Kuapa Kwa Msahafu (Qur-aan) Inafaa?

SWALI:
 
 
 
Assalam alaykum warahmutullahi wabarakatuh, sina budi kumshukuru M/Mungu kwa mpaka hapa nilipifika, M/Mungu atughufirie dhambi zetu na atujaaliye wenye kuipenda dini yetu na tupate uongofu kwake Amin, na nyinyi wana wa Alhidaaya M/Mungu awamiminie kheri zake kwa kutuelimisha na mambo mengi humu.Amin
 
Suala langu : Mimi naishi UK katika utaratibu wa nchi kuna wakati tunafanikiwa kupata passport sasa kabla hujakabidhiwa passport huwa unaitwa kula kiapo ndio upewe na kiapo hicho cha kumtii QUEEN na sheria zake sasa huwa kuna viapo vya aina tatu (1) CHA KIISLAM (2) CHA CHRISTIAN (3)NACHA MTU AMBAYE HANA DINI kama mimi muislam nitachagua cha Islam sasa je hichi kiapo kitakuwa kinakubalika na sheria za kiislam kwa sababu mimi sitomtii Queen na kama hakikubaliki ni vipi nile kiapo na kiapo cha kukamata mas-haf kinakubalika? na kama hakikubaliki tukikamata mash-haf nakuapa hatutokuwa tunamkufu M/mungu? Na kama hujaambiwa uchaguwe kiapo wakikuapisha cha kikiristo je itakuwaje? Naomba mnielimishe kwani ni jumla ya mazingira tunayoishi.
 
WABILLAHI TAWFIQ
Wassalam alaykum warahmatullahi wabarakatuh.
 


 
 
 
 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Suala lako hili ni Swali muhimu linalowahusu ndugu zetu wanaoishi nchi ze Kimagharibi.
 
 
Kuapa kwa maneno ya Allaah kunakubalika kwani maneno yake ni miongoni mwa sifa Zake.
 
Ama kutumia msahafu na kuapa kwa kuushika haifai kwa sababu utakuwa hujataja jina la Allaah bali umeashiria kwenye msahafu ambao ni kitabu kilichotengenezwa kwa karatasi na wino pamoja na kwamba unaweza kusema kuwa unakusudia maneno yaliyomo ndani ambayo yanatoka kwa Allaah! Lakini kwa kufanya hivyo kunahesabika kuwa ni kiapo ambacho si kwa Allaah bali cha msahafu. Na kuapa kwa kitu chochote haifai isipokuwa ni kuapa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Pekee kwani kuapa kinyume Yake huwa ni shirk. Makatazo haya tumepata kutoka katika Hadiyth ifuatayo:
 
 
 
 
 
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( مَنْ حَلَفَ  بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ كَفَرَ أَوْ أَشْرَكَ))  رواه الترمذي   وأبو داود   وصححهالألباني في صحيح الترمذي .
 
 
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeapa pasi na Allaah, atakuwa amekufuru ameshiriki [amemshirikisha Allaah])) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
 
 
Vile vile kuapa kwa nia ya kutaka kukanusha jambo la uongo, kwa maana mtu anaposhadidiwa kuwa kafanya jambo fulani, lakini yeye akakanusha kuwa hakutenda jambo hilo, hulazimishwa ashike msahafu, au atie mkono wake ndani ya msahafu na afanye kiapo. Japokuwa atasema mfano: "WaLLaahi sikutenda jambo kadhaa na kadhaa" au mfano anapotaka kukiri jambo kuwa kalitenda aseme: "WaLLaahi nimefanya kadhaa na kadhaa" atakuwa ameapia msahafu badala ya kumuapia Mwenyeezi Mungu kwa kusema ‘WaLLaahi’, na hivyo itakuwa haikubaliki kisheria kama tulivyoona katika dalili katika Hadiyth hiyo ya juu.
 
 
Hakuna yeyote anayeruhusiwa kuapa kwa kitu chochote kingine pasi na Allaah. Ni Allaah Pekee Anayeweza kuapa kwa vitu vyovyote Avitakavyo, mfano: mbingu, jua, usiku, mchana, majabali, matunda au chochote Atakacho, kwani Yeye Ndiye Muumba wa hivyo vitu. Mifano tunaona mingi katika Qur-aan Anavyoapia mwanzoni mwa baadhi ya Surah, mfano:
 

وَالسَّمَاء وَالطَّارِقِ   -  وَالْفَجْرِ   -  وَالشَّمْس    - وَاللَّيْلِ  -   وَالضُّحَى   -   وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ   -   وَالْعَصْرِ

((Wassamaai Wat-Twaariq – Walfajr – Washamsi – Wallayl – Wadhwuhaa – Wattiyn Wazzaytuun – Wal-‘Aswr))    

 

Hata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haikumpasa kuapia chochote, na ndio maana tunaona mara nyingine akisema anapotaka kuapa:

((والذي نفسي بيده ))

((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake…..)) [Akimkusudia Allaah]

 
 
 
 
 
 

 Kuapa kwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kunapasa kwa kutumia herufi tatu pekee nazo ni 'wa', 'ta', na 'bi' Kwa maana kusema "WaLLaahi", "TaLLaahi", na "BiLLaahi".     

 
Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu hukmu ya kuapia msahafu alijibu: "Hairuhusiwi kuweka nadhiri au kuapa isipokuwa kwa Allaah au moja ya sifa Zake. Ikiwa mtu ataapa kwa jina la Allaah, basi hakuna haja tena kuleta msahafu kwa ajili ya kuapa kwa sababu kuapa kwa msahafu haikufanyika zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba. Hata baada ya Qur-aan kukusanywa katika kitabu kimoja hawakuwa wakiapia msahafu bali mtu alikuwa akiapa kwa Allaah bila ya kushika msahafu" [Fataawa Nuur 'Alaad-Darb]
 
 
 

Ama kwa mujibu wa maelezo ya wale waliokwishaapishwa huko Uingereza, ni kuwa watu hukusanywa kwa pamoja na huwa wanapewa maelekezo yaliyomo kwenye karatasi jinsi ya kutamka utiifu kwa Malkia, na hakuna anayeshurutishwa au kuambiwa ashike msahafu wakati anapofanya hivyo, au kusikilizwa anachotamka wakati huo.

Kwa hali hiyo, kunaonyesha kuwa hakuna uzito huo ulioutaja na hivyo mtu kuwa na khiyari katika jambo hilo.

 

Wa Allaahu A’alam

 
 
Share