Kampa Dada Yake Kama Zawadi Aishi Naye Kinyumba Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalam alaykoum,

 

Tafadhali naomba ufafanuzi na jawabu kwa suala langu hili:

 

Kuna mwanamume mmoja asiyejiweza (masikini) aliyempa dada yake kwa mwanamume mwengine, aishi nae kinyumba kama hadiya (zawadi), kwa lugha ya kiarabu ni 'hiba', bila ya kufunga nikah au kutowa mahari yeyote.

 

Na huyu mwanamume aliyepewa huyu dada amesema ni halal yake kwani imeruhusiwa kwa Qur'an na kama ilivyoandikwa, "Maa malakat aymaanikum". Na akatowa mfano wa Sayyidna Ali (radhi ya allahu anhum) aliyetowa mtoto wake msichana na kumpa Sayyidna Omar (radhi ya allahu anhum) kama hadiya (zawadi).

 

Wameishi pamoja zaidi ya mwaka sasa, huyu bibi ni mja mzito na atajifungua wakati wowote. Swali langu ni jee hii hadiya ya kupeana mwanamke inajuzu kwa dini yetu? Jee ni haram au ni halal?

 

Shukran na jazzakumu llahu khairan.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ‘hiba’ kama ulivyoita, ila kwa ibara sahihi tunaweza kuita ‘zinaa ya hila’. Ifahamike kuwa mwanamme hawezi kukaa na mwanamke kwa njia nyingine yoyote mbali na ndoa. Na pia katika Uislamu mwanamke si bidhaa ambayo inaweza kutolewa kama zawadi au hiba. Ndoa katika Uislamu ina masharti yake na yakiwa hayakutimia huwa hakuna ndoa. Masharti yenyewe ni:

 

  1. Kuwepo kwa walii wa mke.

  2. Kukubali kuolewa mwanamke mwenyewe.

  3. Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

  4. Mwanamme kutoa mahari waliyosikilizana na atakayekuwa mkewe.

  5. Mwanamme naye kuridhia kwa ndoa sio kuishi kinyumba.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema yafuatayo kuhusu kuwaweka wanawake kinyumba:

Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa waliopewa Kitabu kabla yenu, mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uasherati wala kuwaweka kinyumba” (5: 5).

 

Ndugu hana haki kabisa hata akiwa masikini kiasi gani kumtoa dada yake ili awekwe na mwanamme mwengine kinyumba kwani hilo ni jambo lililoharamishwa.

 

Ama kuhusu maa malakat aymaanukum (sio ‘aymaanikum’ kama ulivyoandika) ni iliyomiliki mikono yenu ya kuume (yaani watumwa sio watumishi). Sasa huyu dada alikuwa lini mtumwa na je, kakake anaweza kuwa bwanake? Hilo haliwezekani na wala wakati huu hakuna tena utumwa.

 

Kuhusu mfano uliotolewa wa ‘Umar na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhuma) hauingii kabisa kwani ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuoa binti wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiitwa Ummu Kulthuum na wala hakupewa zawadi.

 

Kwa ufupi, ni kuwa hao wenye kukaa kinyumba wanazini na hiyo mimba si ya halali kabisa. Wanapaswa waachane haraka sana na wafanye tawbah ya kweli. Inabidi waambiwe waepukane wasiwe ni wenye kuishi pamoja mpaka huyo mwanamke azae kisha wafanye tawbah ya kweli kweli ndio hapo wanaweza kisheria kuoana. Tufahamu kuwa huyo mtoto hatamrithi mwanamme huyo.

 

Kwa ufupi ni kuwa kufanya hivyo ni haramu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share