Wanawake Kuvaa Swiming Costume (Nguo Za Kuogelea) Pwani Wakiwa Na Wanaume

 

  Wanawake Kuvaa Swiming Costume (Nguo Za Kuogelea) Pwani Wakiwa Na Wanaume

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

 

Swali Langu Nikuhusu Kama Unaolewa Na Family, Na Ukenda Beach Wao Wakaoga Na Swimming Costume Na Wewe Pia Nawe Ukavaa Na Family Mchanganyiko Ya Wake Na Waume Je Unapata Dhambi?  Please Nijibu Kwa Sababau Nipate Kumwambia Dada Yangu. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Mwanzo tufahamu ya kuwa Uislamu umehimiza sana mas-ala ya mazoezi na hasa kuogelea kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza tuwafunze watoto wetu kuogolea, kulenga shabaha na kupanda vipando (farasi, ngamia, punda, gari, na kadhalika).

 

 

Hata hivyo, tufahamu kuwa Uislamu una misingi na kanuni zake kuhusu mambo tofauti. Katika kila jambo ambalo Muislamu anafanya anafaa achunge maadili ya Kiislamu.

 

 

Uislamu katika hilo umemhimiza mwanamke awe ni mwenye kujisitiri kwa kuvaa mavazi ya Kiislamu hasa anapotoka nje na hata akiwa ndani kukiwa na wanaume ambao si maharimu zake basi anafaa ajitande kabisa. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ 

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. [Al-Ahzaab: 59].

 

 

Hakika ni kuwa mavazi ya kuogelea huwa hayana sitara kabisa. Pia tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka hataki wanawake wawe ni wenye kutoka ovyo ovyo kama walivyokuwa wakitoka nje wanawake katika nyakati za ujahili kwa kujirembesha, kuwa uchi au karibu kuwa uchi na mengineo. Ikiwa hapana budi mwanamke atoke nje basi hana budi kuvaa nguo za heshima kinyume na hivyo ataingia katika ujinga. Anasema Aliyetukuka:

 

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ 

Na bakieni majumbani mwenu, na wala msionyeshe mapambo na uzuri kwa ajinabi kujishaua kama zama za ujahili. [Al-Ahzaab: 33]

 

 

Jamaa za mume, hasa wa kiume ni watu ambao kisheria hawafai kuona uchi wako (mwanamke) na uchi mwanamke ni mwili mzima isipokuwa uso na viganja vya mkono. Ni vyema ikiwa mke hana budi kwenda beach basi asiogelee kabisa kwani atakuwa ameruka mipaka iliyowekwa na Allaah Aliyetukuka na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala isiwe beach ya mchanganyiko wa wanawake kwa wanaume ambapo ataona wanaume waliovaa nguo za kuogelea na hivyo kuona maeneo ya uchi yao.

 

 

Tusome makala ifuatayo tuone madhara na ubaya wa kuchanginyikana wanawake na wanaume wasio Maharimu.

 

 

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amsaidie huyo dada yako na sisi sote katika kufuata maagizo ya sheria ya Kiislamu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share