Mas-ala Mbali Mbali Kuhusu Talaka

 

SWALI:

 

Bismillahi rahmani rahim. Ama baada ya salam hizo naomba kuwasilisha maswali yangu kwa uafafanuzi na majibu kwa mujibu wa kitabu kitukufu qurani na mafunzo ya Mtume wetu mtukufu Muhammad (S.A.W):

 

1. Kuna talaka za aina ngapi katika Uislamu?

2. Talaka tatu hutolewa wakati gani? Kwa kosa gani? 

3. Mume aliyemwacha mkewe kwa talaka tatu aweza kumrejea?

4. Ni mambo gani haramu kwa mume aliyemwacha mkewe kwa talaka tatu kutendewa ama kumtendea mtalaka wake?

5. Neno talaka rejea lina maana katika dini yetu?

6. Nini haki za mke aliyeachwa toka katika mali za mume aliyemwacha?

 

Ahsanteni,

Wabillahi tawfiq asalaam aleikum warahmatullahi taallah wabarakatuh  

 


 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji swali kuhusu mas-ala ya talaka katika Uislamu.

Ama kuhusu swali lako la kwanza, twasema yafutayo:

Mwanzo kabisa maana ya talaka ni kufungua fungo la ndoa kwa tamko bayana au kwa kinaya (isiyo moja kwa moja). Ama vigawanyo vyake ni kama vifuatavyo:

 

i)                   Talaka ya Sunnah: Nayo ni mume kumuacha mkewe katika utwahara ambao hujawahi kukutana naye kimwili.

ii)             Talaka Bid‘ah (Uzushi): Ni mume kumuacha mkewe akiwa katika siku zake za ada, au katika kipindi cha damu ya uzazi, au katika twahara aliyomuingilia au kumuacha talaka tatu kwa mpigo mmoja. Mwenye kutoa talaka aina hii huwa ana madhambi lakini talaka yenyewe huwa imepita ila ile ya tatu huhesabiwa kuwa ni moja tu.

iii)              Talaka Baain: Ni ile ambayo mume anamuacha mkewe akakosa haki ya kumrejea kwa kuwa eda imekwisha. Hivyo, mume huyo akawa ni mposaji kama waposaji wengine na mke akikubali inabidi mume apose, atoe mahari na ifungwe Nikaah upya.

iv)            Talaka Rejea: Hii ni ile ambayo mume anamiliki haki ya kumrejea mtalaka wake. Huku ni mume kumrejea mkewe katika kipindi cha eda la kuachwa talaka ya kwanza au ya pili.

Pia zipo aina tofauti za kutoa talaka. Nazo ni kama zifuatazo:

a)     Talaka Bayana: Hii ni talaka iliyo wazi kabisa isiyo na utata aina yoyote. Nayo ni kama kusema: “Nimekuacha”. Na talaka hii si lazima ukusudie kwani tamko lako linatosha.

b)     Talaka Kinaya (isiyo bayana): Hii ni lazima ukusudie talaka kwa kuwa tamko lako si bayana kama kusema: “Nenda kwa ndugu zako” au “Usiseme na mimi” na yanayofanana na hayo. Ikiwa talaka imenuiwa basi itakuwa imetuka.

c)      Talaka ya hapo kwa hapo: Ni ile ambayo inapotolewa mke huachika hapo hapo bila kuchelewa. Hiyo ni kusema: “Wewe umeachika” baada ya mume kutamka hayo mke atakuwa ameachika.

d)     Talaka ya Kutungika: Ni ambayo mume ameitungika juu ya kitu kingine kuwa kitu hicho akikifanya au akikiacha atakuwa ameachika. Mfano ni mume kusema: ukitoka hapa nyumbani utakuwa umeachika” na mfano kama huo.

e)     Talaka ya Khiyari: Hii ni mume kumwambia mkewe nimekupatia khiyari kutengana nami au kubaki nami. Akichagua kutengana talaka itakuwa imepita. Hii ni kama Anavyotueleza Allaah Aliyetukuka kuhusu uteuzi waliopatiwa wakeze Mtume na Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Suratul Ahzaab (33), ayah ya 28.

f)       Talaka kwa Uwakala au Maandishi: Mume kama atamuwakilisha mtu mwingine kumuacha mkewe au akamuandikia mkewe talaka akimuarifu katika maandishi hayo kuwa amemuacha, mke atakuwa ameachika.

g)     Talaka kwa Kuharamisha: Hii ni kusema kwa mume kumwambia mkewe: Wewe ni haramu kwangu au unakuwa haramu, kama atakusudia kwa tamko hilo talaka itakuwa talaka, na kama atakusudia dhihari itakuwa dhihari naye atawajibika kwa tamko hilo kafara la dhihari.  

Ama kuhusu swali lako la pili, ni kuwa hakuna wakati wowote ambapo mume anakubaliwa kisheria kutoa talaka tatu kwa mara moja au kikao kimoja. Kufanya hivyo ni kosa na inahesabiwa kuwa ni talaka moja peke yake katika sheria ya Kiislamu.

Ama swali lako la tatu, ni kuwa ikiwa mume amemuacha mkewe talaka tatu mara moja huhesabiwa ni moja tu. Ikiwa kwa hilo unamaanisha kumuacha mkeo kwa kumpatia talaka ya kwanza, kisha ya pili mpaka ikafika ya tatu haiwezekani kwa hao wawili kurudiana kama mume na mke mpaka mwanzo mke aolewe na mume mwengine wakutane kimwili kisha aachwe. Hapo utaweza kumrudia tena. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Allaah. Na hii ni mipaka ya Allaah Anayoibainisha kwa watu wanaojua” (2: 230).

 

Ama kuhusu swali lako la nne, ni kuwa haifai kwa watalaka kudhulumiana kwa njia moja au nyingine. Pia haifai kwao kuweka chuki na uadui baina yao na kutoa siri walizoweka baina yao kwa wengine. Kuoana ni kwa wema na kuachana ikiwa hapana budi lazima kuwe kwa wema. Pia haifai kwa mume kuchukua kutoka kwa mtalaka wake alivyompa kama hadiya kwa njia yoyote ile na vile vile si halali kwa mke kuchukua visivyo vyake kwa njia yoyote ile.

Ama kuhusu neno Talaka Rejea ni kama tulivyolieleza hapo juu kuwa hii ni ile talaka ambayo mume anamiliki haki ya kumrejea mtalaka wake nako ni kumrejea mkewe katika kipindi cha eda la kuachwa talaka ya kwanza au ya pili. Allaah Aliyetukuka Anatueleza: “Na wanawake walioachwa wangoje peke yao mpaka tahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alichoumba Allaah katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya suluhu” (2: 228).

Ama swali lako la mwisho (la sita) ni kuwa pindi mke anapoachwa mume ana wajibu wa kumtizama kwa makaazi, chakula, mavazi, matibabu, na yote anayofanyiwa mke akiwa katika ndoa. Ama katika mali mke hatakuwa na haki yoyote isipokuwa walikuwa na ushirika katika hilo. Ikiwa hali ni hiyo kila mmoja atapata haki yake kama walivyopatana wao katika unyumba wao na ile kazi inavyokwenda. Mke atakuwa na yale mali aliyopatiwa na mtalaka wake wakiwa katika ndoa. Haifai kwa mume kuchukua alivyompa kwa njia yoyote ile. Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa wake zenu” (2: 229).

Na pia:

Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa mali nyingi, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhuluma na kosa lilio wazi?” ().

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share