Kuhudhuria Mwaliko Unaochanganyika Mazuri, Maovu na Bid-ah Inafaa?

 

Kuhudhuria Mwaliko Unaochanganyika Mazuri, Maovu na Bid-ah Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam ‘Alaykum Warahmatullah.

 

Naumba kuuliza suala ambalo linanitatiza siku nyingi bila ya kupata ufumbuzi. Jee mfano umepata mualiko siku mbili, moja inafanywa vizuri na siku ya pili huchanganya na yasiokuwemo.  Jee nini wajibu wetu kwa sisi waalikwa?

 

Mara nyengine hutokea haya ndani ya familia, maziko yetu, harusi zetu zote huwa na mitazamo kama hii ya kuchanganya mambo, hivyo nini haki zetu juu ya kushiriki jambo hili?

 

 

Jazaka Allah Khayra

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika hili ni tatizo kubwa ambalo linatukabili katika jamii yetu kuchanganya yaliyo mazuri na mabaya. Inastaajabisha unapoona leo kunafanywa mambo yanayolingana na Sharia na siku ifuatayo hata utashangaa huku unauliza je, hawa ni wale wale au ni wengine?

 

 

Mwanzo katika hayo ikiwa wewe ni jamaa na wale wanaofanya harusi au matanga uwe ni mwenye kuwaelezea namna nzuri ya kutekeleza hayo katika Dini yetu. Kufuata kwao au kutofuata ni juu yao lakini wewe jitoe katika dhimma hiyo ya kueleza na kuwanasihi. Ikiwa watasikiliza itakuwa kheri na ikiwa hawakuchukua nasaha basi dhambi ni kwao.

 

 

Unalopaswa kufanya ni kuwa ikiwa harusi au mwaliko mwengine wowote kwa shughuli unakwenda sambamba na Uislamu utakwenda kuitikia mwaliko huo lakini ikiwa siku ya pili watafanya yao ya upuuzi na kinyume cha Dini utawaelezea tena na hutakwenda katika mwaliko huo. Hii ni kwa mujibu wa Aayah inayosema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚوَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maaidah: 2].

 

Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho:

 

Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bid-ah Ni Dhambi?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share