Mtoto Kukosa Radhi Za Wazazi Kwa Sababu Ya Kuchagua Mwenyewe Mke

 

 

SWALI:

Assalaam alaykum.

Iwapo amejichagulia mchumba kumuoa na wazazi hawakuridhika na msichana huyo akimuoa atakua amekosa kisheria? Na iwapo wamemuambia akimuoa huyo mschana ataikosa radhi yao nini hukmu yake, Maana Hadiyth za haki ya watoto juu ya wazazi, sijaona kuwa wazazi ndio wamchagulie mke mtoto wao, Nifaidisheni Allaah awabariki

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ni jambo la wazi na dhahiri katika Sheria yetu Tukufu, ya Kiislamu kuwa kila ‘Ibadah ina masharti ya kusihi kwake. Nikaah (ndoa) nayo ni ‘Ibaadah ambayo imewekewa masharti ili kusihi kwake. Miongoni mwa masharti ni:

 

  1. Kukubali kwa msichana anayeolewa na kuridhika kwake kuolewa na kijana Fulani.

  2. Kukubali kwa walii wa msichana, mfano babake ndiye wa awali akiwepo. Akiwa ameaga dunia basi babu ya msichana mzaa baba, kisha kakake na kadhalika.

  3. Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

  4. Kukubali kwa mvulana bila kushurutishwa na yeyote yule.

 

 

Haya ni masharti yakipatikana basi ndoa inakuwa imesihi kisheria. Ikiwa wazazi wa mvulana hawakuridhika ndoa itakuwa imesihi na kutolewa radhi mwanzo hakufai kuwepo na jambo kama hilo halifiki wala halitawafika wawili waliooana.

 

Inatakiwa tuelewe pamoja na kufahamu kuwa wazazi nao wana haki na inatakiwa uwasikie na kuwatii katika jambo ambalo si la maasiya. Ikiwa wazazi wamemkataa msichana ambaye unataka kumuoa jambo linalofaa kwako kufanya ni kukaa nao na kuzungumza nao kwa njia ya busara na nzuri sababu ya wao kukataa hilo jambo la kheri. Huenda wazazi wana mambo kumhusu msichana na hawataki wewe uingie katika shimo la taabu na shida. Wao wana hekima zaidi kukuliko na huenda wanamjua huyo msichana zaidi unavyomjua wewe kwani huenda wamemuona kuanzia yulki mchanga.

 

Haifai kwa mtoto kuwa mshindani kwa wazee wake. Ukiona kuwa wazazi wamekosea katika tathmini yao kumhusu huyo msichana basi kaa nao uzungumze nao kwa uzuri na wema na uwafahamishe na kuwakinaisha. Ikiwa hawataki kukusikiliza basi jaribu kuzungumza na maami au wajomba zako ambao wako karibu nawe ili wazungumze na wazazi wako. Pia ni bora katika jambo kama hili kabla hata hujaenda mbali utake ushauri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah. Ule ushauri utakaopata baada ya Swalah hiyo ndio utakaouchukua.

 

Katika Uislamu mwenye kuchagua mke ni kijana lakini kijana anaweza kuwapatia jukumu hilo wazazi kwani hasa kina mama wanawajua wasichana hasa ikiwa wamezaliwa mtaani kwenu kuliko wewe.

 

Tunakuombea usahali katika jambo hili na Allaah Aliyetukuka Awalainishe wazazi wako wakubali yale unayotaka yakiwa na kheri nawe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share