?” [.

Ama hiyana ni alama moja ya unafiki kwa mujibu wa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyonukuliwa na al-Bukhaariy na Muslim.

Allaah Aliyetukuka Amehimiza sana watu na hasa Waislamu wasaidiane katika wema. Wema ulio bora wakati huu ni kumsaidia nduguyo kupata kazi na pato la halali. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na saidianeni katika wema na uchaji Allaah. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah” [5: 2].

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mnusuru (na msaidie) ndugu yako akiwa amedhulumu au amedhulumiwa”. Akaulizwa: “Aliyedhulumiwa tunafahamu, je huyu aliyedhulumu tumsaidie vipi?” Akasema: “Msaidie asidhulumu” [Al-Bukhaariy].

Mbali na kusema ya kwamba Uislamu unapinga sana sifa na tabia ya hiyana na hasadi na kuhimiza sana kusaidiana na kujenga udugu, inatakiwa tufahamu kuwa Uislamu unahimiza sana uadilifu na usawa. Haitokuwa sawa Kiislamu kwa Muislamu kumpatia kazi Muislamu kwa kuwa tu ni Muislamu japokuwa hana uzoefu wa kazi au hakusoma. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na ucha Mungu. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah Anazo khabari za mnayoyatenda” [5: 8].

Pia, “Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi kwa ajili ya Allaah, ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Allaah Anajua vyema mnayoyatenda” [4: 135].

Hapa Aayah zinazungumzia kuhusu ushahidi kwa wenye kutoa ushahidi hawafai kupendelea. Hivyo hivyo, katika kutekeleza mambo mengine kama kuajiri ni lazima mtu Muislamu awe muadilifu katika kutekeleza wadhifa wake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share