Wazazi Wa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Ni Watu Wa Peponi Au Motoni?

 

SWALI:

Ustadh nilikuwa nataka kuuliza kuhusu baba na mama yake mtume Muhammad (saw) ni watu wa motoni au wa peponi?

  

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu wazazi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakika ni kuwa tunapata Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Niliomba ruhusa kutoka kwa Allaah kumuombea msamaha mamangu, lakini Hakunipatia. Nikamuomba idhini nilizuru kaburi lake (mamangu), Naye Akanipatia ruhusa” (Muslim).

Kukatazwa huku kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwa sababu ya mama yake kutokuwa Muislam. Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha:

Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapokuwa ni jamaa zao, baada ya kwishabainika kuwa hao ni watu wa Motoni” (9: 113).

Ifahamike kuwa baba na mamake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuwa Waislamu nao waliaga dunia katika ukafiri. Ama kuwa wataingia Motoni au Peponi hilo ni la Allaah Aliyetukuka kuwasamehe au kuwaadhibu. Hii si ajabu kwani babake Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) hakuwa Muislamu ndio akaagiziwa:

Wala haikuwa Ibraahiym kumtakia msamaha baba yake ila kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui ya Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym alikuwa mwingi wa kuomba, mnyenyekevu, mvumilivu” (9: 114).

Nabii Ibraahim (‘Alayhis Salaam) anamuambia babake:

Ewe baba yangu! Usimuabudu Shetani. Hakika Shetani ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rehema” (19: 44).

Alipoona babake hasikii alijitenga naye: “Nami najitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Allaah. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi” (19: 48).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share