Haki Hii Haki Gani Mbele Ya Allaah?

 

Haki Hii Gani Mbele Ya Allaah?

 

Bint Ahmadah

 

Alhidaaya.com

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatusimulia moja ya visa vilivyomo katika Qur-aan Tukufu:

 

وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا وَصَدَّقَتْ بِكَلِمَاتِ رَبِّهَا وَكُتُبِهِ وَكَانَتْ مِنَ الْقَانِتِينَ﴿١٢﴾

 Na Maryam binti wa ‘Imraan ambaye amehifadhi tupu yake, Tukampulizia humo (katika nguo yake) kupitia kwa Ruwh Wetu (Jibriyl), na akasadikisha Maneno ya Rabb wake, na Vitabu Vyake, na akawa miongoni mwa watiifu na wanyenyekevu. [at-Tahriym: 12]

 

Je kusimama mbele ya vyombo vya habari, au kwenye mikutano ya hadhara, kwa msichana na kudai haki zinazoitwa za binaadamu kwa lengo la kutembea utupu au kujifananisha na mwanaume ndio haki aliyoipigania Bibi Maryam?

 

Dada yangu, haki hiyo waitaka hali ya kuwa ni kichwa kitupu kisichomuelewa Rabb Mlezi utaipata wapi? Ikiwa aayah za Allaah wazigeuza unavyozitaka wewe, salama utaipata wapi? Elewa ya kwamba, hao waliotaka haki ya kweli basi walijitoa kiroho, kiimani, kisubra na kinguvu kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Pitia kurasa za Bibi Fatwimah, Mama 'Aaishah na Bibi Summayyah (Radhwiya Allaahu ‘Anhunna) muone namna walivyokuwa na msimamo madhubuti wa iymaan ya Uislamu. Hawakupigania haki hizo kwa ajili ya matamanio yao binafsi na msukumo wa watu fulani (makafiri na wanafiki).

 

Waislamu hawatakiwi kushirikiana na makafiri kwenye masuala ya kuzipinda kanuni za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama hayo ya haki za binaadamu. Wao ndio wafanyao njama mbali mbali za kuwapotosha Waislamu katika kila upande kama hili suala la kudai haki za wanawake ambalo wao wamelivalia njuga.

 

Lengo lao kuu si jengine ila kuwaelekeza njia nyengine Waislam wauone Uislam ni mgumu usiokwenda na wakati kabisa. Wanatufanyia hila kwa nia ya kwamba Uislam uonekane unawakandamiza wanawake kudai haki yao ya kupanda majukwaani kwenye mambo ya anasa. Anasa zinazohusu utembeaji utupu na uimbaji. Hali ya kuwa Uislam umekataza sauti ya mwanamke kusikikana nje ya mipaka, na imefanananishwa sauti hiyo mfano wa sauti ya punda.

 

Je wanawake tupo tayari kuwa sawa na mapunda kwa kufananishwa na kitendo hicho ambacho Allaah Amekikataza? Tukiona makafiri wa kike wakisimama juu ya majukwaa na wakifanya wao wana haki ya kusema kila kitu hata kama sivyo, na wewe dada yangu Muislam unataka kuwaiga wao wanachokifanya. Si vyema kufanya kila ulionalo, pambanua mambo, na awali ya yote 'tafakari kabla ya athari'.

 

Tambuwa ya kwamba hayo si ya kuiga kwa Muislam wa kweli wa kiimani na kivitendo. Haitokuwa na maana utakaposimama mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Uislam wa kuchovya jina tu wakati vitendo huna kitu. Haki hizi zipaniwazo sio haki tunazozitaka, bali ni mabalaa ndio tunayoyaomba yatufike kutokana na maasi hayo. Kisha tunakaa vikao na kusugua vichwa kujadiliana matatizo ya dunia. Matatizo haya yanatokana na nini kama kiumbe kuacha kutafakari ukubwa wa Aliyetuumba? Hatutafakari tumemkosa nini Allaah?

 

Waliopita nyuma kama Qawm 'Aad waliangamizwa kwa upepo tu kutokana na maasi waliyotenda. Mioyo yao ilifanana na hao wanawake wanaodai haki zao zisizoeleweka mbele ya Rabb Mlezi. Hawakujali ujumbe wa Nabiy Huwd (‘Alayhis-salaam). Qur-aan inatueleza ya kwamba Qawm Huwd waliangamizwa kwa upepo mkali, upepo uliowangoa watu hao mfano wa mti unavyongolewa mzima mzima kutoka ardhini:

 

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُّسْتَمِرٍّ ﴿١٩﴾تَنزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُّنقَعِرٍ ﴿٢٠﴾فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٢١﴾

Hakika Sisi Tumewapelekea upepo mbaya wa sauti kali na baridi kali katika siku ya nuhsi yenye kuendelea mfululizo. Unawang’oa watu kama kwamba vigogo vya mtende vilong’olewa. Basi vipi ilikuwa adhabu Yangu na maonyo Yangu? [Al-Qamar: 19-21]

 

Je na sisi hatuyaoni majanga yote yanayotupata? Juzi Indonesia, jana India, kesho kutwa Tanzania. Tunawaiga Qawm Huud iliyolinganiwa miaka nenda miaka rudi lakini bado hawakuelewa kitu. Leo tuna miaka 1400 ya kushushwa Qur-aan, tunaipa kisogo huku tukijifunza kuimba nyimbo na kutingisha miili mbele ya majukwaa. Tupambanue athari za matendo yetu, tusije kufikwa na mitihani kama hiyo mikubwa mikubwa.

 

Hatutafika pahala kwa kusimama majukwaani tukidai kuwa ndio tunatetea haki zetu wanawake. Na kwa hakika, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Habadilishi nyoyo za watu hadi wao wenyewe wawe tayari kubadilishika.

 

Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anavyosema: 

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ

Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. [Ar-Ra'd: 11].

 

Huo ndio uhuru na demokrasia Aliotuwekea Rabb wetu. Tupo huru kumuasi asubuhi na mchana, lakini tuelewe khatima yetu itakuwa mbaya mno:

 

وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾

 Na Allaah Akiwakusudia watu adhabu, basi hakuna wa kuirudisha. Nao hawana mlinzi yeyote ghairi Yake. [Ar-Ra'd: 11].

 

Tujitahidi kurejea kwa Mola wetu kikweli na tulete toba iliyo ya kweli na tuache yale yote Rabb Aliyoyakataza.

 

 

 

Share