Tunaomba Du’aa Pamoja Kwa Ajili Ya Mitihani Inafaa?

SWALI:

 

ASALAMU ALEYKUM WARAHMATULLAHY WABARAKATU Mmi ni mwanachuo, huwa tuna kawaida ya kuomba dua ya pamoja inapokaribia kipindi cha mitihani (Dua ya kuanza na kumaliza mitihani) katika jumuiya yetu ya waislamu hapa chuoni. Naomba munifafanulie ili niweze kuijua haki kwani kuna wale wanaona haifai kwani haikuthibiti na wengine wanasema inafaa kwa kusema mbona Mtume s.a.w aliomba mvua?

NAMUOMBA ALLAH S.W. AWAFANYIE WEPESI KATIKA KAZI ZENU ILI MUWEZE KUNIJIBU MAPEMA INSHAALLAH.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea.  

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du’aa ya pamoja. Tunaomba Allaah Aliyetukuka Atuonyeshe haki kama haki na Atupe hima ya kuifuta na Atuonyeshe batili kama batili na Atupe hima ya kuiacha.

 

Mas-ala ya du’aa ni suala muhimu katika Uislamu kwani yamehimizwa sana kwa Aayah na Hadiyth tofauti. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na waja Wangu watakapo kuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka” (2: 186).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Duaa ni ‘Ibaadah, kisha akasoma: Na Mola wenu Mlezi Anasema: Niombeni nitakuitikieni(40: 60)” (at-Tirmidhiy).

 

Duaa iliyo bora ni mtu mwenyewe kumuomba Allaah Aliyetukuka hasa katika nyakati ambazo du’aa hujibiwa. Mfano ni kuinuka usiku na kuswali Tahajjud kisha ukaomba, baina ya Adhana na (Iqaamah) Swalah, wakati unapofunga Swawm, na kadhalika. Na kwa sababu unafanya mtihani maombi yako kwa Allaah Aliyetukuka yatakuwa:

 

“Ee, Allaah Nijaalie nipite mtihani wangu, Ee Allaah nizidishie elimu”.

 

Vile vile du’aa zifuatazo  za Qur-aan na Sunnah anaweza kuomba kila mmoja wenu:  

 

 Katika Qur-aan:

 

 

رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي  وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي  وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي يَفْقَهُوا قَوْلِي

(

Rabbishrah Liy Swadriy Wayassir Liy Amriy Wahlul 'Uqdatam-Mil-Lisaaniy Yafqahuu Qawliy.

Ee Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu, Na unifanyie nyepesi kazi yangu. Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu (Taha 25 – 28) 

 رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا   

 

Rabbi Zidniy 'Ilmaa

Mola wangu nizidishie elimu [Twaaha 114]

Katika Sunnah ni du’aa ambayo mtu anapokabiliwa na jambo gumu:

 

اللّهُـمَّ لا سَـهْلَ إِلاّ ما جَعَلـتَهُ سَهـلاً، وَأَنْتَ تَجْـعَلُ الْحَـزَنَ إِذا شِـئْتَ سَهـْلاً

Allaahumma laa sahla illa maa Ja’latahu sahlan, wa Anta Taj’alul-hazna idhaa shi-ita sahla.

 

“Ee Allah hakuna jepesi ila Ulilolifanya jepesi, Nawe Unalifanya gumu jepesi ukitaka”

 

 

Hilo ndio lililo bora na mtu kufanya bidii kwanza ya kusoma na kisha aombe du’aa na vizuri na bora ni kujiombea mtu mwenyewe na pahali pazuri pa kuomba ni wakati wa kusujudu kwenye Swalah na kabla ya kutoa Salaam. Pia hali hiyo ya kukusanyana kwa ajili ya du’aa, mbali na kuwa haikuthibiti, vilevile inawea kujenga nadharia ya kwamba mimi nitafanya mchezo kisha najua kuwa tutakutana na kuomba du’aa na Allaah Atanijaalia nipite. Ni nadharia ya wengi wafanyao hayo kabla ya mitihani na wengine hawaonekani wakati mwengine wote wa mwaka katika shughuli za Kiislamu za jumuiya lakini wanaonekana siku hiyo kwa sababu wana shida.

 

Kwa hiyo inatakiwa Waislamu wema wafanye juhudi ya kuwaelimisha wenziwao kuwa Allaah Aliyetukuka humsaidia mwenye kujisaidia. Hivyo, pamoja na du’aa ni muhimu kwa kila mmoja asome kwa bidii pamoja na kufanya ‘Ibaadah itakiwavyo.

 

Ama kufananisha jumuiko la kuomba kupita mitihani na du’aa ya mvua si sawa na hayo mawili hayalingani kabisa. Hayafanani kivipi? Hebu tutazame:

 

  1. Kuhusu mvua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliiomba du’aa juu ya Minbar wakati wa khutbah siku ya Ijumaa (hapa si wakati wa Swalah ya mvua, kwani Swalah ya mvua inafanyika nje. Hii ilikuwa ziada ya maombi). Nanyi sijui kama mnamuambia Khatibu siku ya Ijumaa kabla ya mitihani awaombee watoto wa Kiislamu wanaofanya mitihani?

  2. Du’aa ya mvua huwa inafuata baada ya Swalah maalumu ya kuomba hilo. Wakati wa kuomba du’aa kupasi mitihani huwa hatuswali wala hakuna Swalah ya kuomba kupita mitihani.

  3. Swalah na du’aa yake ya mvua hufanyika nje ya mji sio Msikitini ilhali hilo hatufanyi tunapoomba kupita mitihani.

  4. Katika siku ya kuomba pamoja na Swalah ya mvua wale waliohudhuria wanatakiwa wavae nguo zao ndani nje. Sijui hilo linafanywa wakati wa kuomba kupita mitihani.  

 

Kwa hiyo kulinganisha mambo hayo mawili si sawa kabisa.

 

Ingia katika viungo vifutavyo upate maelezo zaidi kuhusu makatazo ya jambo hilo:

 

Kualika Watu Kusoma Qur-aan Kuomba Haja

 

Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?

 

Kusoma Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah na Kuomba Du’aa Baada ya Mihadhara

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share