Wanyama Ambao Tumehalalishiwa Kuwala

   

SWALI:

 

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwake Allaah Subhanahu Wataala kwa kunipatia uwezo wa kuandika swali langu, na nategemea jibu jema toka kwenu.

mimi niliwahi kusoma kitabu kimoja ambacho kila milango tafauti, jina lake melisahau. Sasa katika kitabu hicho kinaelezea kuwa Mtume Muhammad S.A.W aliwahi kula Farasi na pia amekataza kuliwa punda anaefanyishwa kazi. Jee hili suala la wanyama hawa kuhalalishwa kuliwa ama laa likoje? Naomba unifafanulie pia unielezee ni kitu gani kinatubainishia kuwa mnyama huyu anafaa kuliwa na huyu hafai. Napenda kujiondoshea hofu kwani hofu itanipelekea kufanya maovu.

Ahsante, nategemea jibu jema. Allaah Karim.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako hili zuri kuhusu halali na haramu katika Dini yetu Tukufu. Ni vyema kabla ya kuingia katika kiini cha suala lenyewe tutazame baadhi ya misingi ya kisheria kuhusu halali na haramu.

 

Msingi wa Kwanza: Asili ya vitu vyote ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kaviumba kwa manufaa ya wanaadamu ni halali na mubaha, wala hapana la haramu ila lile ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake wameliharamisha kwa kulitaja katika Shari‘ah. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na Amekubainishieni waziwazi Alivyokuharamishieni” (6: 119).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

La halali ni lile Alilolihalalisha Allaah katika Kitabu Chake na la haramu ni lile Aliloliharamisha Allaah katika Kitabu Chake, na ambalo hakulitaja basi ni msamaha kwenu” (at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Msingi wa Pili: Kuhalalisha na kuharamisha ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake peke yao. Hii si haki ya Shaykh wala Sultani wala Khalifa. Anayefanya hilo huwa amejiingiza katika ushirikina. Qur-aan inatufahamisha kuwa Watu wa Kitabu waliwapa watawa na wanazuoni wao uwezo wa kuhalalisha na kuharamisha, hivyo kuwaweka katika daraja ya uungu (). Vile vile, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amewakarapia washirikina ambao walikuwa wakiharamisha na kuhalalisha mambo bila idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), kama alivyosema haya katika Surah Yunus (10): Aayah 59 na Suratun Nahl (16): Aayah 116.

Msingi wa Tatu: Kuhalalisha ya haramu ni sawa na shirki. Uislamu umewakemea na kuwafanyia tashdidi zaidi wale wenye kuharamisha kwa sababu ya kuwazuilia watu na kuwadhiki bila ya sababu katika mambo ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amewapa wasaa na nafasi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga vita sana msimamo huu wa kupindukia mipaka katika Dini na kuwakaripia wenye tashdidi hizi na kuwapasha habari ya kuangamia kwao:

Ee, wamehiliki wenye kutia tashdidi katika Dini; ee, wamehiliki wenye kutia tashdidi katika Dini; ee, wamehiliki wenye kutia tashdidi katika Dini” (Ahmad, Muslim na Abu Daawuud).

Waarabu wakati wa ujahili walikuwa na tabia hii. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuelezea kuhusu mipaka Yake

:

Enyi Mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyo kuhalalishieni Allaah, wala msiruke mipaka. Hakika Allaah hawapendi warukao mipaka. Na kuleni katika vile alivyokuruzukuni Allaah vilivyo halali na vizuri; na mcheni Allaah ambaye nyinyi mnamwamini” (5: 87 – 88).

 

Msingi wa nne: Jambo huharamishwa kwa ajili ya uovu wake na madhara yake.

 

Msingi wa Tano: Haramu ni haramu kwa wote.

Hakika Uislamu umetuwekea wazi wanyama walio halali kuliwa nasi na wale walio haramu ili tusipate shida katika hilo. Wanyama walioharamishwa ni kama wafuatao:

1.     Mzoga.

2.     Damu ya kuchuruzika.

3.     Kinachochinjwa kwa asiyekuwa Allaah.

4.     Nyama ya Nguruwe. Aina hizi nne (4) ni kwa mujibu wa Qur-aan 5, ayah ya 3.

5.     Punda kwa kauli ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuliwa kwa nyama ya punda na ndoa ya Mut‘ah siku ya Khaybar” (al-Bukhaariy na Muslim).

Hadiyth nyingine ni ile ya Jaabir bin ‘Abdullah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: Siku ya Khaybar tulichinja farasi, nyumbu na punda. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza sisi kula nyama ya nyumbu na punda, lakini hakutukataza kula nyama ya farasi (Abu Daawuud). Katika riwaya ya Muslim imeongezeka: “Punda wa mjini”.

 

Huenda wengine wakawa wameiona Hadiyth iliyonukuliwa na Abu Daawuud kutoka kwa Khaalid bin al-Waliid (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kula nyama ya farasi”. Tufahamu kuwa Hadiyth hii ya Khaalid (Radhiya Allaahu ‘anhu) mwanzo ni dhaifu na wengine wanasema hata kama ingekuwa sahihi, hata hivyo, hukumu yake imebatilishwa/imefutwa (Mansuukh).

Ama kuhusu kula nyama ya farasi, ni rai ya Maulamaa wengi kwamba inaruhusiwa kutokana na Hadiyth Swahiyh zilizosimuliwa:

عن جابر بن عبد الله رضي الله عنهما قال :" نهى رسول الله صلى الله عليه وسلم يوم خيبر عن لحوم الحمر الأهلية ورخص في الخيل"   رواه البخاري   ومسلم  

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: " Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza kula nyama ya punda na akaruhusu nyama ya farasi" [al-Bukhaariy na Muslim]

 

وعن أسماء بنت أبي بكر رضي الله عنهما قالت :  " نحَرْنا على عهد النبي صلى الله عليه وسلم  فرساً فأكلناه"   رواه البخاري   ومسلم   

Na kutoka kwa Asmaa bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Tulichinja farasi zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumla" [Al-Bukhaariy na Muslim]   

وعن جابر رضي الله عنه قال : "سافرنا مع رسول الله صلى الله عليه وسلم وكنا  نأكل لحم الخيل ونشرب ألبانها   رواه الدارقطني والبيهقي . قال النووي : بإسناد صحيح  .

Na kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: "Tulisafiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tukawa tunakula nyama ya farasi na tunakunywa maziwa yake" [Ad-Daaraqutwniy na Al-Bayhaqiy. An-Nawawy amesema kuwa isnaad yake ni Swahiyh]

 

 

Maulamaa wengine pamoja na Abu Haniyfah na Maswahaba zake wawili wao rai yao ni kwamba ni makruuh (inachukiza) kula nyama ya farasi. Wamenukuu Aayah ya Qur-aan na Hadiyth. Ama Hadiyth waliyonukuu ni hiyo tuliyoinukuu juu ya Khaalid bin Waliyd ambayo imetambulikana kuwa ni dhaifu. Aayah waliyonukuu ni:

((وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَة))

((Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo)) [An-Nahl: 8]

Wamesema kwamba Allaah Hakutaja kuwala bali kataja kuwa ni vipando, ila kataja kula wanyama (ngamia, ng'ombe n.k.) katika Aayah ya nyuma yake ambayo inasema:

((وَالأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ))

 

((Na nyama hoa Amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala)) [An-Nahl: 5].

Maulamaa wamejibu kuhusu hoja hii kwamba kutajwa kuwapanda na mapambo haimaanishi kwamba manufaa yao yamewekewa mipaka kwa hayo tu, bali, kupandwa kwao hao wawili kumetajwa kwa sababu ni aghlabu kuwa hao ndio wanatumika kwa hivyo. Hii ni kama Aayah ambayo Allaah Anasema:

 ((حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالْدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنْزِيرِ))

((Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe)) [Al-Maaidha: 3]

 

Hapa nyamafu imetajwa kwa sababu ndio inayoliwa aghlabu. Na pia pamoja na Allaah kutaja uharamu wa nyama ya nguruwe, hiyo haimaanishi kuwa ni nyama yake tu ndio iliyo haramu, bali Waislamu wamekubaliana kwamba shahamu yake, damu yake na sehemu nyingine zote za nguruwe zimeharamishwa.

Na hali kadhaalika, pamoja na kuwa Allaah Hakutaja kubeba mizigo farasi, japokuwa Amesema kuwa wanyama wengine kama ngamia n.k wanabeba:

((وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ))  

((Na hubeba mizigo yenu)) [an-Nahl: 7]

 

hii haimaanishi kwamba ni haramu kuwabebesha mizigo farasi!

Kwa hivyo, hoja ya Abu Haniyfah na wafuasi wake, haina nguvu kama tunavyoona.

6.    

Wanyama mwitu wenye meno ya kushambulia na kula wanyama wengine na ndege wenye makucha. Hiyo ni kwa mujibu wa Hadiyth: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kula kila mnyama wa mwitu wenye kutia meno (wenye kula nyama) na kila ndege mwenye kutumia makucha” (al-Bukhaariy na Muslim).

Wanyama kuruhusiwa kuliwa au kukataliwa ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Yeye ndiye Anayejua yaliyo na faida nasi na maslahi kwetu. Kulingana na maelezo ya hapo juu ni wazi kuwa punda ni haramu kuliwa na farasi ni halali. Hekima kwa hayo ni nini hali hawa wawili wanafanana? Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anajua zaidi hilo, kwetu sisi ni kusema:

 

Tumesikia na tunatii” (2: 285).

 

Ni muhimu kuwafunza watoto kuanzia utoto wao kujua na kuelewa mas-ala ya halali na haramu. Katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhuma):

Fanyeni amali katika kumtii Allaah na ogopeni kumuasi Allaah, waamrisheni watoto wenu kufuata amri na kuacha makatazo, kwani hilo litawakinga wai na nyinyi na moto” (Ibn Jariyr na Ibn al-Mundhir).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share