Mume Mlevi, Mtusi, Anaiba Vitu Vyangu Na Ananipiga Nimeamua Kumfukuza. Je, Nimekosea?

SWALI:

 

As/aleikum, sheikh, mimi nina mume ambaye ni mlevi, mtusi mpigaji, mwizi wa vitu vyangu vya dhahabu, kauza vitu vyangu vyote vya dhahabu, analeta ulevi ndani ya nyumba, nikimkataza anatoa maneno mabaya kwangu na watoto. Nikuwa mja mzito ikawa ananipiga nakuniapiza maapizo mabaya, mpaka akanambia nitakufa juu ya kitanda wakati wa kujifungua. Nimejifungua kwa uperesheni.

Baada ya wiki nimetoka hosp. akaanza tena kunitukana, nimeshamwitia watu kumsema nae ajirekebishe lakini hataki. Nimeamua kumtoa katika nyumba yangu, na nimemuomba anipe talaka hataki. JEE SHEKHE NINI HUKUMU YA NDOA HII? KWA SABABU MIMI SIMTAKI TENA HATA KUMUONA KWA VITENDO VYAKE VIOVU NAOMBA USHAURI WA KISHERIA YA DINI YETU TUKUFU. ASSALAM ALEIKUM.

 

MWISHO WA YALIYO MUHIMU

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu vurugu za mumeo kwako. Hakika, matatizo ya kijamii na kwa wanandoa ni mengi hasa katika jamii yetu.

 

Hata hivyo, hata matatizo na misiba kama hii mara nyingi huwa tunajitakia sisi wenyewe. Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha kuhusu hilo: “Na misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye Anasamehe mengi” [42: 30].

 

Tunajitakia sisi wenyewe kivipi? Hili ni swali zuri na jawabu lake ni kuwa tumeshindwa au kukosa kuchaguana kwa misingi ya kidini na maagizo tuliyopatiwa na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ikiwa mume ana matatizo hayo huenda akawa alikuwa nayo kuanzia kitambo na sio wakati huu wa sasa.

 

Hayo kando, madhara makubwa yanaweza kukupata ikiwa unaishi na mlevi, mtu asiyejali maslahi yako kabisa. Shari'ah inakupatia wewe fursa ya kujivua katika ndoa hiyo lakini kabla ya kufanya hivyo inabidi wewe uitishe kikao ambacho utakuwepo wewe, yeye, mzazi (au wazazi) wako na wake. Katika kikao hicho unatakiwa uelezee yote hayo nao wanaweza kutoa uamuzi ambao unaofaa, ima wa mumeo kupatiwa muda mwingine wa kujirekebisha au kukuacha au kuachishwa. Ikiwa hakuna natija yoyote katika kikao hicho basi itabidi upeleke kesi yako kwa Qaadhi ikiwa yupo katika mji wako au kwa Shaykh muadilifu, yule aliyefungisha nikaah yenu au mwengine. Naye amepatiwa ruhusa kwa maonevu kama hayo uliyoyaeleza kuwaachisha musiwe tena ni mume na mke.

 

Tunakuombea kila la kheri katika mambo yako yote.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share