Skip navigation.
Home kabah

Mwezi Ulionekana Siku Moja Nchi Nyingine Mapema Zaidi Yetu Je, Tulipe Siku Hiyo?

 

SWALI:

A. aleykum,

Nengependa kupata ufafanuzi wa haya; je wakati tupo mwezi 29 Ramadhani yasemekana baadhi ya maeneo ya NIJERIA? Nimeyapata haya kupitia radio times na radio Quran na pakatolewa ushahidi wa internet juu ya madai hayo. Ikiwa hivyo itathibitika je tutalazimika kuilipa siku hiyo kwa sie tunaefuata mwezi ma kimataifa?

 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya mwezi. Kwa wakati huu hasa katika mataifa ya Tanzania na Kenya kumekuwa na mgogoro wa mwezi baina ya wanazuoni. Majirani wa nchi hizo tayari wametatua mgogoro huo kama vile Uganda, Rwanda na Burundi kwa kufuata Saudi Arabia.

 

Kabla ya kuingilia katika suala lako hilo ni vyema kutoa baadhi ya misimamo ya watu (Waislamu) hasa kwa Tanzania na Kenya ambayo yamezua utata. Inafahamika misimamo mikuu kuhusu suala la mwandamo wa mwezi ni miwili. Nayo ni kama ifuatayo:

 

  • Mwezi wa kimataifa.

 

  • Mwezi wa kwetu (kitaifa).

 

Hii miono imegawanyika kwa kiasi kikubwa kutegemea maeneo wanayokaa Waislamu.

Ama wenye kufuata mwezi wa kwetu (kitaifa) mara nyingi hilo halipatikani hasa kwa wanaoishi katika nchi hizi. Hapa tutatoa baadhi ya mifano:

  • Katika miaka ya themanini, wavuvi waliokuwa wakija katika kisiwa cha Lamu waliuona mwezi wa kuingia mwezi wa Ramadhaan. Mashaykh wa kisharifu Lamu waliukataa wakisema: ‘Kuna watonyi wakaona mwezi?’ (Kuna wavuvi wakaona mwezi?) Suala hili liliwakasirisha jamii ile kuwafanya mpaka sasa kuanzia wakati huo kutosikiliza habari za mwezi kutoka sehemu nyingine mpaka wauone wao wenyewe kwa macho yao. Mwaka huo wale waliokuwa Lamu walifunga siku 28 ikabidi walipe siku moja.

 

  • Muono wa kitaifa pia haujapatikana Kenya kwani Qaadhi mara nyingi hukataa mwezi wa kutoka sehemu wanazoishi Wasomali au bara kufanya watu wafunge siku tofauti. Hili lilitokea mara nyingi katika miaka ya karibu.

 

  • Kuna muono wa kimaeneo ambapo mwezi ukionekana Tanzania Waislamu wa Kenya wafunge pia. Hata hivyo, kuna mwaka ambapo mwezi ulionekana Zanzibar na Qaadhi mkuu wa Kenya akaukataa kabisa.

 

  • Pia lipo tatizo la Waislamu kufuata matamanio yao mbali na kuwa wengi wanasema wanafuata uamuzi wa Qaadhi au Mufti wa Bakwata n.k. Hata hivyo, mwezi ukaonekana kabisa Kenya siku moja na nchi nyingine za Waislamu hasa Saudia lipo pote kubwa linahalifu amri hiyo. Mfano mzuri ni mwaka uliopita (1428 H) katika ‘Iyd al-Adhwhaa wakati Qaadhi mkuu wa Kenya alipotangaza kuwa mwezi umeonekana na ‘Iyd itakuwa tarehe 19 Disemba sawa na Saudia wapo wengi waliopinga na kuswali tarehe 20.

 

Utapata kuwa wapo Waislamu ambao wana muono wa mwezi wa kimataifa lakini kihakika wanafuata mwandamo wa Saudia pekee. Hii inaleta nadharia kuwa msimamo wao sio thabiti kwani mara nyingi zinakuja habari kutoka mataifa wa Waislamu lakini zinakataliwa. Ama kwa hakika wenye msimamo huu wanafaa wafuate mwezi unapothubutu kwa mara ya kwanza kutoka sehemu yoyote ile ye ulimwengu na si mpka tu Saudia wauone au watangaze. Ingawa hata hivyo, Saudia mara nyingi hutokea huwa ndio wa mwanzo kuuona mwezi.

 

Hali ikiwa ni hiyo, ikiwa mtu kweli ana msimamo wa mwandamo wa kimataifa anatakiwa afuate msimamo huo kisawasawa bila kubagua kuonekana na Waislamu kutoka sehemu yoyote ya ulimwengu. Na kwa mfano ikiwa utachelewa kupata habari kama ulivyosikia kuwa NIGERIA waliuona mwezi mwanzo kuliko nchi nyingine za Waislamu. Ikiwa hizo ni taarifa za kweli na zenye kuthibitika (maana hatukuweza kuthibitisha hilo), basi unachotakiwa siku hiyo uilipe baada ya Ramadhaan.

 

Baada ya kusema hayo, yeyote anayefuata mwandamo wa kimataifa anafaa awe ataulizia habari ya sehemu zote hasa zile ambazo huwa na ada ya kuona mwanzo kama NIGERIA, YEMEN, U.A.E. SAUDIA, KUWAIT, na kadhalika. Kuna baadhi ya nchi huwezi kuzihesabu kama LIBYA maana wao wanafuata mahesabu yao wenyewe ya mwezi na hivyo taqriban kila mwaka huwa wanatangaza mwezi mapema kuliko nchi nyingine yoyote ile duniani.

 

Na Allaah Anajua zaidi