Mkwe Anapasa Kuchukua Pesa Ninazompelekea Mama Yangu Kwa Ajili Ya Kuwahudumia Watoto Wetu?

 

Mkwe Anapasa Kuchukua Pesa Ninazompelekea Mama Yangu Kwa Ajili Ya Kuwahudumia Watoto Wetu?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Mimi Na Mume Wangu Tunaishi Nchi Ya Nje Watoto Tumemuachia Mamangu. Nilimuacha Mtoto Wa Kwanza Na Mkwe Wangu Nikenda Kusoma. Nilipata Habari Na Mimi Mwenye Kumsikia Akilalamika Anataka Apewe Pesa Kwa Kumuangalia Mtoto Lakini Kwa Bahati Mbaya Hali Zetu Ki Fedha Zilikua Mbaya, Mama Huyo Alikua Akitoa Maneno Mabaya Ya Chuki Dhidi Yetu Ikafika Hadi Mwisho Akatwambia Tutoke Kwenye Nyumba Yake Kama Hatuna Pesa. Nilipata Safari Na Nilijifungua Mtoto Wa Pili Nkamwachia Mamangu Watoto Bila Pesa Za Kutumia Lakini Mamangu Akasema Hakuna Neno Atawaangalia Watoto. Sasa Mimi Na Mume Wangu Tumepata Kazi Alhamdullillah Tumemwambia Mama Awe Akichukua Pesa Za Rent Ya Mume Wangu Ziwe Za Watoto. Ingawa Si Pesa Za Haja Lakini Abudget. Shida Imekuja Mama Wa Mume Wangu Zile Pesa Anazochukua Mamangu Za Watoto Na Yeye Pia Akataka Sehemu Asema Ni Za Mwanawe. Jee Tunayo Haki Yakumkataza Asichukue.

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Mwanzo ni muhimu tuelewe kuwa kila upande ni lazima umuelewe mwenziwe wala isiwe ni mas-ala ya kuvutana baina ya pande mbili.

 

 

Ilikuwa si vyema kwa mkweo kutoa maneno yasiyofaa bali kwa umri wake alikuwa atumie busara hata kutaka anachotaka. Na kwenu ilikuwa ni makosa kumuachia mzigo mama ambaye amepata shida ya kuwalea watoto aliowalea kisha mkamuachia mtoto bila masurufu yoyote yale. Ilikuwa mfanye juhudi mbali na kuwa mnasoma ili mpeleke japokuwa kitu kidogo cha kumsaidia.

 

 

Pia inafaa tufahamu kuwa mama ana haki katika mali ya mtoto wake, bali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Swahaba mmoja kuwa yeye na mali yake ni ya mzazi wake. Na katika haki mama ana haki zaidi kwa mtoto wake kuliko baba. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth: Imepokewa na Abi Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu.) ambaye amesema:

 

 

"Alikuja mtu kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Mjumbe wa Allaah! Ni nani mwenye haki zaidi miongoni mwa watu kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Babako" [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Na katika riwaya nyingine: "Ee Mjumbe wa Allaah! Nani ana haki zaidi kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mamako, kisha mamako, kisha mamako, kisha babako, kisha wale walio karibu, wale walio karibu nawe kijamaa”.

 

 

Hadiyth hii inatuonyesha kuwa mama ana sehemu tatu ziada za kufanyia wema na watoto kuliko baba. Na hii ni sababu ya shida na uzito anaopata wa kubeba mimba, kisha kuzaa na baadae kunyonyesha. Al-Qurtubiy amesema: “Mama anastahiki wema na ihsani zaidi kuliko baba, na amemtangulia baba katika mashindano hayo”.

 

 

Hivyo, mkweo ana haki katika mali ya mwanawe na inatakiwa wewe umsaidie mumeo katika kumtii mamake. Hakika ni kuwa kushindwa kwake kumtii, na kuelekea katika kumuasi kutamwingiza yeye katika moto wa Jahanamu. Ushauri wetu wa dhati kwako ni kuwa katika ijara ya nyumba inayopatikana jaalieni kuwa sehemu mnampelekea mamako kwa ajili ya watoto na nyingine mkweo kwa ajili ya kuunga kizazi na wema wa mtoto kwa mamake. Hata kama katika kazi zenu mnapata kidogo wekeni akiba na mpelekeni mama wa mumeo na ndio mtakapobarikiwa katika mambo na kazi zenu. 

 

 

Tunawaombea kila la kheri na fanaka.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share