Mume Anataka Kunipa Talaka Kwa Sababu Siwezi Kumlea Mtoto Wa Mke Wake

 

SWALI:

 

Al-hidaaya,

 

Asalam Alaikum, Warahmatulahi wabarakatu. Nashkuru kwa barua yenu na naelewa kwanini ni vigumu kutoa namba za simu.

 

Anyway tatizo langu ambae sijui nifanyeje, kwa kweli ina husu ndoa yangu. Kwa ufupi, nina mume wangu ambae nisha zaa nae mtoto moja wakiki na nina mwingine njiani (alhamdulilah). Niliolewa Mke wa pili ambapo mi na mke wa kwanza Al-hamdullilah tuna elewana vizuri. Ila kulitokea na ugomvi kipindi cha nyuma ambapo tulimfumania mume wetu na mwanamke mwingine huyu wa tatu tena sio wa ndoa, kisha sote tuka ondoka na kurudi kwa wazazi wetu. Ala kuli Hal, baada ya mda, mimi nika kubali kurudi kwenya nyumba, ila mwenzangu mpaka leo Zaidi ya mwaka kakataa.

 

Kuridi kwangu, mume wangu akaniletea mtoto wa mke mwenzangu ambae kasha shindikana ili nimlee kwa utaratibu ipaswavyo, nikatia juhudi zangu zote na kujitahidi kumrudisha na kumungoza mtoto ipaswavyo mana mtoto (Miaka yake 9) alikua hataki kusoma, dini wala shule, alikua akitoka kwa shangazi yake saa 12 asubui anarudi saa 4 usiku. (Mume wangu ni dereva wa magari makubwa kwa hiyo kukaa kwake nyumbani ni adimu) Mtoto utakavyo mwambia hasikii wala hataki kujua anafanya ajuavyo yeye. Alipo anza mchezo mchafu wa kuchezeana na watoto wenzake wakiume, ndio baba yake kamuondoa na kumleta kwangu. Mimi nikajitahidi kuletana nayeye shuleni na madrasa kidogo tukawa na maendeleo. Ila sasa mtoto ka anza mchezo yake akiwa kwangu kila ninapo mueleza baba yake anapo toka safari, anaona kama mi ni mwongo, mana sielewi mtoto alivyo miliki baba huyo. Anambagua mwanagu wazi mbele ya mwenzie, anaweza kuleta nguo akamletea wa kiume asimlete wa kike napo muliza kwanini ana fanya hivi ana sema wa kike mdogo haelewi kitu. Ila kwa yote tuna jenga imani gain kwa hao watoto?

 

Pili Mtoto wa kiume ameanza kutumia lugha chafu kwenye nyumba na napo mwambia kitu ananijibu kua nitamfanya nini… Juzi nikamueleza mumewangu kinacho endelea ila kaja ju na kunifokea na kunaimbia kama ntashindwa kumlea mwane huyu wa kiume basi atamuondoa nay eye pia (mume wangu) ataondoka. Akasema pia “utakapo jifungua ntakutumia talaka yako”. Nikaona tena maswala ya talaka, kisa ni mtoto nikajaribu kumueleza kua mtoto wangu (wa kike ) pia ni mwanae kwanini atubague kama vipi wampeleke kwa mama yake pengine kule atapata malezi wanavyotaka. Ila kwa mimi sizani ntaweza mana nina mtoto wa kike na kwa vile huyu wa kuime yupo exposed vibaya anaweza kumzuru wa kwangu. (mana kasha wai kuchukua kiberiti na kumchoma mwanagu mgu) nilipomueleza baba yao kasema alikua akimtania dada yake.

 

Hebu ndugu zanguni niambieni nifanyeje? Mume wangu ninapenda ila nami pia nampenda mwanagu… Ila ubuaguzi ikiwa wazi hivi au inafika anitishie Talaka kisa mtoto wa mke mkubwa mi nifanyeje?

 

Hi maneneo nawaelezeni ndugu zangu waislamu, naomba ushauri, mana nyumba yetu haieleweki tena saa zote natishiwa maswala ya mtoto wa kiume… pamoja na kwamba mtoto kasha jua baba anafoka na huyu mama juu yangu amesha kua na kichwa. Sijui nifanyeje…

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunasikitika na hali yako hiyo. Kutokana na maelezo yako tumeona kwamba umejitahidi uwezavyo kumlea mtoto wa mumeo kwa wema na ihsaan na ujira wako utaupata kutoka kwa Mola wako. Lakini sasa kama mtoto huyo anakushinda kutokana na tabia zake chafu, ujeuri na uongo n.k., huna budi kufanya lililo bora lenye maslahi na wewe pamoja na mtoto wako wa kike, kwani kama ulivyosema una khofu asije kumdhuru mwanao.

 

 

Katika hali kama hii ambayo hakuna masikilizano na mmoja katika wanandoa anashikilia atakavyo bila ya kutaka kumfahamu mwenzake, na hali inafikia kutengana, hakuna budi ila kuita kikao cha jamaa zako na jamaa zake ili mjadili matatizo hayo na kupatikane suluhisho kama tunavyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

 

((وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُواْ حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلاَحًا يُوَفِّقِ اللّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا))

 

((Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari)) [an-Nisaa: 35]

 

Na ikiwa bado atashikilia atakavyo nawe una haki ya kukhofu mwanao wa kike asidhurike na yeye anakutia kitisho cha kukuacha, hivyo tunaona hakuna ila mawili; ima huna haja ya kujilazimisha kwake kwani kukubali kumlea mwanawe ambaye humuwezi kutakuletea madhara wewe katika ndoa yako baina yako na mumeo na pia huenda akadhurika mtoto wako wa kike ambaye ni muhimu kumpatia malezi mema. Kufanya hivyo itakuwa unajikalifisha jambo ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mwenyewe Hakutaka kutukalifisha katika jambo tusiloweza kulibeba:

 

 ((لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا)) 

 

((Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ila kwa kadiri ya iwezavyo))   [Al-Baqarah: 286]

 

 

Juu ya hivyo ni kwamba mumeo hakuamini usemalo kuhusu mtoto wake wa kiume, japokuwa umejitahidi kumlea na kumuongoza. Badala ya kukusaidia wewe uweze kumlea mwanawe anakuzidishia mashaka ya kukuhutumu uongo. Hivyo inakuwa ni kumpandisha kichwa mwanawe azidi kukufanya atakalo.

 

Pia kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa hana uadilifu katika malezi kama kumbagua mwanao. Yote hayo yanachangia kuonyesha kwamba maisha ya ndoa naye ikiwa hatajirekebisha yatakuwa magumu kwako. Hivyo inampasa kwanza ajirekebishe ili uweze kuendeleza ndoa yako kwa usalama au sivyo tunaona kwamba itakuwa ni matatizo yasiyokwisha.

 

La pili, ni kwamba ukiweza kuwa na subra kwa kuendelea kumlea mwanawe na hapo hapo ukawa unaweza kumhifadhi mtoto wako wa kike, basi hivyo ni bora zaidi kwani subira ina malipo makubwa kwa Mola wetu. Pia kubakia katika ndoa ni stara ya mwanamke. Ukiweza ni kheri na huku umuombe sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akufanyie wepesi na Amuongoze mtoto huyo, na muombe Akupe masikilizano na mumeo.

 

 

Hukututajia uko nchi gani kwani tungeliweza kukupa namba za simu za Mashaykh wetu wakusaidie ikiwa uko Afrika Mashariki' ima Tanzania au Kenya.

 

 

 Na Allaah Anajua zaidi

Share