Ndoa Na Aliyesilimu Asiyekuwa na Walii Inafaa

SWALI:

Asalaam alaikum!naomba kupata ufumbuzi wa suala hili kwani mimi nimeoa mwanamke ambaye amekubali kuwa muisilamu kwa kunifata mimi pia kukubali uisilamu,lakini wazazi wake ni wakiristo bado na katika ndoa yetu kulikua hakuna mtu wa upande wake mwanamke isipokua rafiki wa mbali tu,je vipi ndoa imekubalika?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwako ewe ndugu yetu kwa swali lako hilo zuri.

Alhamdulillaahi, Uislamu kwetu ni mfumo kamili wa maisha nao haukuacha chochote ila umetuelezea kinaganaga. Kila kitu katika Dini yetu kina masharti na kanuni zake ndoa ikiwa mojawapo. Miongoni mwa masharti ya ndoa ni lazima mwanamke awe na walii wake, kwani hakuna ndoa bila ya walii.

 

Asiyekuwa Muislamu anaposilimu wazazi wake hawawezi kuwa walii wake lakini hata hivyo ni vyema kuwajulisha kuhusu suala hilo la ndoa la binti yao na hata kuwaalika kuhudhuria harusi hiyo. Hiyo ni njia ya kuwavutia katika Uislamu. Uislamu umeweka kuwa msichana asiyekuwa na walii basi sultani au Qaadhi anakuwa walii wake. Na katika sehemu ambayo hakuna ma-Qaadhi basi kiongozi mmoja wa kidini kama Imaam anaweza kuchaguliwa akiwa ana maadili ya Kiislamu na muruwa kutekeleza jukumu kama hilo. Rafiki wa mbali hawezi kuwa walii wake katika suala nyeti kama hilo. Pia tuelewe kuwa Uislamu umekataza urafiki baina ya mwanamme na mwanamke. Ikiwa hakuna kabisa watu kama hao wanaoweza kuwa walii wake basi anaweza kumchagua yeyote katika Muislamu muadilifu kusimamia jambo hilo.

 

Hakika ni kuwa ndoa hiyo haina tatizo ikiwa masharti mengine yametimizwa kama kupatikana mashahidi wawili waadilifu, kuridhika kwa mwanamke mwenyewe na kumpatia mahari yake kamili mliyosikilizana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share