Yupo Nje Masomoni Hapati Nafasi Ya Kuswali Chuoni, Aswali Swalah Ya Safari?

 

SWALI:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu muumba mbingu na Ardhi, sala na salaam zimshukie Kipenzi chetu Mtume Muhammad SAW. Na sahaba wake na ahli zake. Napenda kuwapongeza watayarishaji wa Web site hii na Allaah inshalla atawalipa kheri. Suala langu ni hili, mimi nimesafiri nje ya nchi yangu, nchi niliyoenda husikii adhana.Na ofisi tunayosoma hamuna muda wa kuruhusiwa kusali hata muda wa mapumziko unaoupata huwezi kusali mana kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume na hakuna sehemu nyengine unayoruhusiwa isipokuwa darasa lako tu, hvyo ninaporudi hotelini ninapokaa ndio huwa nasali safari, kurudi ni saa kumi na nusu.Jee ninavyosali safari siendi kinyume na kama naenda kinyume nifanye nini.

Naomba jawabu tafadhali.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu mwanafunzi nasi tunakuombea kila la kheri katika masomo yako. Hata hivyo hukutufahamisha unasomea wapi, kwani kwa kufanya hivyo ungekuwa umetusahilishia sana kukupatia nasiha muafaka kabisa.

Je, wewe utakuwa nchi hiyo kwa muda gani hukutueleza? Hata hivyo, hilo ulilolieleza si udhuru unaokubalika kisheria. Hakika ni kuwa wewe una fursa nzuri ya kuweza kuswali Swalah ya Adhuhuri bila matatizo. Tufahamu kuwa japokuwa ni bora kwa Muislamu kuswali Swalah zake Msikitini kwa wakati wake lakini kukiwa hakuna budi umepatiwa ruhusa kuswali nyumbani au sehemu nyingine yoyote ile.

Huu ndio uzuri wa Uislamu na pia umuhimu wa Swalah kwa wakati wake. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

"Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu" (An-Nisaa: 103).

Hatudhani katika chuo hicho kutakuwa hakuna fursa yoyote ya kutekeleza hilo au uongozi umekukataza kufanya hivyo. Kwa kuwa hakuna Msikiti na nyumba iko mbali unaweza kuswali Swalah yako sehemu nyingine yoyote, kwa mfano darasani, uwanjani au mahali ambapo una fursa ya kuswali Swalah yako. Hili ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Abu Dharr (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amemnukuu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

"Ardhi yote imefanywa kwangu mimi ni twahara na ni Msikiti (sehemu ya mtu kuswali ndani yake)" (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).

Na katika Hadiyth nyingine Hudhayfah bin al-Yamaani (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amemnukuu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

"Tumefanywa bora kuliko watu wengine katika mambo matatu: Safu zetu zimefanywa katika safu za Malaika, ardhi yote imefanywa kwetu kuwa Msikiti na mchanga wake umefanywa twahara kwetu ikiwa hakuna maji " (Muslim).

Waweza kuswali bila matatizo sehemu yoyote ya ulimwengu bila matatizo yoyote.

Bali wewe unatakiwa uende zaidi ya hapo kwa kujaribu kuzungumza na Waislamu wengine ikiwa wapo hapo mkaweza kusaidiana na kwenda kwenye idara ya chuo na kupeleka maombi yenu ya kupatiwasehemu ya kuswalia, nao wakawapatia chumba hasa cha nyinyi kujumuika na kuswali pamoja. Ukifanya hivyo utakuwa umepata thawabu nyingi zaidi kwani kila atakayejaaliwa kuswali hapo utakuwa ni mwenye kupata thawabu. Muislamu hawi mgeni mahali popote pale kwani ana ndugu zake katika Imani. Toa hofu na fanya bidii na Allaah Aliyetukuka Atakupatia tawfiki inshaAllaah.

Hakikisha unfanya juhudi za kutosha kabla hujafikiria masuala ya kutaka kuswali safari au kuziswali Swalah zote kwa pamoja ukirudi nyumbani. Jitahidi na Allaah Anaziona juhudi za waja Wake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share