Skip navigation.
Home kabah

Mwandamo Wa Mwezi, Kila Mji Ufuate Mwezi Unapoonekena Kwao Au Mwandamo Wa Kimataifa?

 

SWALI  

  

Nimesikia kupitia radio times na radio Quran kupitia masheik maarufu wa bakwata wakisema wanao warka uliosambazwa na mufti wa saudia kwamba kila sehemu wafunge kwa kufata mwez wa sehem zao, vipi hamkubaliani na warka huo kuwepo? Ama hamkubalian na mufti huyo kwa sababu zipi? Ukizingatia hapo ndio mahala patakatifu zaidi?

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hili. Ingekuwa vyema kama wewe mwenyewe ungeupata waraka huo kisha ukatutumia nasi tukauona yale yaliyosemwa. Fataawa za Mashaykh wakubwa wakati mwingine zinabadilika kwa sababu moja au nyingine ima kwa kupatiwa maelezo yanayotumwa kwao kwa kwa kubadilika mazingira. Uko waraka wake, aliekuwa Mufti wa Saudi Arabia, Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz wa Sha‘abaan 1392 H (sawa na 1971) unaosema: “… lililo bora zaidi katika mas-ala haya ni kuweka wasaa (uhuru wa kuchagua) katika jambo hili, nako ni kujuzisha kuchukuliwa kauli moja yoyote kati ya kauli mbili (ya kufuata mwandamo wa kitaifa au kimataifa), kulingana na vile wanavyoona wanavyuoni wa nchi inayohusika. Nami nasema hii ndiyo kauli ya kati na kati na ndiyo iliyokusanya dalili na kauli za wenye elimu …” (Majallatul Buhuuuth al-Islaamiyah, Nam. 22, uk. 335).

Kauli hii ya Shaykh haifuatwi wala haitolewi na wenye mrengo mmoja. Nchi za Kenya na Tanzania ndiyo yenye tatizo hili sugu kwani watu wengi ni wenye kufuata dhehebu la Imaam Shaafi‘iy na hivyo hawataki kukaa na wenziwao wenye muelekeo tofauti ili kujadili hilo kielimu.

Je, hao mashekhe maarufu wa Bakwata katika waraka huo walitoa swali aliloulizwa Shaykh Ibn Baaz au walitoa sehemu ya jibu wanayotaka iunge msimamo wao tu? Kwetu sisi tunawaheshimu sana Mashaykh wote wenye kuzingatia na kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na tunawaombea kwa Allaah Aliyetukuka Awasamehe wanapokosea. Tufahamu kuwa Mashaykh nao ni binaadamu huenda wakakosea wakati mmoja au mwingine. Ndio tunampata Imaam Maalik akisema: “Kauli ya mtu mwingine yeyote inaweza kuchukuliwa au kurudishwa kwao wenyewe ila kauli za sahibu wa kaburi hili (yaani Mtume)”.

Kwa kweli tunaona ajabu kwa mashekhe hao wa serikali wanaotoka mbelembele kwenye vyombo vya habari walivyopewa kutumia na kupotosha watu kwa kuchukua kauli hiyo pekee kutoka kwa Shaykh Ibn Baaz lakini wakaacha kufuata yale maelekezo mengine ya Shaykh Ibn Baaz ya kukataza kusoma Khitmah, Mawlid na kuacha kufuata Bid‘ah nyinginezo ambazo hao mashekhe wa serikali wanazifanya na kuzieneza?

Tufahamu kuwa msimamo wa Muislamu yeyote unatakiwa uwe ni kufuata haki na ukweli. Ikiwa Shaykh Ibn Baaz amesema hivyo na kwa ibara yake hapo juu wawaachie Mashaykh wa nchi hiyo waamue, amewapatia Mashaykh wa sehemu zao watazame ukweli na haki. Lakini hata hivyo wapo Mashaykh wengi waliosema kuwa kufuatwe mwandamo wa kimataifa na hiyo ndio kauli ya Jamhuur (wanachuoni wengi). Msimamo huu ndio muono wa madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, Maalik, na Ahmad bin Hanbal. Wengine wenye msimamo huu ni Ibn Taymiyah, Ibn Qudaamah al-Maqdisiy,, ash-Shawkaaniy, Dkt. Yusuf al-Qaradhwaawiy, Dkt. Ahmad Shaakir, Dkt. Wahbah az-Zuhayliy, al-Qaanujiy, ‘Abdur-Rahman al-Juzairiy na pia Sayyid Saabiq. Na kwa upande wa dalili, rai hii ya kufuata mwezi wa kimataifa una nguvu zaidi kuliko kufuata mwezi wa nchi.

Tazama masuala hayo kwenye vitabu vya Fiqh vya kutegemewa kama Fiqhus Sunnah cha Shaykh Sayyid Saabiq, na Swahiyhu Fiqhus Sunnah cha Shaykh Abu Maalik Kamaal bin Sayyid Saalim, utaona kuwa rai yenye nguvu ni ya kufunga kwa kufuata mwezi wa kimataifa popote utakapoonekana Muislam hutakiwa kufunga na si hadi asubiri mwezi wa kutangazwa na Bakwata.

Na Allaah Anajua zaidi