Duaa Gani Kuomba Ya Kujiokoa Na Zinaa

 

Du’aa Gani Kuomba Ya Kujiokoa Na Zinaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Ni dua gani mtu anaweza kusoma ili apate mchumba mwema (mwanamuke awo mwanawume). Ni duwa gani mtu mzinifu anaweza kusoma ili Allah Amnusuru na zina?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Katika jamii ambayo tunaishi ndani hivi leo hakika maasiya yamezidi maradufu mpaka mema yanaonekana kuwa ni mabaya na maovu kuwa mema.

Zinaa katika jamii zetu za leo inaonekana kuwa ni jambo la sawasawa tu mbali na kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatufahamisha:

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu umekuwa na ni njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32]

 

Hapa Allaah  Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatupatia muongozo kuwa dawa ya zinaa ni kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kukupeleka huko. Hayo ni kama kusalimiana na msichana asiyekuwa maharimu yako kwa kumpa mkono, kukaa faragha na msichana, kuangalia filamu na picha chafu, kwenda disco, kuwa katika hafla za mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake na mengineyo.

 

Pia inafaa uwe na marafiki ambao ni wema wanaoweza kukuelekeza katika mambo ya kheri.

 

Kushikamana na ‘Ibaadah tofauti kwani ‘Ibadah zote zinatuepusha na machafu. Kwa mfano, Swalaah, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aala) Anasema:

 

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾

Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. Na bila shaka kumdhukuru Allaah ni kubwa zaidi. Na Allaah Anajua yale mnayoyatenda. [Al-‘Ankabuwt: 45]

 

Pia kujilazimisha kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) mchana na usiku kwa nyiradi mbali mbali.

 

Hali kadhalika kuweza kutafakari juu ya yule ambaye utazini naye. Ima huyo atakuwa ni mama, dada, binti, shangazi, khalat (mama mdogo au mkubwa) wa mtu. Basi ujiulize Swali ni kuwa je, wewe utakubali au kuridhika mamako au dadako au binti yako azini na mtu. Ikiwa hupendelei jamaa zako wafanyiwe kitendo hicho kwa nini unataka kufanya na dada au mama au shangazi za wengine?

 

Ukitafakari hayo basi yatakuepusha na zinaa isipokuwa akili yako iwe kama ya hayawani.

 

Njia bora ya kuweza kujiepusha na zinaa ni kutafuta msichana mwenye Dini na maadili mema ufunge naye ndoa na ikiwa hujaweza hilo kwa sababu moja au nyingine fanya bidii ujilazimishe na Swiyaam kwani Swawm ni kinga  kama alivyotuambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

الصِّيام جُنَّة يَستَجِنُّ بها العبدُ من النار

((Swiyaam ni kinga itamuokoa mja kutokana na moto [wa Siku ya iyaamah])) [Ahmad 2/402, Swahiyh At-Targhiyb 1/411 na Swahiyh Al-Jaami’ 3880]

 

Ama kujiepusha huko hakuna du’aa fulani ambayo unaweza kuisoma hasa kwa suala hilo. Bali ni juu yako umuombe Allaah (‘Azza wa Jalla) na jambo hilo hasa unapoinuka katika Swalaah za usiku. 

 

Pia hakuna du’aa maalumu ya kupata mchumba bali inafaa ufanye juhudi ya kutafuta msichana ambaye ana sifa zilizopendekezwa na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyosema katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تُنْكَحُ الْمَرْأَةُ لأَرْبَعٍ: لِمَالِهَا  وَلِحَسَبِهَا   وَجَمَالِهَا  وَلِدِينِهَا. فَاظْفَرْ بِذَاتِ الدِّينِ تَرِبَتْ يَدَاكَ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Mwanamke huolewa kwa sababu nne; Kwa mali yake, nasaba yake [ukoo], uzuri wake na Dini yake. Tafuta mwenye Dini ubakie salama)). [Al-Bukhaariy na Muslim] (yaani usiharibikiwe katika maisha yako). 

 

Unaweza pia kutuma jamaa zako wa karibu kukutafutia.

 

Baada ya kupatikana na kabla ya kupeleka posa inafaa uswali Swalaah ya Istikhaarah kumtaka shauri Allaah (‘Azza wa Jalla):

  

Tunakuombea kwa Allaah (‘Azza wa Jalla)  Akuepushe na zinaa pamoja na kukupatia msichana mwema mwenye Dini mtakayesikilizana kwa njia nzuri.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share