Wameingiliana Baada Ya Alfajiri – Nini Hukmu yake? Na Je, Swawm Inafaa?

 

Wameingiliana Baada Ya Alfajiri – Nini Hukmu yake? Na Je, Swawm Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Nakutakieni kila kheri,na mwezi mtukufu wa Ramadhani utuwie wa kheri na baraka. Swali langu ndio hili, nina mke na tupo katika mwezi mtukufu Ramadhani, imefika usiku tumekwenda kulala na usingizi kutupitia ktk chumba hamna saa ,kurupu umejishtua na kumtafuta mke, uku ukitazama bado kunaonesha giza, unajua bado muda upo, je swaumu ipo? natayari imegundulika muda wadaku umepita, na mapenzi tayari kupeyana. Kila la kheri na swaum njema.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Waislamu wanapaswa kuzingatia sana matendo yanayobatilisha Swawm na ambayo ni haraam, kama kufanya jimai mke na mume akiwa katika Swawm.

 

 

Amri kama ya kufunga mwezi wa Ramadhwaan ambao ni mwezi mmoja tu tulioamrishwa tubakie katika Taqwa na kutekeleza Swawm ipasavyo. Kwa Rahma Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Ameturuhusu tule, tunywe, na kuruhusiwa yote mengineyo ambayo mja amejizuia mchana wa Swawm. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ ۚ وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿١٨٧﴾

 Mmehalalishiwa usiku wa kufunga Swiyaam kujamiiana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah Anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkijifanyia khiyana nafsi zenu, hivyo Akapokea tawbah yenu na Akakusameheni. Basi sasa waingilieni na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku). Kisha timizeni Swiyaam mpaka usiku. Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf Misikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Allaah Anavyobainisha Aayaat (na hukmu) Zake kwa watu wapate kuwa na taqwa [Al-Baqarah: 187]

 

 

 

Sasa vipi muda wote huo usiwe wa kumtosha Muislamu kufanya yote anayoyatamani na kusubiri hadi karibu na Alfajiri ndio atake kufanya? Kwa nini usifanye hima ya kujiwekea saa ukahakikisha kuwa utaamka muda wa kutosha kamakama Alivyotuwekea Shariy’ah hiyo Allaah ('Azza wa Jalla)?    

 

 

Makosa hayo ni kujitakia mtu mwenyewe kujiingiza katika shida na mashaka ya kulipa kafara yake ambayo ni kuacha huru Mtumwa mmoja Muumini au kufunga miezi miwili mfululizo.

 

 

Ikiwa hukujua hakika kuwa wakati wa Alfajiri umewadia unatakiwa ulipe siku hiyo na uombe maghfirah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Lakini ikiwa ulijua au ulikuwa una hisia kuwa wakati umekwisha lakini tendo lile likawa limekukolea hadi ukashindwa kujizuia, basi itabidi ulipe kafara yake. Na mkeo ikiwa alitaka mwenyewe kujimai nawe pia naye itabidi atimize kafara hiyo na ikiwa ulimlazimisha basi yeye atakuwa hana kafara hiyo ila tu ailipe siku hiyo moja.  

 

 

Haipasi kufanya mchezo na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) khaswa katika mwezi huu mtukufu, kwani amri kama hizo ukienda nazo kinyume basi utapata matatizo duniani na Aakhirah, na matatizo ya kidunia ni kama hayo ya kulipa kafara ambayo si rahisi na wengi hawawezi kuitekeleza.

 

Tunawapa nasaha ndugu zetu Waislamu wote katika mwezi huu wawe na tahadhari kubwa kufanya kinyume na ipasavyo ili kujiepusha na dhambi, kulipa kafara na kubakisha Swawm zenu katika usalama wake.

 

 

Ingia katika viungo vifuatavyo usome maelezo zaidi ya hukmu zake:

 

Alifanya Jimai (Kitendo Cha Ndoa) Bila Ya Kujua Kwamba Alfajiri Imeingia

 

Kufanya Jimai Katika Mwezi Wa Ramadhaan

 

Kitendo Cha Ndoa Wakati Wa Ramadhaan

 

Hizi ni Fataawa zote zinazohusu Kafara ya Swawm:

 

Kulipa Swawm Na Kafara

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share