Mabwana Harusi Walichanganyiwa Wake Zao

 

SWALI:

Mzee mmoja alikuwa na watoto wawili wakiume, kisha wale vijana wakatafuta wachumba    na wachumba walio wapata ni ndugu. Ikawa kwa kila mchumba ni mwenye kutowa mahari kisha ndoa zikafungwa, Ilipofika usiku wakawa ni wenye kuletewa wake zao lakini wale waliowaletea wake zao wakawa ni wenye kuchangaya, mke wa huyu wakampeleka huyu na huyu mke wake wakampeleka kwa huyu, na kila mmoja akalala naye mpaka asubuhi, kunako hili jambo ktk dini hukumu yake ni ipi?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kutoka kwetu za dhati kwa ndugu yetu kuhusu swali lako hilo. Kwangu naliona ni la ajabu lakini katika dunia hii mengi hutokea.

Tunasema ni ajabu kwani ingekuwa wanandoa wamefuata Sunnah za bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi tatizo kama hilo halingekuwa ni lenye kutokea.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuachia maagizo kadhaa kuhusu mahusiano baina ya wanaotakana kuingia katika ndoa wafanye. Moja katika hilo ni mume na mke kuonana kabla ya ndoa mbele ya maharimu wa mke. Hili ni agizo alilopatiwa Mughiyrah bin Shu‘bah (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Je, umemuona?” Nikasema: “La”. Akasema: “Nenda ukamuone kwani hilo ni bora zaidi katika kujenga mapenzi na makubaliano” (an-Nasaaiy kwa Isnadi iliyo sahihi).

 

Usiku wa harusi (baada ya Nikaah), mume anafaa amwekee mkewe mkono wa kichwa kisha aombe du’aa aliyoifundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Allaahumma inniy as-aluka khayraha wa khayra maa jabaltaha ‘alayhi wa a‘udhubika min sharrihaa wa sharri maa jabaltaha ‘alayhi – Ee Allaah, hakika mimi nakuomba kheri ya mke huyu na kheri ya maumbile uliyomuumba nayo, na najilinda Kwako na shari yake, na shari ya maumbile uliyomuumba nayo” (Abu Daawuud na Ibn Maajah). Hili linafanyika katika weupe na sio kiza totoro.

Inafaa mume ampatie mkewe kinywaji kama maziwa anywe kisha naye anywe kwenye chombo hicho hicho. Baada ya hapo wanafaa wanandoa waswali rakaa mbili kama alivyoagiza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakapooa mmoja wenu na ikawa ni siku ya mjengo na aswali rakaa mbili na amuamuru mkewe aswali nyuma yake, kwani Allaah Ataajaalia katika nyumba hiyo kheri” (al-Bazzaar). Baada ya Swalah hiyo waombe du‘aa ya kuleta baraka katika ndoa hii na kuwa pamoja kwa kheri.

Swali ni kuwa je, haya yote yalifanywa kizani au hayakufanywa? Ikiwa yalifanywa vipi tena walichanganyiwa wake. Ikiwa walikuwa wameonana na kuzungumza kabla ya usiku huo mambo yote yatawafahamisha kama ndio waliotakana au sio wao? Inawezekana tu labda kutofahamiana ikiwa wanawake ni pacha moja waliofanana kwa kila kitu rangi, mwenendo, sauti, sura, umbile na kadhalika.

Kosa hilo linatendeka tu ikiwa mke ameletwa, mume akafanya haraka ya kumaliza uchu wake bila ya kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tulizotaja hapo juu. Mbali na kusema hayo huenda kosa hili likatokea kwa mwanadamu kwani yeye ni mkosa. Huenda pia waliowaleta mabibi harusi walifanya kusudi. Ikiwa ni hivyo basi watu hao waliofanya hivyo watakuwa ni wenye makosa na madhambi na itabidi watubie na warudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kuomba msamaha na maghfira. Ikiwa walifanya hilo kwa kukosea au kutojua basi wao hawatakuwa na dhambi. Mabibi na mabwana harusi ikiwa wengine wamekosea au wamefanya makusudi hawatakuwa na dhambi kwani wao hawajui hayo waliotendewa. Jambo hili ni muhimu na linatakiwa tuchukue tahadhari zinazofaa.

 

Ikiwa jambo hilo ni kama lilivyoelezwa inafaa wake baada ya kujulikana kwa waume zao wa kweli wapelekwe kwao ikiwa ni asubuhi na yaliyopita yamepita. Wao hawatakuwa na kosa wala madhambi yoyote. Pia ni muhimu kwa wake hao wawe ni wenye kusafishwa ili kusiwe na mbegu ya mwingine iliyobaki ndani siku hiyo wanayojua kuwa wake wamechanganywa. Itabidi pia waume wasikutane na wake zao kwa kuhakikisha kuwa hakuna kuchanganya kwa kizazi cha hao ndugu na madada. Au kwa wepesi zaidi wawe ni wenye kupima kama wana mimba au hawana kabla ya mume na mke wa kihakika kujamiana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share