Mfano Wa Neno Zuri (La Tawhiyd) Ni Kama Mti Mzuri (Mtende) Na Faida Zake

 

Mfano Wa Neno Zuri (La Tawhiyd) Ni Kama Mti Mzuri (Mtende) Na Faida Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾

Je, huoni vipi Allaah Amepiga mfano wa neno zuri kama mti mzuri mizizi yake imethibitika imara na matawi yake yanafika mbinguni? (marefu mno).

 

تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا ۗ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٥﴾

Unatoa mazao yake kila wakati kwa idhini ya Rabb wake. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu ili wapate kukumbuka. [Ibraahiym (14: 24-25)]

 

 وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الْأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍ ﴿٢٦﴾

Na mfano wa neno baya ni kama mti mbaya uliong’olewa juu ya ardhi hauna imara.  

 

ثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ﴿٢٧﴾

Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo. [Ibraahiym (14: 26-27)]

 

 

Aayah hizi tukufu zina mafunzo muhimu kwetu yanayohusu Tawhiyd, (Kumpwekesha Allaah bila kumshirikisha na chochote) kuthibitika kauli duniani na Aakhirah na pia kutuonyesha tofauti ya matunda yanayotokana baina ya  maneno mawili haya; neno la tawhiyd kuwa matunda yake ni kheri tupu, na neno la kufru kuwa matunda yake ni mabaya hayana thamani wala faida yoyote bali ni shari tupu.

 

'Aliy bin Abiy Twalhah amesimulia kwamba 'Abdullaah bin 'Abbaas amesema kuhusu:

 

 كَلِمَةً طَيِّبَة  

 ((neno zuri))

 

ina maana ni kushuhudia: “Laa ilaaha illa-Allaah” (Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah).

 

 كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾

Je, huoni vipi Allaah Amepiga mfano wa neno zuri kama mti mzuri mizizi yake imethibitika imara na matawi yake yanafika mbinguni? (marefu mno).

 

تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا ۗ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٥﴾

Unatoa mazao yake kila wakati kwa idhini ya Rabb wake. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu ili wapate kukumbuka. [Ibraahiym (14: 24-25)]

 

 

'Abdullaah bin 'Abbaas amesema kuhusu ((Kama mti mzuri)) "Ni mti wa Peponi" [At-Twabariy 16: 573]

 

Ad-Dhwahaak, Sa'iyd bin Jubayr, 'Ikirimah, Mujaahid na wengineo wamesema, maana ya mfano huu wa huo mti mzuri unaotoa matunda yake kila mara, ni kama Muumini ambaye naye hufanya vitendo vyema kila mara usiku na mchana navyo vinapanda juu kila mara mchana na usiku. [At-Twabariy 16:572-573]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutajia jina la mtu huo  kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

 عَنْ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَال: كُنَّا عِنْد رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: ((أَخْبِرُونِي عَنْ شَجَرَة تُشْبِه - أَوْ - كَالرَّجُلِ الْمُسْلِم لاَ يَتَحَاتّ وَرَقهَا صَيْفًا وَلاَ شِتَاء وَتُؤْتِي أُكُلَهَا كُلّ حِين بِإِذْنِ رَبّهَا)) قَالَ اِبْن عُمَر: فَوَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة وَرَأَيْت أَبَا بَكْر وَعُمَر لاَ يَتَكَلَّمَانِ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّمَ فَلَمَّا لَمْ يَقُولُوا شَيْئًا. قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وآله وَسَلَّمَ: ((هِيَ النَّخْلَة)). فَلَمَّا قُمْنَا قُلْت لِعُمَرَ: يَا أَبَتَاهُ وَاَللَّه لَقَدْ كَانَ وَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة. قَالَ: مَا مَنَعَك أَنْ تَتَكَلَّم؟ قُلْت: لَمْ أَرَكُمْ تَتَكَلَّمُونَ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّم أَوْ أَقُول شَيْئًا.  قَالَ عُمَر: لَأَنْ تَكُون قُلْتهَا أَحَبُّ إِلَيَّ مِنْ كَذَا وَكَذَا - البخاري

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما)  ambaye amesema: "Tulikuwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akauliza: ((Niambieni kuhusu mti unaofanana na (au) ulio kama Muislamu, ambao majani yake hayaanguki wakati wa majira ya joto, wala wakati wa majira ya baridi, na hutoa matunda yake kila mara kwa idhini ya Rabb wake)). Ibn ‘Umar akasema: “Niliufikiria kuwa ni mtende, lakini niliona vibaya kujibu nilipoona Abuu Bakr na ‘Umar hawakujibu”. Akasema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Ni mtende)). Tulipoondoka, nilimwambia ‘Umar: “Ee baba yangu! Wa-Allaahi nilihisi kuwa ni mtende”. Akasema: “Kwa nini basi hukutaja?” Nikasema: “Nilikuoneni kimya, nikaona vibaya kusema kitu”. Akasema ‘Umar: "Ungelisema, ingelikuwa bora kwangu kuliko kadhaa na kadhaa” (Yaani ningelikuwa na fakhari zaidi kuwa wewe mwanangu ndiye uliyeweza kujibu pekee). [Al-Bukhaariy]

 

 

Hebu basi tutazame sifa za mti huu mzuri (mtende) na sifa za Muumimi tuone jinsi zilivyofanana:

 

1-Mtende:

Umethibiti ardhini kwa mizizi yake

 

Muumini:

Anathibiti iymaan yake daima na huwa na iymaan ya hali ya juu.

 

 

 

2-Mtende:

Tunda lake ni zuri na tamu.

 

Muumini:

Mazungumzo na vitendo vyake ni vizuri na vya kupendeza, na si mwenye maneno maovu yanayoudhi, kudharau, kukashifu, kusengenya, kufitinisha n.k.

 

 

 

3-Mtende:

Umepambika vizuri na kufunikika.

 

Muumini:

Mavazi yake ni mazuri ya heshima.

 

 

 

4-Mtende:

Ni wepesi kula tunda lake.

 

Muumini:

Ni wepesi kujadiliana na watu kwa hoja, dalili na kwa busara.

 

 

 

5-Mtende:

Una faida kwa anayekula, kwani matunda yake yana siha mwilini na huwa ni  kinga ya maradhi, uchawi, na kila aina ya maovu kwa kula (aina ya) tende saba  (za aina ya 'ajwah) asubuhi kabla kula chochote.

 

Rejea Hadiyth kuhusu kula tende saba (za aina ya 'ajwah) asubuhi katika Al-Bukhaariy na Muslim.

 

 

Muumini:

EIimu yake anayotoa ina faida kubwa ya kuwaongoza Waislamu na wasio Waislamu kutoka katika upotofu kuingia katika hidaaya na hivyo ni kuutakasa moyo  katika usalama wa shirki na maovu mengineyo, kinyume na moyo wenye maradhi ya shirki, unafiki n.k.

 

 

 

6-Mtende:

Ni mti madhubuti sana wenye kustahmili upepo mkali.

 

Muumini:

Iymaan yake imethibiti vizuri hata anapopata misukosuko na mitihani, huwa na moyo mkubwa wa kustahmili kama ilivyothibiti katika Hadiyth:  

 

((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ،  وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

 

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lakeni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake)) [Muslim]

 

 

 

7-Mtende:

Kila unapokuwa mkubwa unazidi kutoa matunda na faida nyinginezo.

 

Muumini:

Kila anapozidi umri huongezeka elimu, busara na huzidi kunufaisha watu kwa khayr zake.

 

 

Huo ndio mfano wa neno zuri na mti mzuri.

 

 

Ama mfano wa neno ovu na mti muovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

  وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الْأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍ ﴿٢٦﴾

Na mfano wa neno baya ni kama mti mbaya uliong’olewa juu ya ardhi hauna imara. [Ibraahiym (14: 26)]

 

 

Unaelezea kutokuamini kwa kafiri kuwa ni kama  mti usiokuwa madhubuti, mti mchungu kabisa, na bila shaka vitendo vyake havipandi juu wala havitakabaliwi.

 

 

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa Humthibitisha mwenye kuamini katika maisha ya dunia na pia maisha ya Aakhirah kwa neno hilo lililothibiti kama mti, Yaani: “Laa ilaaha illa-Allaah”.

 

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ﴿٢٧﴾

Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo. [Ibraahiym (14: 27)]

 

 

Duniani huthibiti kumuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwa kuendesha maisha yake yote yakiwa katika mipaka ya Rabb wake Mtukufu. Na nje ya maisha ya dunia huthibitika kwa kuweza kujibu maswali atakayoulizwa na Malaika wawili kaburini ambao ni Munkar na Nakiyr kama ilivyotajwa katika Hadiyth: 

   

 

عَنْ الْبَرَاء بْن عَازِب رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((الْمُسْلِم إِذَا سُئِلَ فِي الْقَبْر شَهِدَ أَنْ لاَ إِلَه إِلاَّ اللَّه وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُول اللَّه فَذَلِكَ قَوْله (يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ)) البخاري  وَرَوَاهُ مُسْلِم أَيْضًا وَبَقِيَّة الْجَمَاعَة

Imepokelewa kutoka kwa Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم) amesema: ((Muislamu akiulizwa katika kaburi, atashuhudia kwamba: "Laa ilaaha Illa-Allaah wa anna Muhammadar-Rasuwlu-Allaah" (Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Rasuli wa Allaah), basi hiyo ndiyo maana ya kauli ya Allaah: ”Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah”)) [Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo]

 

   

Hadiyth nyingine imeelezea: 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاة الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَة)) قَال: ((ذَلِكَ إِذَا قِيلَ لَهُ فِي الْقَبْر مَنْ رَبّك وَمَا دِينك وَمَنْ نَبِيّك؟ فَيَقُول رَبِّي اللَّه وَدِينِيّ الإسْلاَم, وَنَبِيِّي مُحَمَّد, جَاءَنَا بِالْبَيِّنَاتِ مِنْ عِنْد اللَّه فَآمَنْت بِهِ, وَصَدَّقْت. فَيُقَال لَهُ: صَدَقْت عَلَى هَذَا عِشْت وَعَلَيْهِ مُتّ وَعَلَيْهِ تُبْعَث))  

 

Imekutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah)). Akasema: ((Hivyo atakapoulizwa kaburini; Nani Rabb wako, nini Dini yako, nani Rasuli wako? Atasema: Rabb wangu ni Allaah, Dini yangu ni Islaam na Rasuli wangu ni Muhammad, ametuletea dalili za wazi kutoka kwa Allaah, nikamuamini na nikamsadikisha. Ataambiwa: Umesema ukweli, umeishi kwa hayo, umefia kwa hayo na utafufuliwa kwa hayo)). [Atw-Twabariy (16: 596)] 

 

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuthibitishe kwa Al-Qawl Ath-Thaabit  katika maisha ya duniani na Aakhirah,   na Atuwezeshe kujibu maswali tutakayoulizwa kaburini.

 

Wa biLLaahi At-Tawfiyq

 

 

 

 

Share