Jimai: Kujamiiana Kitendo Cha Ndoa Na Mume Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

SWALI:

 

Asalamaleikum ndugu zangu wa Alhidaaya.

 

Kufanya mapenzi kama mke wa ndoa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan inakubalika hivyo? ahsante sana. Nategemea kupata uhakika kutoka kwenu.  asalamaleikum ndugu zangu wa Alhidaaya.

 


 

 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho 

Swali lako hukufafanua kama kufanya kitendo cha ndoa wakati wa Swawm au baada ya kufuturu. Ikiwa ni wakati wa Swawm basi ni haraam na dhambi kubwa na kafara (malipo) yake yatakuwa ni kuachia huru mtumwa, na kama hamtoweza  basi mfunge miezi miwili mfululizo (bila ya kukatiza), na ikiwa hamtoweza kufanya hivo basi mlishe masikini 60 au watu wanaohitaji. 

Kufanya hivyo inawapasa wote wawili mume na mke kila mmoja afanye sehemu yake. Lakini kama mke alilazimishwa kufanya kitendo hicho basi yeye haimpasi kulipa 'kafara'.

Kwa maelezo zaidi soma Fataawa katika viungo vifuatavyo:

 

Hukmu Ya Kutenda Kitendo Cha Jimai Mchana Wa Ramadhaan

 

Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Zaidi Ya Mara Moja Kwa Siku Moja Ya Ramadhaan

 

Je, Mke Anatakiwa Kulipa Kafara Ikiwa Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Na Mumewe Siku Za Ramadhaan?

 

 

 

Ama ikiwa baada ya kufuturu, hakuna shaka kuwa imeruhusiwa. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَى نِسَآئِكُمْ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ عَلِمَ اللّهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ فَالآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُواْ مَا كَتَبَ اللّهُ لَكُمْ وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّواْ الصِّيَامَ إِلَى الَّليْلِ وَلاَ تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ تِلْكَ حُدُودُ اللّهِ فَلاَ تَقْرَبُوهَا كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللّهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ))

 

((Mmehalalishiwa usiku wa Swawm kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Allaah Anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo Amekukubalieni toba yenu na Amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni Aliyokuandikieni Allaah. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka Allaah, basi msiikaribie. Namna hivi Allaah Anabainisha Ishara Zake kwa watu ili wapate kumcha)) [Al-Baqarah: 187] 

 

Kabla ya kuteremshwa Aayah hizo Maswahaba walikuwa wakijizuia kuonana na wake zao nyakati za usiku za Ramadhaan. Ilikuwa wameruhusiwa kula na kunywa na kujimai kutoka mwanzo wa Magharibi baada ya kufuturu hadi wakati wa 'Ishaa pekee. Wale waliolala kabla ya 'Ishaa au walioswali Swalah ya 'Ishaa hawakuruhusiwa kunywa au kula au kujimai hadi usiku wa siku ya pili yake. Hivyo waliliona ni jambo gumu na hadi baadhi ya Maswahaba walishindwa kuvumilia wakaingia kufanya jimai. Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akalifanya liwe jepesi kwa Rahma Yake.

 

Ruhusa ya kujimai hivyo ipo kuanzia baada ya kufuturu hadi kabla ya Alfajiri kuingia kama ilivyotajwa katika hizo Aayah ((Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku…))

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share