Skip navigation.
Home kabah

Tunaambiwa Wanaofuata Mwezi Wa Kimataifa Wamekosea Na Walipe Swawm Je, Ni Sawa?

 

SWALI   

Napenda kuuliza maswali mawili ambayo yananitatiza katika maelezo tuliyuyapaya kutoka kwa masheikh mbalimbali.

kuna masheikh wenye msimamo wa kufunga/ kufungua kwa kufuata muandamo wa mwezi kitaifa wanasema mwaka huu waliofungua kwa kufuata muandamo wa mwezi kimataifa wamekosea kwani hakuna sehemu yeyote duniani mwezi uliondama siku ya alkhamis,kwa hiyo watu waliokula sikukuu siku ya ijuamaa wamekula ramadhani mchana na walipe na hata wakilipa haitokubaliwa, je hii ni sahihi?

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ni hakika kuwa haya mas-ala tumeyatia u’aswabiyah (kasumba) na ushabiki mpaka tukasahau Uislamu ambao umekuja kuondoa ujahiliya wa kikasumba na kitaifa.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Si katika sisi anayeita watu katika utaifa (kasumba n.k.) …” (Abu Daawuud).

Sisi tunasema ipo misimamo miwili mikuu iliyochukuliwa na wanazuoni wa Kiislamu – msimamo wa kufuata mwandamo wa kitaifa na kimataifa. Hata hivyo msimamo wa mwandamo wa kimataifa ndio wenye dalili za nguvu zaidi lakini hatuwachukulii wenye kufuata mwezi wa kitaifa kuwa funga zao ni batili. Hakika ni kuwa mwenye kujua usawa halisi wa funga na Ibaadah nyingine ni Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) peke Yake. 

Ni ajabu ya kwamba hao unaosema kuwa ni mashekhe wamechukua jukumu la Mwenyezi Mungu la kukubali au kukataa Ibaadah ya mja. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Sema: Enyi waja Wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allaah. Hakika Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (39: 53).

Kisha huu msimamo wa kitaifa unakuaje? Kwa mfano, ikiwa mwezi umeonekana Namanga, Kenya na bahati mbaya au nzuri haukuonekana Namanga ya Tanzania au sehemu nyingine yoyote katika Tanzania, je Waislamu wa Tanzania watafunga? Ikiwa kweli watafunga kama inavyofanyika, kweli watakuwa wamefuata mwezi wa kitaifa au kieneo?

Ajabu ni kuwa, mashekhe hao hao uliowataja, waliwahi kukataa taarifa sahihi za mwezi mara mbili walizoletewa na hivyo kusababisha wa-Tanzania kufunga siku 28 na mwezi kuonekana na hivyo kulipa Swawm zao! Na mifano ni mingi ya upotoshaji wao wa mara kwa mara. Na kwa sababu hizo, ndio utaona leo hii Tanzania, watu wengi wanafuata mwezi wa kimataifa kwa kukosa imani na mashekhe hao.

Na ni mara ngapi umeona hao mashekhe wanapinga ‘Arafah iliyopo Makkah na kuweka ‘Arafah yao na kuadhimisha ‘Iyd Al-Adhwhaa zao tofauti na ulimwengu mzima? 

Soma pia makala hii kwa faida zaidi na uone tegemeo kubwa la wanaofuata mwezi wa kitaifa na uone majibu yake:

Mjadala Wa Mwandamo Wa Mwezi

Na Allaah Anajua zaidi