Zingatio: Tujiepushe Na Kamari

 

Zingatio: Tujiepushe Na Kamari

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Maisha ya Muislamu daima ni yenye mabadiliko katika hali yoyote ile. Muislamu yeyote yule hatoweza kuishi pekee bila ya kuchanganyika na wenzake na bila ya kwenda huku na kule ili kutafuta njia mbali mbali za kujitafutia rizki za kimaisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kawaamrisha waja Wake waende kutafuta rizki katika Ardhi hii kwa kusema:

 

هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ۖ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ﴿١٥﴾

Yeye Ndiye Aliyeidhalilisha ardhi kwa ajili yenu basi nendeni katika pande zake na kuleni katika riziki Yake, na Kwake kufufuliwa. [Al-Mulk: 15]

 

Hakika kutafuta rizki ni jambo la lazima katika maisha ya Muislamu. Rizki hizo huenda zikachumwa kwa njia za halali au haramu. Miongoni mwa rizki zilizo haramu ni ile inayotokana na kamari.

 

Kamari ni miongoni mwa kazi chafu za Shaytwaan na yampasa Muislamu kujiepusha nayo. Hii ni kwa mujibu wa Qawl ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 90].

 

Tunashuhudia jamii yetu kuzungukwa mno na michezo hii ya kamari. Hufikia hadi kubadili jina ili kuwachanganya Waislamu pamoja na kujihalalishia kazi hiyo chafu.

 

Hivyo, tunawanasihi na kuwakumbusha Waislamu kuzingatia kwamba; mlango wowote unaoelekea kwenye haramu basi Uislamu umeufunga. Hivyo, haifai kucheza kamari wala kujinasibisha na mchezo huo wa shetani. Iwe mchezo huo unachezwa kwa njia ya redio, TV, simu au hata kuvaa fulana yenye kuhamasisha mchezo huo mchafu. Waislamu tunatakiwa kujiepusha kabisa kushuhudia michezo hii michafu na yenye uongo kwa ushahidi wa Qawl ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا ﴿٧٢﴾

Na wale ambao hawashuhudii uongo, na wanapopita kwenye upuuzi hupita kwa heshima. [Al-Furqaan: 72].

 

Vikao vya kamari vinakusanya uongo, dhulma, wasiwasi na hakuna chochote ndani yake ambacho kina faida ya kidini. Hivyo vitendo vyao ni vya uongo, na kuvishuhudia kunamaanisha kuvifanya.

 

Vikao vina adabu zake ndani ya Uislamu. Miongoni mwa adabu alizotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni; "Kuinamisha macho, kutokuwaudhi watu, kutoa salaam, kuamrisha mema na kukataza mabaya na kumuongoza aliyepotea njia". [Imepokewa na al-Bukhaariy]. Nje ya kuta hizo, kikao kitakuwa hakina manufaa yoyote kwa Muislamu na anatakikana ajiepushe nacho, kikiwemo kikao cha kamari.

 

Ndugu zangu Waislamu tuzingatie, je adabu alizozitaja Habiybul Mustwafaa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimo ndani ya vikao vya kamari? ‘balaa’ Bali vikao vya kamari vimekusanya mambo maovu kabisa kama vile; kuwasengenya watu, kuwadhulumu watu, uongo, uzushi na wasiwasi tu.

 

Enyi Waislamu wenzangu, tuzindukane kwani binaadamu tumekuwa na khulka za ajabu kabisa. Vijana wanaharibika katika vikao kama hivyo vya kamari. Wazazi musikubali kuwaacha watoto kukaa karibu kabisa na vikao kama hivyo.

 

Mcheni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika kuwalea watoto kwenye malezi mema yenye faida na wao katika maisha yao ili wafuzu duniani na akhera. Aamiyn.

 

 

Share