Uchawi Upo? Na Vipi Kujitibu?

 

 Uchawi Upo? Na Vipi Kujitibu?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum ndugu zangu! Nimefurahi sana kupata website hii sababu ya mafunzo na faida nyingi nilopata ndani yake.suali langu ni: jee sihri ya exist, yaani mtu anaweza kufanyiwa sihri? Na kama ipo mtu atajua vipi kama amefanyiwa sihri? Na yafaa kufanya dawa kujitopoa??? Naomba munifafanulie suali langu. Shukran.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Sihri iko na kuweko kwa sihri haimaanishi kuwa ni halali kama ambavyo tembo lipo, nguruwe wapo lakini kutumia vitu hivyo ni haramu. Hata Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa Sallam) aliwahi kufanyiwa sihri na Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa al-Labiyb bin ‘Aaswim na mabinti zake. Ndio ikawa sababu ya kuteremshwa kwa Mu‘awadhatayn (Suwrah Al-Falaq na An-Naas). Kwa kirefu tafadhali angalia tafsiri ya Suwrah hizi mbili katika vitabu vya tafsiri vikubwa kama Tasiyr ya Ibnu Kathiyr.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ

Na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah;[Al-Baqarah: 102]

 

Zipo ishara au alama za kuonyesha kuwa mtu amefanyiwa sihri na zipo aina tofauti za sihri. Kwa mfano, kuna sihri ya mtu kuwa mgonjwa daima. Mtu huyu akienda hospitali na kupimwa anaonekana kuwa yupo sawa kabisa.

 

Kuna zile za mtu kusikia sauti bila kumuona mtu mwenyewe, au kuona vitu ambavyo havipo, na ile ya uenda wazimu.

 

Kujipotoa zipo aina mbili – moja kati ya hizo haifai na nyengine yafaa.

 

Ile aina ambayo haifai ni kutoa uchawi kwa uchawi, kupunga, kwenda katika mizimu na kadhalika.

 

Na ile ambayo inafaa ni kwa Ruqya (Poza kutokana na Qur-aan na Sunnah). Kuisoma Qur-aan na Adhkaar au Du’aa zilizosuniwa na kupokewa kutoka kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) na watangu wema.

 

Hivyo, kufanya dawa kujitopoa (kujizungua) yafaa lakini katika njia ambazo ni za halali.

 

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share