Mashairi: Khitmah
Khitmah
‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)
Naanza Bismillaahi, salaamu zipokeeni,
Hakika nimefurahi, kuyaandika maoni,
Sikuja kuwakebehi, nawaomba samahani,
Khitma ni jambo geni, kusoma hawakuwahi
Hawakuwahi kusoma, maswahaba wa zamani.
Na Mtume hakusema, dalili tuonyesheni,
Qur-aani kuisoma, haifiki kaburini,
Khitma ni jambo geni, hawakuwahi kusoma.
Bid’aa ina madhambi, ya kukutia motoni,
Husomwa kwenye ukumbi, wanasoma Qur-aani,
Eti hivyo ni maombi, Kumuomba Rahmani,
Khitma ni jambo geni, ni mbali na rambirambi.
Ni kinyume na sheria, na sunna ya yetu dini,
Tunazidi kupotea, faida yake sioni,
Anazidi kuchochea, adui wetu shetani,
Khitma ni jambo geni, Qur-aani kusomea.
Ndugu acheni uzushi, kudanganya Waumini,
Mwahangaika bilashi, na kuwakera jirani,
Na watu kuwashawishi, kuwatia ujingani,
Khitma ni jambo geni, kusoma kwenye mazishi.
Khitma ni upotofu, ndugu mpo hatarini,
Tusiwe kama vipofu, kujiunga makundini,
Na kusoma misahafu, kwa maiti ndio nini?
Khitma ni jambo geni, na dini yetu tukufu.
Maiti hufaidika, dua sana ziombeni,
Mtoleeni sadaka, ziende kwa masikini,
Pia fanyeni haraka, mlipe yake madeni,
Khitma ni jambo geni, bure mnahangaika.
Amali inakatika, hana chake duniani,
Dunia anaondoka, na amali mikononi,
Kaburini akifika, ni mwanzo wa mtihani,
Khitma ni jambo geni, uzushi wa vibaraka.
Ukiotesha nafaka, nyingi sana mashambani,
Mavuno yatakufika, utafurahi moyoni,
Na mema ni kadhalika, utayavuna mwishoni,
Khitma ni jambo geni, tena haina Baraka.
Jitahidi fanya mema, akiba yenye thamani,
Usingojee khitima, ikuokoe shimoni,
Tena waambie mapema, “Nikifa msisomeni.”
Khitma ni jambo geni, ni jambo lenye lawama.
Yatatufika mauti, kama si leo mwakani,
Tuwaombee maiti, pepo iwe maskani,
Tamati nafunga beti, nakimbilia kazini,
KHITMA ni jambo geni, BID’AA na usaliti.