Kufunga Ndoa Kwa Njia Ya Simu, Inafaa Bila ya Walii?

SWALI:

Assalaam Aleikum Warahmatulllah Wabarakatuh Mungu awajaze khery kwa kazi yenu ya kutuelimisha. Ameen! Suali langu naulizia kwa niaba ya rafiki yangu. Aliolewa akaachika, hii ni ndoa yake ya pili.

Ameolewa kwa simu, coz wako nchi mbali mbali.Yaani alipigiwa simu na mchumbake akiwa na kadhi, na mashahidi upande wa mume, Kadhi akamuuliza ikiwa amekubali kuolewa na huyo mume, akakubali. Wakaozeshwa.

Kusoma katika jawabu mliyojibu hapa lazima kuwe na walii wa mke,na hapo hakukuweko walii wake kwani wazazi wake walifariki. Hakukuweko mtu yoyote upande wa mke. Jee nikah hii yaswihi kisheria? Nawaomba munijibu kwa haraka kwani mume ataka mke aende huko aliko kwa haraka. Shukran wa Jazakumullahu alf khayra


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa kwa njia ya simu. Hakika ni kuwa ndoa katika Uislamu ina kanuni zake na masharti yake. Miongoni mwa masharti yake ni yafuatayo:

  1. Kukubali kwa mume kuingia katika mafungamano ya kindoa.
  2. Kupatikana kwa mashahidi wawili waadilifu.
  3. Kuwepo kwa walii wa mke.
  4. Kukubali mwanamke kwa ndoa hiyo.
  5. Kusomwa kwa khutbah.
  6. Mume kulipa mahari waliyokubaliana.

Kulingana na maelezo yako ni kuwa mwanamke hana wazazi kwani wote waliaga dunia. Tufahamu kuwa walii anakuwa ni baba na wala sio mama, ikiwa hayuko atashika hatamu hizo babu (upande wa baba). Ikiwa hawapo basi hatamu hizo atashika ami yake (kakake baba), nduguye shakiki, au mtoto wake wa kiume. Swali ambalo tungependa kuuliza je, huyu mwenye kuolewa hana watu wote hao tuliwataja hapo juu kama mawalii? Ikiwa jamaa zake wote hao hawapo basi Qaadhi tayari ni walii wake na ndoa ni sahihi.

Lakini ikiwa jamaa zake wapo kwa nini hakuwaambia? Je, aliwaambia wakakataa au alikuwa anaogopa kuwaambia? Uislamu umetupatia njia na suluhisho katika kila hali. Ikiwa jamaa hao walikataa basi Qaadhi ana uwezo kuwaita ikiwa mwanamke amekubali kuolewa na mume huyo. Ikiwa jamaa zake hao hawana hoja yoyote kwa nini wanakataa hapo Qaadhi atawaozesha lakini ikiwa wanakataa kwa sababu maalumu kama mume haswali, maadili yake si mazuri basi pia Qaadhi hatochukua jukumu la kuwaozesha.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share