Istihaadhwah Damu Inayoendelea Baada Ya Hedhi Na Hukumu Zake

Istihaadhwah Damu Inayoendelea Baada Ya Hedhi Na Hukumu Zake

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI LA KWANZA:  

 

Asalamu aleykum

Naomba munisaidiye tatizo langu napata hedhi kwa kuda mrefu siku 24 hadi mwenzi sasa nataka kujua baada ya siku ngapi naweza kufunga na kuswali mana nimesikia baada ya mda kadhaa huwa ni maradhi kwahiyo waweza kufunga na kuswali inatoka kidogo kidogo inakuwa kama makruu

Naomba munisaidye tatizo hilo ahasantum wabilah taufq

SWALI LA PILI:

 

Sheikh, mimi nauliza kama wapata hedhi mara mbili kwa mwezi hio huwa ni isthadhwa au nikitu kingine?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hali yako hiyo bila ya shaka itakuwa ni hali ya Istihaadhwah nayo ni damu inayomtoka mwanamke isiyokuwa ya hedhi au nifaas bali ni damu ya kawaida kwani haiwezekani mwanamke kuwa na hedhi siku zote hizo au hadi ifikie mwezi. Kwani ingawa ‘Ulamaa wameona kuwa hakuna idadi maalumu za hedhi na nifaas na rai mbali mbali zimetolewa kuhusu muda au damu ya hedhi na nifaas kama ifuatavyo:

 

1-Mwanamke ahesabu idadi ya siku zake za hedhi za kawaida yake ilivyo mfano kama ni siku saba basi akifikisha ya nane afanye ghuslu zilizobakia ni Istihaadhwah.

 

2-Ikiwa ni kawaida yake ya hedhi siku saba basi asubiri hadi apitishe siku kumi na tano.

 

3-Atazame sifa za damu zifuatazo ili aweze kutofautisha baina ya damu ya hedhi na ya Istihaadhwah:    

 

Rangi:   

    

Damu ya hedhi huwa ni nyekundu iliyoiva kukaribia kuwa nyeusi na damu ya Istihaadhwah  ni nyekundu inayong'aa (bright red)

 

Shakili yake: 

 

Damu ya hedhi huwa nzito, ama ya Istihaadhwah huwa ni nyepesi.

 

Harufu:     

 

Damu ya hedhi huwa ina harufu ya kukirihisha, ama damu ya Istihaadhwah  haina harufu kwani huwa inatoka katika mishipa ya kawaida katika mwili wa bin Aadam.

 

Lakini kutokana na hali yako kufikisha siku ishirini na tano au mwezi basi hakuna shaka kuwa hiyo ni Istihaadhwah kwani sio twabi'iy (natural) mwanamke kuwa katika hedhi mwezi mzima takriban. Hivyo uhesabu ima idadi ya siku zako za kawaida kisha utazame kama damu inayotoka baada ya hapo inazo sifa zilizotajwa hapo juu au la. Au uhesabu siku kumi na tano kisha zilizobakia zitakuwa ni Istihaadhwah na utafuata hukmu za Istihaadhwah kama ifutavyo:

 

Hukmu Za Istihaadhwah:

 

Hukmu za Istihaadhwah ni sawa sawa na hukmu za mwanamke anapokuwa katika twahaara yaani mwanamke asiyekuwa katika hedhi. Hivyo anatakiwa aswali na kufunga kama kawaida kama ilivyokuja dailili ifuatayo:

 

 عن عائشة قالت : جاءت فاطمة بنت أبي حبيش إلى النبي صلى الله عليه وسلم فقالت : يا رسول الله إني امرأة أستحاض فلا أطهر أفأدع الصلاة ؟ فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( لاَ ، إِنَّمَا ذَلك عِرْقٌ وَلَيْسَ بِحَيْضٍ ،فَإذا أَقْبَلتْ حَيْضتُكِ فَدَعِي الصَّلاةَ , وَإِذَا أَدْبَرتْ فَاغْسِلي عنكِ الدمَ ثُمَّ صَلِّي))  رواه البخاري   ومسلم.

 

Kutoka  'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Faatwimah bint Hubaysh alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Ee Rasuli wa Allaah, mimi ni mwanamke ninayepatwa na Istihaadhwah, siwi katika twaahara, je niache kuswali?" Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hapana huo ni mshipa tu na sio hedhi. Unapopata hedhi acha kuswali na inapomalizika osha damu [baada ya kufanya ghuslu) kisha Swali.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn katika kuelezea maana yake kasema: "Ni mshipa tu. Hivyo inafahamika kwamba ikiwa damu inayotoka katika mshipa pamoja na damu inayomtoka mtu kutokana na operesehi haitambuliki kuwa ni damu ya hedhi. Kwa hiyo yanayokuwa haraam katika hedhi hayawezi kuwa haraam katika hali hii, na mwanamke anatakiwa aswali, afunge inapomfikia……Ramadhwaan" [Majmuw' al-Fataawa Ibn 'Uthaymiyn 11/Swali Namba 226]

 

Pia

 

وعن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم اعتكف معه بعض نسائه , وهي مستحاضة ترى الدم , فربما وضعت الطست تحتها من الدم . رواه البخاري.

Na kutoka 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa I'tikaaf na mke wake mmoja  naye alikuwa katika Istihaadhwah akiona damu. Mara nyingine aliweka chombo kukingia damu. [Al-Bukhaariy]

 

Kutokana na hiyo Hadiyth pamoja na nyinginezo, ni dalili kwamba hakuna tofauti ya mwanamke mwenye Istihaadhwah na mwanamke asiyekuwa na hedhi isipokuwa yafuatayo:

 

 

Wudhuu Kwa kila Swalaah:

 

Afanye wudhuu kwa kila Swalaah kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimwambia mkewe:

 

“Basi fanya wudhuu kwa kila Swalaah.’ [Al-Bukhaariy]

 

Ina maana kwamba asifanye wudhuu mapema kabla ya Swalaah kuwadia bali afanye wudhuu pale pale  anapotaka kuswali.

 

 

Kujisafisha kabla ya kufanya wudhuu:

 

Anapotaka kufanya wudhuu kwanza ajisafishe vizuri na alama zote za damu ziondoke. Kisha ajiwekee pamba sehemu zake siri ili kuzuia damu isitoke wakati anaposwali kama Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwambia Hamnah:

 

( أنعت لك الكرسف  فإنه يذهب الدم)) ، قالت : فإنه أكثر من ذلك ، قال : ((فاتخذي ثوباً)) . قالت : هو أكثر من ذلك . قال  ((فتلجمي))  الحديث

 

“Nakudokeza uweke kipande cha pamba kwani itanyonya damu.” Akasema (Hamnah): Ni zaidi ya hivyo [yaani haifai kitu damu bado inatoka]. Akasema (Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam akamwambia: “Tumia kitambaa.” Akasema: Ni zaidi ya hivyo: Akasema “Basi ikaze vizuri nayo.”

 

Akifanya hivyo mwanamke mwenye Istihaadhwah kisha ikitoka damu basi haitodhuru kitu kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Faatwimah bint Abi Hubaysh:

 

((اجتنبي الصلاة أيام حيضك ثم اغتسلي وتوضئي لكل صلاة ، ثم صلي ، وإن قطر الدم على الحصير))  رواه أحمد وابن ماجة

.

“Acha kuswali wakati wa siku zako za hedhi, kisha fanya ghuslu na ufanye wudhuu kwa kila Swalaah hata damu ikimwagika katika mswala.” [Ahmad na Ibn Maajah]

 

Maingiliano na mume:

 

‘Ulamaam wamekhitilafiana kuhusu kuruhusiwa jimai (kitendo cha ndoa) ikiwa hakutakuwa na mashaka ya kuacha kabisa. Lakini rai iliyo Swahiyh ni kwamba inaruhusiwa katika kila hali kwa sababu kwanza wanawake wengi walikuwa wakipata Istihaadhwah zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wala hakukuwa na makatazo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   au Rasuli  Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwakataza jimai bali kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala)

 

فَاعْتَزِلُواْ النِّسَاء فِي الْمَحِيضِ

 

Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi [Al-Baqarah: 222]

 

inafahamika kwamba haikukatazwa kujitenga nao nyakati nyinginezo. Na ikiwa wameruhusiwa kuswali basi kufanya jimai ni tendo lisilo na uzito sana kama kuacha kuswali.

 

Haitokuwa sawa kama italinganishwa kwa kupima kwa Qiyaas (analogy) baina ya kujimai na mwanamke aliyekuwa katika Istihaadhwah  kuwa ni sawa sawa kwa sababu uhakika ni kwamba hawako sawa  japo kuwa wengine rai zao wameona kuwa ni haraam. ['Risaalah fid-dimaa' at-twaabi'iyyah lin-Nisaai' - Shaykh Ibn 'Uthaymiyn - “Risala Kuhusu Damu Za Maumbile Za Wanawake” ya Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn]

 

Na makala hii ndefu ya “Risala Kuhusu Damu Za Maumbile Za Wanawake” ya Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn imetafsiriwa kwa lugha ya kiswahili ambayo imewekwa katika kitabu kidogo ambacho kinapatikana katika maduka ya vitabu vya Dini mjini Dar-es-Salaam. Ni kitabu kizuri ambacho kinamama wanapaswa kuwa nacho.

  

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo, na faida tele uongeze elimu kuhusu mas-ala haya ya hedhi:

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share