Mashairi: Dini Imekamilika

 

‘Abdallaah Bin Eifan,

(Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

(1) Salaam zangu narusha, tena zinatoka mbali,
      wakati umeshakwisha, wa kuchezewa akili,
      dini imetuonyesha, kila kitu kwa dalili,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(2) Mungu Keshabainisha, Katowa Yake kauli,
      hatuwezi kuzidisha, chochote kiwe cha pili,
      hatuwezi kufupisha, yaloandikwa awali,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(3) Mtume katufundisha, katuonyesha ukweli,
      mengi ametusomesha, yalotoka kwa Jalali,
      hapana kubadilisha, Mungu Hatayakubali,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha

 

(4) Imekamilika dini, hakuna tena badili,
      ukweli umebaini, dini moja sio mbili,
      Imesema Qur'aani, maneno yote kamili,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(5) Swala tano Ameweka, zote hizo tuziswali,
      zakaa kufaridhika, iwe tohara ya mali,
      saumu kulazimika, iwe tohara ya mwili,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(6) Hija ni ya tano nguzo, pesa ziwe za halali,
      kwa yule mwenye uwezo, na mwenye rasilmali,
      yote hayo maelezo, dini imeyasajili,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(7) Wanaopenda nyongeza, hao watu majahili,
      wakati wanapoteza, mambo yao ni batili,
      swali ukiwauliza, wanashindwa kujadili,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(8) Khitma wanaisoma, kwa maiti iwasili,
      nini mbele watasema, Mungu Wakimkabili,
      ikigeuka kilema, kuitibu ni muhali,
      Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(9) Na lini zitasimama, za maulidi shughuli,
       lini watu watakoma, mambo hayana asili,
       hii ni moja alama, ya dini kuitapeli,
       Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(10) Jirekebishe mapema, nakuomba tafadhali,
        usiibebe lawama, ya wale mabaradhuli,
        nawaonea huruma, akhera moto mkali,
        Dini yetu ni kamili, Mungu Amebainisha.

 

(11) Mungu Atatunusuru, Anajuwa yetu hali,
       Atumulikie Nuru, viumbe kila mahali,
       wasomaji nashukuru, naomba mnihimili,
       DINI YETU NI KAMILI, MUNGU AMEBAINISHA.

 

Share