Fadhila Za Hijaab

 

 

Fadhila Za Hijaab

 

Imefasiriwa na Salwa Muhammad

 

Alhidaaya.com

 

 

Hijaab ni tendo tiifu kwa Allaah na kwa Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kasema katika Qur-aan:

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia kasema:

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ 

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, [An-Nuwr: 31]

 

Juyuubihinna: Wanachuoni wastahifu kutoka katika zama za as-Salafus Swaalih (watangu wema) wamekhitalifiana kama vazi (Jilbaab) linalofunika mwili lazima lifunike mikono na uso au laa. Leo, wanachuoni wanaoaminika wanasema kuwa mikono na uso lazima ifunikwe. Wanachuoni wengine wanasema bora kwa wanawake kufunika mwili wao mzima.

 

 

Hijaab ni ‘Iffah (Stara)

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kaifanya Hijaab dhahiri kuwa ni takaso na hayaa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59]

 

 

Katika aayah hiyo hapo juu kuna ushahidi kuwa utambulifu wa kuonekana uzuri wa mwanamke ni madhara kwake. Na pindi sababu hiyo ya vile vyenye kusababisha mvuto na vishawishi vitakapoondoka, basi makatazo hayo huondoka. Hii ni kama tunavyoona kwa upande wa wanawake vizee ambao wanaweza kuwa wamepoteza kila kipengele cha kuvutia. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kahalalisha kwa wao kuweka pembeni buraa zao na kuonyesha sura na mikono yao, lakini ni bora zaidi kuweka stara zao.

 

 

Hijaab ni Twahara (Utakaso)

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kautonyesha hekima nyuma ya Shari'ah ya Hijaab:

 

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ 

Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. [Al-Ahzaab: 53]

 

Hijaab ni muundo wa usafi kwa mioyo ya waumini wa kiume na kike kwa sababu ni kinga au kiziuzi dhidi ya matamanio ya moyo. Bila ya Hijaab, moyo unaweza kutamani mambo machafu. Na hivyo ndio maana moyo upo safi zaidi wakati mwanamke anapojifunika, au kuhifadhiwa (na Hijaab) na vile vile inazuia fitna (matendo maovu). Hijaab inakata taamuli (fikra) mbovu na matamanio mabovu ya moyo.

 

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٣٢﴾

Enyi wake wa Nabiy!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake; mkiwa na taqwa, basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika. [Al-Ahzaab: 32]

 

 

Hijaab Ni Ngao

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

 

"Allaah, Aliye juu, ni Pepo, ni Hayii (Mwenye Kustahi), Sittiyr (Kinga). Anapenda Hayaa na Sitr (Kinga)" [Abu Daawuud]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia kasema:

 

"Mwanamke yeyote anayevua (hajisitiri sawasawa) nguo zake mbele ya yeyote zaidi ya mume wake (ima kwa kuijionyesha au kusifiwa), amevunja kinga ya Allaah juu yake".

 

Hadiyth hii inaonyesha namna ambavyo kitendo kinalipwa kutokana na uzuri au ubaya wake.

 

 

Hijaab ni Taqwah (Ucha wa Allaah)

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿٢٦﴾

Enyi wana wa Aadam! Kwa yakini Tumekuteremshieni libasi (nguo) inayositiri tupu zenu na libasi ya mapambo. Na libasi ya taqwa ndiyo bora zaidi. Hizo ni katika Ishara za Allaah ili wapate kukumbuka. [Al-A‘araaf: 26]

 

Hizi zama tulizonazo hivi sasa, mtindo mingi ya mavazi iliyopo ulimwenguni leo, ni ya kujionyesha tu na aghlabu sana kuchukuliwa kama ni stara ya mwili wa mwanamke. Lakini kwa wanawake waumini, makusudio ni kujihifadhi miili yao na kuficha maumbo yao. Kama walivyoamrishwa na mwenyewe (Allaah). Na hilo ni tendo la Taqwa (Ucha  wa Allaah).

 

 

Hijaab Ni Iymaan

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hakuyaeleza maneno yake kuhusu Hijaab ila kwa wanawake Waumini (al-Muuminaat). Katika sehemu nyingi kwenye Qur-aan Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anarejea kutaja "Wanawake Waumini"! Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha), mke wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliwambia baadhi ya wanawake wa kabila la Banu Tamiym waliokuja kumtembelea yeye (Radhwiya Allaahu ‘anha) na wakawa wamevaa nguo nyepesi, yaani nguo ambazo si stara kwa mwanamke wa Kiislam. Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akawaambia: “Ikiwa nyinyi ni wanawake Waumini, basi hakika, hilo sio vazi la mwanamke Muuminah analotakiwa kuvaa, na ikiwa sio wanawake Waumini, basi shauri yenu ikiwa mnaona mnafaidika”

 

 

Hijaab ni Hayaa

 

Kuna Hadiyth mbili Sahihi ambazo zinasema: "Kila Dini ina maadili na maadili ya Uislamu ni Hayaa" (Ibn ‘Abdil-Barr, al-Mundhiry na kutoka katika kitabu cha at-Targhiyb wa at-Tarhiyb cha Shaykh al-Albaaniy), na "Hayaa ni katika Iymaan na Iymaan imo katika Pepo" [at-Tirmidhy]

 

 

Hijaab ni (Ghiyrah) Ghera

 

Hijaab inaungana na hisia za kimaumbile ya Ghera, ambayo ni lazma kwa mwanamme aliyekuwa hapendi kuona watu wakimwangalia mke na watoto wake wa kike. Ghera ni mtukutiko unaochemka kwa mwanamme unaomsukuma kuona wivu na kuwakinga wanawake waliokuwa wamehusiana nae kutoka kwa wageni na wasio Maharimu zao. Mwanamme mkamilifu wa Kiislamu ana Ghera (wivu) kwa wanawake wote wa Kiislamu kuwakinga hao wanawake na matamanio na uchu wa wanaume. Katika Itikio la matamanio, wanaume wanawaangalia wanawake wengine kwa uchu na matamanio na hawajali kama wanaume wengine wanafanya hayo kwa wake zao na watoto wao wa kike. Mchanganyiko wa kijinsia na kukosekana Hijaab ni jambo lenye kuangamiza Ghera ya wanaume. Uislamu unachukulia Ghera ni sehemu ya Iymaan. Heshima ya mke na binti au mwanamke yeyote wa Kiislamu ni lazima iheshimiwe na kulindwa.

 

Share