Mwanamume Kufanya Kazi Ya Kuonyesha Mitindo Ya Mavazi

 

Mwanamume Kufanya Kazi Ya Kuonyesha Mitindo Ya Mavazi

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Ama baada ya kumshukuru Allaah S.W na kumtakia rehma Alhabib Almustaffa S.A.W. A/alkm ndugu muislamu, naomba kupata jawabu la swali lifuatalo.

 

Ni halali ama ni haramu kwa Mwanamume kufanya kazi ya modelling? Yaani kuonesha mitindo ya mavazi, na mavazi yenyewe ni yale yenye kustiri.

 

A/alkm.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

 

Kawaida ambayo inafaa kufuatwa katika kustarehe na vizuri vyote vikiwa ni katika vyakula, vinywaji au mavazi, ni kujiepusha na kufanya ubadhirifu na majivuno katika matumizi. Israfu ni kukeuka mipaka katika kustarehe na vya halali, na kiburi ni jambo la moyoni zaidi kuliko machoni kwani linahusika na niya ya mtu nacho humfanya mtu kukusudia kujivuna na kujifakhirisha mbele za watu, na Allaah Aliyetukuka Hampendi mtu kama huyo kama isemavyo Qur-aan:

....وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾

Na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha. [Al-Hadiyd: 23].

 

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kuburuta nguo yake kwa majivuno, Allaah Hatomtazama mtu huyo Siku ya Qiyaamah" [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Kwa hiyo, ili Muislamu ajiepushe na kudhaniwa kuwa ni mwenye kiburi, Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kuvaa nguo za fakhari ambazo zitasababisha watu kufakhiriana na kushindana na kujivunia mapambo yao, kama alivyosema katika Hadiyth ifuatayo: "Mwenye kuvaa nguo ya fakhari hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya idhlali kesho Aakhirah, kisha Ataiwashia moto" [Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

 

Baada ya maelezo hayo hapo juu utapata uwiyano na yale yanayofanyika katika kazi ya mtindo wa mavazi ‘modelling’. Nayo ni kama yafuatayo:

 

  • Kunafanyika ubadhirifu (israfu).

  • Kuna uburuzaji wa nguo.

  • Utapata mchanganyiko wa jinsiya (wanaume kwa wanawake).

  • Pia utapata utumiaji wa pombe na muziki (kwa sababu inaonyesha swali lako linahusu mitindo ya mavazi yasiyo ya Kiislam wala yanayoendeshwa kwa nidhamu ya Kiislam).

  • Nguo zenyewe si za kawaida bali ni za upeo wa fakhari.

  • Huenda akaingia katika kiburi kwa kuingia katika mambo yaliyokatazwa.

  • Kutembea kwa wenye kuonyesha hiyo mitindo wakati wa uonyeshaji mitindo ni kwa njia iliyokatazwa. Wanatembea kwa maringo na kujilegeza mwili wao wakiuita mwendo huo ‘mwendo wa paka’, hali ya kuwa Allaah Amekataza watu kutembea hivyo. Tazama Suwrah Luqmaan Aayah 18. Allaah Anasema:

لَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾

 wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye kujivuna mwenye kujifakharisha.

 

 

Na Anasema tena Allaah Aliyetukuka katika Suwrah Al-Israa (Banuu Israaiyl) Aayah ya 37:

وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا ﴿٣٧﴾

Na wala usitembee katika ardhi kwa majivuno. Hakika wewe huwezi kupasua ardhi, na wala huwezi kufikia urefu wa milima.

 

 

Kwa vidokezo na maelezo yaliyo hapo juu, ufanyaji wa kazi hii haukubaliki katika Sheria.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share