Anafanya Kazi Inayohusu Ubebaji Wa Maboksi Yenye Ulevi

SWALI:

Asalam aleikum warahmatulahi. kuna rafiki yangu twafanya kazi kiwanja kimoja {EUROPE} sehemu ambayo niko mimi, ni sehemu ya mboga. lakini huyu rafiki yangu hufanya sehemu ya kulord makeji ya supermarket, sasa swali langu katika keji hizo kuna maboksi mengine yana tembo. nilazimu kwake kufanya hivyo. niliwahiyi kumwambiya lakini. akaniambiya kuwa yeye, hufanya kila siku. nainapotokeya basi lazima afanye hivyo. kwa sababu yeye hufanya sehemu ya goods in, inapotokeya upungufu wa watu ndiyo yeye hupelekwa huko.

kufanya hivyo, sasa nauliza kwa hayo niliyoyaeleza kwake ni haramu kufanya hivyo. shukran. Mungu awazidishieni ilimu na awape subra amen amen.



 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako zuri. Hakika hilo ni tatizo linalowapata watu wengi wenye kwenda Bara Ulaya kwa sababu moja au nyingine lakini sababu kubwa ikiwa ni kupata ajira yoyote ile.

Uislamu umehimiza sana Muislamu awe ni mwenye kutafuta na kufanya kazi ili aweze kujikimu kimaisha na kuweza kusaidia jamaa zake. Dini yetu tukufu imefanya ufanyaji wa kazi kuwa ni Ibadah na hivyo mwenye kuchuma chumo la halali kupata thawabu. Ufanyaji wa kazi ulikuwa ndio mfumo wa Manabii wote akiwemo wa mwisho, Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo Uislamu umeweka misingi na kanuni za kutekeleza shughuli hizo. Msingi mkubwa ukiwa ni wajibu wa Muislamu kufanya kazi ya halali tu kinyume chake ni haramu kwa Muislamu.

Msingi mkubwa katika Uislamu wa kukataza kitu kilicho haramu ni kuwa bidhaa ikiwa haramu basi vyote vinavyosaidia vinakuwa haramu. Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hakukataza zinaa tu bali vyote vinavyomkaribisha mtu kutekeleza kitendo hicho kibaya. Amesema Aliyetukuka:

Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo (zinaa) ni uchafu mkubwa na ni njia mbaya kabisa” (17: 32).

Kwa ajili hiyo, ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukataza pombe tu bali pia mbebaji, mtengenezaji, mpandaji mimea au matunda kwa ajili hiyo, mnywaji, na wengineo kama tunavyoona katika Hadiyth ifuatayo:

Kutoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelaani mambo kumi yanayohusiana na ulevi; mwenye kuukamua (kuutengeneza), Mwenye kutengenezewa, mnywaji, mbebaji, anayebebewa, anayeendesha (kuupeleka ulevi), muuzaji, anayekula thamani yake, anayenunua na anayeuza. [At-Tirmidhiy na Ibn Maajah)

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuwa haifai kwetu sisi kusaidiana katika uovu: Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” (5: 2).

Hivyo, haifai kwake kufanya kazi ya kubeba masanduku ya pombe kwa hali yoyote ile. Inafaa kwake afanye juhudi sana ili asiwe ni mwenye kufanya hivyo. Na jambo hilo litafanikiwa tu pale atakapozungumza na mkubwa ili asiwe ni mwenye kufanyishwa kwa sababu za kidini.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share