Mke Anaposafiri Kikazi Ni Jukumu La Mume Kumhudumia?

 

SWALI:

 

Rehema za Allah ziwashukie hapo mlipo, wana wa Alhidaaya.

Ningependa kushukuru kwa kujibiwa masuala yangu ambayo nimeuliza. Suala langu ni hili ikiwa mke kasafiri kwa safari ya kikazi, na wakati wa kuondoka kwake mume hakuchangia kiasi chochote kwa ajili ya kujikimu mkewe huyo, ijapokuwa alitoa ruhusa na roho ya safari hiyo, jee mume huyo vipi atatimiza wajibu wake wa kumpatia huduma mkewe au amesamehewa hana jukumu la kumpatia huduma (za chakula)? Jee mke huyo akirudi anaweza kumdai mumewe huduma ambazo alizikosa kipindi hicho? 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Mume ana wajibu na jukumu kwa mkewe katika yale yote yaliyobainishwa na sheria ya Kiislamu. Mke anapotaka kusafiri hawezi kufanya hivyo mpaka aruhusiwe na mumewe, ikiwa hataruhusiwa hataweza kusafiri hata ikiwa ni safari ya kazi.

Wakati mke anasafiri ni muhimu kuwe na maelewano kuhusu safari hiyo. Ikiwa wanandoa wamesikilizana kuwa mke atasafiri kwa kuwa ni safari ya kiofisi ofisi yenyewe itakimu masrufu yake na wakaelewana hivyo basi lile jukumu linamuondokea mume. Hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Waislamu wapo katika masharti (waliyosikilkizana)".

Ama ikiwa hakuna masikilizano yoyote baina yao ule msingi wa kisheria unabaki kuwa ni lazima ufuatwe, nao ni uwajibu wa mume kumtazama mkewe kwa masrufu yake ya chakula na mengineyo. Ikiwa mume hakutekeleza hayo atakuwa ni mwenye kufanya makosa na hivyo kupata dhambi kwayo.

Tunapenda kukumbusha hapa kwamba mwanamke haimpasi kusafiri akiwe pekee bali lazima awe na mahram wake. Haya ni makatazo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 ((Mwanamke asisafiri ila awe na mahram wake)) [al-Bukhaariy na Muslim]

Na usimulizi ufuatao tunaona kwamba hata katika kutekeleza ibada ya fardhi imekatazwa, seuze kusafiri kwa ajili ya mambo ya kidunia?

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa awe na mahram yake wala asisafiri mwanamke ila awe na mahram wake pia”. Akasimama mtu mmoja na kuuliza: “Ewe Mtume wa Allaah! Mke wangu ametoka kwenda kuhiji nami nimejiandikisha kwenda jihadi kadhaa”. Alasema: “Nenda ukahiji pamoja na mke wako” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share