Zingatio: Hatukuletwa Duniani Kucheza

 

Zingatio: Hatukueletwa Duniani Kucheza

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Mafundisho sahihi ya Uislam yanaonesha dhahiri kwamba mwanaadamu alikuwa ni kiumbe cha mwisho kuumbwa, na akaletwa duniani hali ya kuwa kila kitu kishaumbwa kwa ajili yake. Akatunukiwa hadhi ya uongozi wa ulimwengu huu. Hivi sasa wanaadamu wapo kila pembe ya dunia hii, wakiwa mchanganyiko wa rangi na makabila tofauti.

 

 
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakuwaacha tu wanaadamu wakakosa muongozo na malengo ya kuumbwa kwao. Hivyo aliwaleta Rusuli ('Alayhim- salaam) ambao baadhi yao walikuja na maandiko matukufu. Qur-aan ni miongoni mwa maandiko hayo matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ni muongozo wa maneno haya matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Muislamu anaweza kuelewa lengo la kuumbwa na asili ya kuumbwa kwake. Nayo Qur-aan yatueleza kwamba tumeletwa duniani kumuabudu Allaah tu: 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat: 56]
 
 

Kulala na kuamka kwetu, kula, kufanya kazi au mazoezi, kutimiza shahawa, kutembea, kuvaa nguo na mengineyo kadha wa kadha, yote yawe ndani ya taratibu bora kabisa za Uislamu. Kinyume cha kuelewa na kutekeleza maagizo ya aya hiyo juu, ndio tunashindwa kujinasua na matatizo tuliyonayo. Mashaka ambayo yamerudisha nyuma Uislamu na kutuacha tukikosa muelekeo.

 

Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Mwingi wa Rahma Anatuongoza lakini sisi tunakaidi. Yeye ndie Anayetupatia upenyo wa khitilafu za shughuli zetu na Anatupa riziki bila ya kuelewa inatokea wapi [47:7].

 

 

Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameahidi kumnusuru yule ambaye atainusuru dini ya Kiislamu, ikiwa kwa jihaad ya vita, kujitolea kwa da'awa, matendo au matamshi [2:212].

 

 

Kwa masikitiko makubwa, tumedharau muongozo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), tukajichagulia mfumo tuutakao wa maisha. Maisha ambayo yamejaa dhulma, uzinzi, liwaat na kadhalika. Dunia inakaribia kupasuka kwa madhambi yetu. Ghadhabu na laana za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) zinatuteremkia pasi na kutanabahi kwa kufikiri na kuzingatia.

 

Iweje ulimwengu huu, wenye wataalamu na wasomi wa kulla namna, washindwe kuzuia mfumko wa bei duniani? Wanashindwaje kuhimili mikeke ya mitihani ya dhoruba na mitetemeko? Kila tulifanyalo laenda arijojo. Iwapi heshima yetu wanaadamu?

 

Naye Muumba wa Mbingu na Ardhi, Anatujibu kwamba, hii mitihani inayotukumba ni kutokana na chumo la madhambi yetu. Anafanya hivyo, ili tu kutuonjesha adhabu ya baadhi ya ufisadi tunaofanza mchana na usiku. Sasa lengo la hii misukosuko ni nini? Tupate kurudi na kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwani katu hatukuletwa kufanya uharibifu [30:41].

 

 

Share