Vipi Kumshukuru Allaah Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika

 

Vipi Kumshukuru Allaah Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalaam Aleikum,

 

Kwanza sina budi na kumshukuru Allah Subhabana wa Ta'aalaa aloniwezesha kunifikisha siku nyengine ili niweze kuwasiliana na nyinyi.

 

Pili sina budi na kukushukurini kwa majibu na maelekezo yenu mema na nasema ahsnteni. Wazee wa zamani wanasema uliza ujinga upate uerevu, na mimi nimeuliza na nimepata maelekezo mema nasema ahsanteni.

 

Ama ibada zangu zote ninazozifanya nafanya kwa "Allaah", na shida zangu zote nazielekeza kwake kwa kuamini kuwa yeye ndie mfumbuzi pekee, na hakuna mwengine. Na ndio maana nikasema rakaa zangu za mwanzo 2 baada ya salamu husoma yale majina yake 99 kwa kumshukuru na neema na ukarimu wake. Labda nikueleze kwanini nafanya hivyo?  Usingizi ni kufa, maana ukilala roho huondoka kwa uwezo Allaah, hukurejeshea tena roho yako na ukajiona imeshaondoka tu kitandani, sasa hapa ndipo ninapomshukuru Allaah kwa yafutayo:-

 

1-kunijaalia uzingizi mnono na kunirejeshea roho yangu tena, navuta pumzi bila taabu, nimenyanyua mikono yangu inakwenda juu a miguu yangu inatembea vizuri, macho yanaona almurdi viungo vyangu vyote vinafanya kazi sawa, basi hapo ndipo niposhukuru kwa ufalme.

 

2-kunijaalia kunilete katika umati huu wa Muhammed ukiwa ndio umati bora na umati wa mwisho, pasina  ulemavu wowote wa kiwili wili.

 

3-Kunifikisha huu umri niliofikia siku ya leo, nikikumbuka wenzangu wangapi wameshaondoka na kutangulia mbele ya haki na kuwacha kila kitu nyuma, wakiwemo Watoto, wajukuu, wazee, waume wao wapenzi,

 

4-Akanijaalia anakipa mume mwenye imani, mapenzi na mashikiano mazuri, na akatufungulia kizazi kiliokuwa kitulivu, tukatia harusi zao na kushuhudia vizazi vyao (Alhamdullillah).

 

5-Mimi mwenyewe akanijaalia kibarua chenye mafanikio mema, kibarua ambacho kinaniwezesha kuyatatua matatizo yangu. Basi kwa kufikiria hayo, mimi ndio huleta hizo rakaa mbili na majina yake Allah kwa kumshukuru kwa hayo na mengi mengi.

 

Kumbe nilikuwa nakosea? Namuomba Allaah anisamehe kwani nimetenda hayo bila kujua na kwa kipindi kirefu sana.

 

Sasa hebu nifahamishe njia gani ya kuweza kumshukuru Allah kwa hizi neema zake? Kusali nasali, Qur-aani nasoma kila nikimaliza msahafu naanza tena, ambazo hukusanya na kufanya ni hitma kwa wazee wangu na kuzihitimisha kila tarehe 27 Ramadhwaan ambazo wakati mwingi nina kua nin hitma 4.

 

Naomba kuelelimishwa, na Allaah Atujaalie kila tunamkosea atusamehe, kwani yeye ni mwingi wa msamaha kwa majina yake matukufu 99 kwa kumshukuru kwa neema na ukaramu wake.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya-Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa neema hii ya kuona ndugu zetu mmo katika jitihada kubwa ya kujifunza mengi katika Dini yenu, khaswa Dada zetu ambao ni muhimu sana kwao kujifunza mafunzo sahihi ili waweze kuwapa watoto wetu wa Kiislamu msingi bora kabisa wa elimu sahihi ya dini yao iwafae katika maisha yao ya duniani na Aakhirah.

 

 

Hakika Ne'ema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) ni nyingi sana hazihesabiki kama Alivyotaja Mwenyewe mara mbili katika Qur-aan:

 وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾

“Na Akakupeni kila mnachomuomba. Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika insani ni mwingi wa dhulma, mwingi wa kukufuru akasoye shukurani.” [Ibraahiym: 34] 

 

Vile vile:

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٨﴾

Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika Allaah bila shaka ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nahl:18]

 

Kutokana na hayo, utatambua kwamba kwa vovote  tutakavyomshukuru Allaah ('Azza wa Jalla), hatutaweza kutimiza shukurani Kwake kutokana na wingi wa neema Zake kama Anavosema: 

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

Na wachache miongoni mwa waja Wangu ni wenye kushukuru.[Sabaa: 13]

 

Wasiomshukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hakika wanakosa faida kubwa kwani Allaah ('Azza wa Jalla)  Ametangaza kuwa kila mja anapomshukuru Humzidishia neema hizo:

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ 

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu)... [Ibraahiym: 7]

 

Na hakika hivyo unavyofanya ni dalili ya iymaan kubwa kwamba unatambua neema za Rabb wako na uko katika jitihada ya kumshukuru kwa kuzikumbuka neema Zake hizo,  kwani kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Taa'alaa) ni kutumia kila chema Alichojaaliwa nacho mtu. Mfano Allaah ('Azza wa Jalla) Akikujaalia mwili mzuri basi inapasa kutumia viungo vyake kwa yale yatakayomridhisha.  Akikujaalia masikio yaliyo salama basi uyatumie kwa kusikilizia yale tu Yanayomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Akikujaalia  macho basi yatumie kutazama yale yanayomridhisha Allaah ('Azza wa Jalla) tu. Na hali kadhaalika kwa viungo vinginevyo.   

 

 

Na ikiwa ni neema ya mali basi pia ni kuitumia kwa yale yatakayomridhisha kama kutoa sadaka na kadhalika.

 

Ikiwa ni neema ya kujaaliwa kizazi basi kuitumia neema hiyo kwa kuwapa malezi bora watoto wako waongoke katika Dini yao.

 

Ikiwa ni neema ya kujaaliwa mume mwema, basi ni kumtii mume wako amri zake na kutimiza wajibu wako kwake.

 

Ikiwa ni neema ya elimu basi uitumie kwa kuifundisha elimu hiyo kwa wenzako.

 

Ikiwa neema ya kujaaliwa rizki basi itunze hiyo rizki bila ya kuifanyia israaf na kadhalika.

 

Amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotoka kwa ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa):

 

((نعمتان مغبون فيهما كثير من الناس  الصحة والفراغ)) البخاري

Ne'ema mbili zimeghafilikiwa na watu wengi; siha na faragha [wakati])) [Al-Buhaariy]

 

Tunapotambua kuwa hatuwezi kuzihesabu neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) haina maana kwamba ndio tuache kumshukuru au tumshukuru kidogo tu, bali tunaweza kujitahidi kumshukuru kwa njia nyingi tukimuomba Atupokelee shukurani zetu. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuacha kutufundisha namna ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kama tutakavyoelezea.

 

Kwanza tutambue kuwa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kunaweza kuwa kwa kukiri moyoni, kutamka shukurani na kwa matendo. Na mafundisho mengi tumeyapata katika Sunnah ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) machache ni kama yafuatayo:

 

 

1-Kila unapojaaliwa neema yoyote ile, fanya sajdah moja inayoitwa 'Sajdatu-shukr', na sio kuswali Rakaa mbili kama wengi wanavyofikiria kuwa kuna Swalaah inayoitwa Swalaatu-shukr.

 

 

2-Katika nyiradi za kila siku asubuhi ukisema du'aa hii ifuatayo utakuwa umetekeleza shukurani ya siku nzima, na ukiisoma jioni utakuwa umetekeleza shukurani ya usiku mzima:

 

اللّهُـمَّ ما أَصْبَـَحَ بي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

Allaahumma maa aswbaha biy min ni’-matiy aw biahadim min Khalqika faminka Wahdaka laa shariyka Laka, falakal-Hamdu walakash-shukru

 

Ee Allaah, sikuamka na neema yoyote au kati ya kiumbe Chako chochote, na neema ila inatoka Kwako hali ya kuwa peke Yako Huna mshirika, ni Zako  Himdi na ni Zako shukurani. [Abu Daawuwd (4/318) [5073], An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [7]. Ibn As-Sunniy [41], Ibn Hibbaan “Mawaarid” [2361] na isnaad yake ameipa daraja ya Hasan Ibn Baaz (رحمه الله) katika Tuhfat Al-Akhyaar (Uk. 24)]

 

 

3-Amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 ((أفضل الذكر لا اله إلا الله، وافضل الدعاء: الحمد لله))   رواه الترمذي حديث حسن

Dhikr bora kabisa ni Laa ilaaha illa Allaah  na du'aa bora kabisa ni Alhamdulillah)) [At-Tirmidhiy hadiyth hasan]

 

 

4-Hadiyth ya ibn 'Umar kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth ya Al-Qudsiyy:

 

إن عبدًا من عباد الله قال: يا رب، لك الحمد كما ينبغي لجلال وجهك وعظيم سلطانك، فعضلت بالملكين فلم يدريا كيف يكتبانها، فصعدا إلى السماء فقالا يا رب، إن عبدا قد قال مقالة لا ندري كيف نكتبها، قال الله  وهو أعلم بما قال عبده : ماذا قال عبدي؟ قالا يا رب إنه قد قال: يا رب لك الحمد كما ينبغي لجلال وجهك وعظيم سلطانك. فقال الله لهما: اكتباها كما قال عبدي حتى يلقاني فأجزيه بها -   إبن ماجه

Mja katika waja wa Allaah alisema: “Ee, Rabb wangu! Zako wewe tu Himdi  Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Ujalali wa Wajihi Wako na Utukufu wa Usultani Wako.”  Malaika wawili walibabaika hawakujua vipi waandike maneno hayo (jinsi alivyomtukuza utukufu wa Rabb wake) Wakaenda kwa Allaah wakasema: Ee Rabb wetu! Hakika mja wako kasema aliyoyasema na wala hatujui vipi tuyaandike. Akasema Allaah   Kwani kasema nini mja wangu? (Na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anajua aliyoyasema mja Wake bila ya Malaika kumwelezea) Wakasema amesema: “Ee, Rabb wangu! Zako wewe tu Himdi  Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Ujalali wa Wajihi Wako na Utukufu wa Usultani Wako.” Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Akasema: “Yaandikeni kama alivyosema mja Wangu mpaka atakaponikuta (siku ya malipo) basi nitampa jazaa yake kwa hayo (aliyoyasema).”  [Ibn Maajah 2:1249]

 

Kusoma kwako Qur-aan na kukhitimisha kisha kuanza tena na kuendelea hivyo hivyo pia ni mojawapo ya njia ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa. Lakini makosa unayofanya ni kukusanya hizo khitma siku ya tarehe 27 ya Ramadhaan kwa niya ya kuwombea wazazi wako. Hakuna dalili katika Shariy’ah kwamba thawabu za kusoma Qur-aan zinamfikia maiti, bali unaweze kuwafanyia wema wazazi waliofariki ni kuwatolea sadaka, kuwafanyia Hajj ikiwa hawakujaaliwa kutekeleza, au kuwafanyia ‘Umrah na mema mengineyo kwa niya yao na In Shaa Allaah thawabu zitawafikia.

 

Kusoma majina ya Allaah 99 hakuna ubaya lakini sio kuyasoma kwa niya ya kumshukuru, kwani kila jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) lina Sifa fulani, kwa hiyo unaweza kuyatumia kwa kumuomba jambo fulani kutokana kulingana na haja zako.  Mfano ukitaka Akughufurie madhambi utasema 'Yaa Ghafuwr', ukitaka Akusamehe utasema 'Yaa 'Afuww' ukitaka Akuruzuku utasema 'Yaa Razzaaq', ukitaka kumshukuru utasema 'Ya Shakuer", 'Yaa Hamiyd' na kadhalika. Inakupasa uwe na ujuzi wa maana ya Majina Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Sifa Zake ndipo utaweza kuyatumia inavyopasa.

 

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share