Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah Ni Nini? Ipi Historia Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?
Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah Ni Nini? Ipi Historia
Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?
SWALI:
Nini Ahl Sunnah wal Jama'ah, historia yake na malengo yake. Hii Ahl Sunnah wal Jama'ah haina kasoro zozote?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Tunakushukuru ndugu muulizaji kwa swali lako hili zuri na muhimu, nasi tutajitahidi kukujibu kwa kadiri tutakavyowezeshwa na Allaah.
Maana ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
Maana ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah ni neno la Kiarabu lenye kukusanya majina mawili, kwanza ni Sunnah na pili ni Al-Jamaa’ah, ambayo yote mawili yanatafsirika kilugha kama ifuatavyo:
- As-Sunnah: maana yake ni njia, na hapa inamaanisha kufuata na kuchukua yote yaliothibiti kutoka kwa Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kauli zake, au matendo yake, au kukiri kwake; kwa dhahiri na siri.
-
Al-Jamaa’ah: Maana yake kilugha ni idadi yenye wingi, na wametofautiana Wanachuoni wa Kiislamu kuhusu maana yake kishari’ah; baadhi ya Wanachuoni wanasema kuwa Al-Jamaa’ah ni Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wengine wakasema kuwa ni Wanachuoni wa Kiislamu, kama alivyosema Imaam At-Tirmidhiy “ Tafsiri ya neno Al-Jamaa’ah kwa Wanachuoni wa shari’ah ni wataalamu wa Fiqhi (elimu ya shari’ah za Kiislamu) na Wanachuoni wa Hadiyth (maneno yaliyothibiti kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na wengine wakasema Al Jamaa’ah ni wale walioshikama na haki, hata kama watakuwa wachache, kama alivyosema Ibn Masu'ud “ Al-Jamaa’ah ni wale walioafikiana na haki hata kama watakuwa peke yako. Na baadhi ya Wanachuoni wakasema Al-Jamaa’ah ni kundi kubwa la watu walio chini ya kiongozi anayehukumu kwa mujibu wa shari’ah za Allaah na kujiepusha na matamanio na mambo ya uzushi.
Kadhalika ibara Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah ni Watu wa Sunnah na Jamaa’ah (kikundi). Kusudio la hilo ni wale watu wanaofuata vilivyo njia ya Sunnah za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) kuhusiana na Imani, Itikadi, amali na utekelezaji wa kijumla wa Dini ya Kiislamu.
Na kauli yenye nguvu miongoni mwa tafsiri hizo, ni mkusanyiko wa yote yalioanishwa na Wanachuoni wetu, kwa maana kuwa, Al-Jamaa’ah ni Swahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao ndio kioo na kielelezo cha Manhaj ya Uislamu iliyo safi, aidha wao ndio Wanachuoni na wataalamu wa Shariy’ah na Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Vilevile ndio kundi la Waislamu liliokuwa chini ya kiongozi mmoja anayeongoza kwa mujibu wa shari’ah za Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa). Na Imaam Ibn Hazm amefupisha maelezo haya kwa kusema “Ahlus-Sunnah ambao tunawazungumzia ndio watu wanaofuata haki, na kinyume chao ni watu wanaofuata mambo ya uzushi, hao (Ahlus-Sunnah) ndio Swahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ndio wale waliofuata nyayo za Swahaba katika kizazi cha (At-Taabiu'un) watoto na wafuasi wa Swahaba wa Rasuli, kisha ndio watu wa Hadiyth, na waliowafuata miongoni mwa Wanachuoni wa Fiqhi (elimu ya shari’ah za Kiislamu), kizazi kwa kizazi hadi zama tulizonazo hivi sasa.” Angalia kitabu cha Al-Milal wal Ahwa'a wan-Nihal 2/271
Majina mengine ya Ahlus Sunnah Wal Jamaa’ah
Aidha Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah wanafahamika kwa majina mengine ambayo yamebeba sifa zao, na ambayo yanatokana na maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwa majina hayo ni:
Al-Firqat An-Naajiyah (kundi litakalookolewa na moto)
Na sifa ya kundi hili imeelezwa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw amesema, amesema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((ليأتيَنَّ على أُمَّتي ما أتى على بني إسرائيلَ حَذْوَ النعل بالنعل، حتى إن كان منهُم مَن أتى أُمَّه علانية؛ لكان في أُمَّتي مَن يصنع ذلك، وإنَّ بني إسرائيل تفرَّقت على ثنتين وسبعين ملَّة، وتفترق أُمَّتي على ثلاث وسبعين ملة؛ كلهم في النار؛ إلا ملة واحدة. قالوا: ومَن هي يا رسول الله؟ قال: ما أنا عليه وأصحابي)) رواه الترمذي وحسنه الألباني
“Zitawafikia Ummah wangu zama zilizowafikia banu Israaiyl unyayo kwa unyayo, hata kama mtu atamuingilia mama yake hadharani, basi atapatikana miongoni mwa Ummah wangu atakaeigiza hivyo, hakika banu Israaiyl wamafarikiana katika matapo sabini na mbili, na Ummah wangu watafarikiana katika matapo sabini na tatu, wote wataingizwa motoni, ila tapo moja. Wakasema: ni tapo gani hilo ee Rasuli wa Allaah? akasema; ni wale ambao watakuwa kama nilivyo mimi na Maswahaba zangu” [At-Tirmidhiy imesahihishwa na Al-Abaaniy].
At-Twaaifat Al-Manswuwrah (Kundi lilionusurika)
Kundi hili limetokana na maelezo ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipolisifia kwa kusema:
(لا تزال طائفة من أمتي قائمون بأمر الله لا يضرهم من خذلهم أو خالفهم حتى يأتي أمر الله وهم ظاهرون على الناس) رواه مسلم في صحيحه،
“Halitoacha kundi katika Ummah wangu, wakisimamia maamrisho ya Allaah, hawaathiriwi na wanaowapinga au kuwakhalifu mpaka Allaah Atakapoleta amri Yake, nao watakuwa juu ya watu (wote).” [Muslim].
As-Salafus-Swaalih (Waja wema waliotangulia)
Na kundi hilo limeitwa hivi kwa sababu ya kufuata nyayo za Swahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Imamu waongofu katika karne tatu bora ambazo zilisifiwa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni zama bora kuliko zama zote baada yao, kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(خيركم قرني ثم الذين يلونهم ثم الذين يلونهم) رواه البخاري ومسلم
“Wabora wenu ni wale wa karne yangu, kisha wale ambao wanaowafuata, kisha wale ambao wanaofuatia” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Kadhaalika, hujulikana kwa majina mengine kama Ahlul-Hadiyth n.k.
Historia ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
Ama kuhusu historia yake ipo wazi kwani ilianzia wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa akiwahimiza Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) wawe ni wenye kufuata vilivyo Uislamu kama alivyoteremshiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kufuata Uislamu kikamilifu ni kufuata Qur-aan na Sunnah za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama tutakavyoona katika dalili zifuatazo:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٠٨﴾
Enyi walioamini! Ingieni katika Uislamu kikamilifu, na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi. [Al-Baqarah: 208]
Inafahamika kuwa wanadamu, Waislamu wakiwa miongoni mwao kwa wakati mmoja au mwengine wanakengeuka na msimamo wa sawa. Ili kuubakisha Uislamu katika utwahara wake, Amekuwa (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akileta kila karne mwenye kujadidi (kuifufua na kuelekeza watu kati njia ya sawa) Dini. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Hakika Allaah Anatuma kwa Ummah huu mbele (katika) ya kila karne mwenye kuijadidisha Dini kwao." [Abu Daawuwd, Al-Haakim, Al-Baghdaadiy na Al-Bayhaqiy].
Na pia kasema,
"Kutabaki katika Ummah wangu kipote kitakachosimama kwa amri za Allaah. Hawatowadhuru wenye kuwaacha wala wenye kuwapinga mpaka ije amri ya Allaah wakiwa katika hali (msimamo) hiyo hiyo." [Al-Bukhaariy].
Misingi ya Itikadi (‘Aqiydah) ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
Itikadi (‘Aqiydah) ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah inasifika kwa sifa zifuatazo:
-
Chimbuko moja la Shari’ah: Ahlus Sunnah hawategemei chanzo kingine katika misingi ya Itikadi yao zaidi ya Qur-aan, Sunnah na makubaliano ya waja wema waliotangulia, wala hawapingani na yaliyothibiti katika vyanzo hivyo kwa kutumia Qiyaas (kipimo cha akili) au rai.
-
Kuafikiana kwao na dalili sahihi kunakubaliana na maumbile, akili, na mapokeo: kwani hakuna kinachotuliza nyoyo, zaidi ya Itikadi ya waja wema waliotangulia.
-
Itikadi ya Ahlus Sunnah iko wazi na nyepesi kueleweka: Ni Itikadi iliyo nyepesi kufahamika kwa watu wa aina zote, isiyokuwa na mafumbo wala mizunguko.
Kwa kifupi, tunaweza kusema, Misingi ya 'Aqiydah ya Ahlus-Sunnah ni kufuata Qur-aan, Sunnah, Kwa ufahamu wa Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia).
Malengo ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
Ama malengo yake kwa sasa ni kuwarudisha Waislamu katika kufuata kikamilifu Uislamu (Qur-aan na Sunnah) na kuwatoa katika shirki, uzushi na kufuata matamanio ya nafsi zao.
Ikiwa mtu atasema kuwa Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah ni Uislamu wenyewe hatakuwa na makosa wala kasoro yoyote. Na kila Muislamu ni lazima awe na Itikadi hiyo kwa ubora wa Uislamu na ukamilifu wake. Hata hivyo, kwa sababu Uislamu unaelezwa na Wanachuoni kuanzia wale wa awali huenda wao wakakosea kwa kutumia dalili (hasa Hadiyth) ima dhaifu, au ya kutungwa, au kukosa kupata iliyo sahihi au kutopata Hadiyth kabisa na hivyo kutumia ijtihadi yake mwenyewe. Ni kwa ajili hii ndio utapata tofauti katika mas-ala tofauti ya Fiqh baina ya Maimaam kwa mfano Abu Haniyfah, Maalik, ash-Shaafi'iy, Ahmad bin Hanbal na wengineo.
Sifa muhimu za Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
Pamoja na vigezo hivyo, vilevile Itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah inasifika kwa sifa muhimu zifuatazo:
- Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake kuwa; Allaah ni mmoja Hana mshirika, Hafanani na chochote.
- Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake juu ya majina na sifa za Allaah Subhanahu wa Ta'ala.
- Kuthibitisha majina na sifa alizozithibitisha Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) kwa nafsi Yake, na zikathibitishwa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bila kubadilishwa, au kuharibiwa, au kufananishwa, au kuhojiwa.
- Iymaan isiyokuwa na shaka kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja wa Allaah na Rasuli Wake, na ndio Rasuli wa mwisho na Imaam wa wacha Allaah na kipenzi cha Allaah.
- Iymaan isiyokuwa na shaka juu yake juu ya nguzo sita za Iymaan.
-
Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake kuwa, moto na pepo ni viumbe vya Allaah vilivyokwishaumbwa, havimaliziki wala kuangamizwa, na kwamba Allaah Ameumba moto na pepo kabla ya viumbe vingine na kuwaumbia watu Wake, kwa mwenye kuamini na kutenda matendo memo Allaah Atamuingiza katika pepo kwa fadhila Zake, na atakaye kufuru Atamuingiza katika moto kwa uadilifu Wake.
- Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake, kwa Waumini watamuona Rabb wao peponi kama ilivyobainishwa na Qur-aan na Sunnah, Allaah Anasema:
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ﴿٢٢﴾إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ﴿٢٣﴾
Nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Rabb wake. [Al-Qiyaamah: 22-23].
Amesema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(إنكم سترون ربكم) رواه البخاري ومسلم
“Hakika nyinyi mtamuona Rabb wenu” [Al-Bukhaariy na Muslim]
- Kuwa na Itikadi ya kuwa haijuzu kumshuhudilia Muislamu mwenzako kuwa ni mtu wa peponi au wa motoni isipokuwa yule ambae Aayah ya Qur-aan imemshuhudilia hivyo, pamoja na kutaraji malipo mema kwa watendao mema, na kutaraji msamaha kwa wenye makosa.
-
Kuamini kuwa wenye madhambi makubwa ni miongoni mwa Ummah wa Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawatoadhibiwa milele motoni pindi wakifa hali ya kuwa wanampwekesha Allaah, hata kama watakuwa hawajatubu, na watakuwa baina ya matakwa ya Allaah na hukmu Yake, akitaka Atawasamehe kwa fadhila Zake, na Akitaka Atawaadhibu motoni kwa uadilifu Wake, kisha Atawatoa kwa huruma Yake na kwa kuombewa na waombezi miongoni mwa waja wake watiifu na kuwaingiza peponi.
-
Hawasimami dhidi ya viongozi wa Kiislamu, muda wa kuwa ni Waislamu na hawaamrishi maasi na kuwazuia Waislamu kutekeleza wajibu wao wa kishari'ah.
-
Wanawapenda Swahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bila kupunguza mapenzi kwao wala kupituka mipaka katika kuwapenda.
-
Wanaamini kuwa, Ukhalifa baada ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni wa Abu Bakr, kisha 'Umar bin Al-Khattwwaab, kisha 'Uthmaan bin ‘Affaan, kisha 'Aliy bin Abi Twaalib.
-
Kuamini alama za Qiyaamah, kama vile kuchomoza kwa Dajjaal, na kushuka kwa Nabii 'Iysaa (‘Alayhis Salaam) na kuchomoza jua kutoka upande wa Magharibi na mengine yaliyobainishwa na Hadiyth sahihi.
Baadhi ya Imaam wa Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah
-
Kiongozi mkuu na Imaam wa kwanza kabisa wa Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah ni Muhammad bin Abdillaah bin ‘Abdil-Mutwalib (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
-
Kisha wanafuatia Makhalifa waongofu, nao ni:
Abuu Bakr As-Swiddiyq
'Umar bin Al-Khatwaab
‘Uthmaan bin ‘Affaan
'Aliy bin Abi Twaalib
-
Kisha wanafuatia Maswahaba watukufu na kisha waliowafuata baada yao ambao wameacha athari kubwa kama:
Abuu Haniyfah An-Nu'maan
Abuu Abdillaah Maalik Bin Anas
Muhammad bin Idriys Ash-Shaafi'iy
Ahmad bin Muhammad bin Hanbal
-
Na wengineo ambao pia wameacha elimu kubwa sana katika Ummah huu kama:
Abuu ‘Abdillaah Muhammad bin Isma’iyl bin Ibraahiym bin Al-Mughiyrah bin Bardizbah Al-Bukhaariy
Abu Al-Husayn Muslim bin Al-Hajjaaj bin Muslim Al-Qushayriyy an-Naysaabuuriyy, Muslim
'Abdullaah bin Mubaarak
Sufyaan Ath-Thawriy
Abuu Al-Faraj, 'Abdur-Rahman bin Ahmad, Ibn Rajab Al-Hanbaliy
Abuu Al-'Abbaas Ahmad bin ‘Abdil-Haliym, Ibn Taymiyah
Muhammad bin Abiy Bakr bin Sa‘ad, Shamsud-Diyn, Abu ‘Abdillaah Al-Zur‘i ad-Dimashqiy Al-Hanbali, Ibn Qayyim Al-Jawziyyah
Muhammad bin Ahmad bin 'Uthmaan bin Qaymaz, Abuu 'Abdillaah Shamsud-Diyn Adh-Dhahabiy
Abuu Al-Fidaa, 'Imadud-Diyn Isma'iyl bin 'Umar, Ibn Kathiyr
Abuu Zakariyya Muhyud-Diyn Yahya bin Sharaf An-Nawawiy
'Al-Haafidhw Shihaabud-Diyn Abul-Fadhwl Ahmad bin ‘Aliy bin Muhammad, Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy
Abuu Ja'afar Ahmad bin Muhammad bin Salaamah bin Salamah 'Abdil-Maalik bin Salamah Al-Azdiy Atw-Twahaawiy
Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab
-
Baadhi ya waliotangulia miaka ya karibuni:
‘Abdul-‘Aziyz bin 'Abdillaah bin Baaz
Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn
Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy
Muhammad bin Amaani Al-Jaamiy
'Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa'diy
Muhammad bin Ibraahiym Aal Ash-Shaykh
-
Baadhi ya waliohai:
Wako wengi kupita kiasi, hawa chini ni baadhi tu:
Swaalih Al-Fawzaan
‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbaad
‘Abdul-‘Aziyz Aal Ash-Shaykh
Na wengi wengine.
Hao ni baadhi tu ya Wanachuoni maarufu wa Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah.
Ama kasoro muulizaji alizotaka kuzijua kuhusu msimamo wa Ahlus Sunnah, tunasema, kasoro si katika msimamo, kwani kama tulivyosoma, huu ni msimamo unaotokana na Qur-aan na Sunnah hivyo hauwezi kuwa na kasoro, bali kasoro ni watu wanaodai wanafuata msimamo huo. Unaweza kukuta wanaojinasibisha na msimamo ndio wenye matatizo kwa kutofuata yale ambayo msimamo na msingi mzima wa mwenendo huo wanaojinasibisha nayo, au kuingiza mambo yasiyokuwemo; kama kumkuta mtu anasema yeye ni Ahlus Sunnah na huku anazusha ya kuzusha katika Dini au msimamo wake huyo mtu unapingana na ‘Aqiydah ya Ahlus Sunnah nay eye ameshikilia kujiita Ahlus Sunnah! Hivyo, tatizo au kasoro ni kwa wale wanaojinasibisha na msimamo na si msimamo wenyewe kuwa na kasoro.
Kwa faida zaidi, soma makala zifuatazo:
'Aqiydah Ya Ahlus Sunnah Wal Jama'ah
'Aqiydah Yetu Ahlus Sunnah Wal Jama'ah
Hii Ndiyo Itikadi Sahihi Ya Kiislamu
Mukhtasari Wa 'Aqiydah Swahiyh Ya Muislamu - 1
Mukhtasari Wa 'Aqiydah Swahiyh Ya Muislamu - 2
‘Aqiydah Ya Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (Aliyefariki 161H)
Wanaopinga Sifa Za Allaah (Ahlul-Bid'ah) Hawana Dalili Za Msingi
Kwa mukhtasari hii ndio Ahlus Sunnah wal Jamaa'ah
Na Allaah Anajua Zaidi